Iran yasema ina haki ya kujilinda baada ya shambulio la Israel kuwaua wanajeshi wawili

Israel ilitekeleza kile ilichokitaja kuwa "mashambulizi yaliyo sahihi" dhidi ya maeneo ya kijeshi nchini Iran.

Muhtasari

  • Wanajeshi wawili wa Iran waliouawa walikuwa sehemu ya kundi la kijeshi linalolinda mipaka
  • CAF yaiadhibu timu ya soka ya Libya kwa mechi iliyofutwa dhidi ya Nigeria
  • Mataifa ya Kiarabu yalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran
  • Beyoncé awaomba Wamarekani kumuunga mkono Kamala Harris
  • Mashambulizi dhidi ya Iran yanaashiria huenda Israel imezingatia onyo la Marekani
  • Zaidi ya watu 300 wakamatwa kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi Msumbiji
  • Iran imelipa gharama ya mashambulizi ya hivi karibuni - msemaji wa jeshi la Israel
  • Iran yarejelea safari za ndege baada ya shambulio la Israel
  • Biden aliionya Israel kuepuka maeneo ya nyuklia na mafuta ya Iran
  • Katika picha: Muonekano wa anga ya Iran baada ya shambulio la Israel la usiku kucha
  • Marekani yatoa wito kwa Iran kutolipiza kisasi
  • Iran inasema Israel ilishambulia kambi zake za kijeshi
  • Mashambulio dhidi ya malengo ya kijeshi ya Iran yamekamilika - jeshi la Israel
  • Iran yafunga anga zake
  • Shambulio la Israel dhidi ya Iran: Tunachojua kufikia sasa
  • Israel yafanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran

Moja kwa moja

Ambia Hirsi & Peter Mwangangi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo haya ya mubashara. Kwaheri.

  2. Wanajeshi wawili wa Iran waliouawa walikuwa sehemu ya kikosi cha kulinda mipaka

    Maafisa wawili wa Iran waliuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran; wote wawili walikuwa askari wa jeshi la Iran, sio Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

    Tofauti na IRGC, jeshi la Iran - linalojulikana kama Artesh - kwa ujumla haliogopi wala kuchukiwa na Wairan wengi, kwani jukumu lake ni kulinda mipaka ya Iran.

    Walinzi wa Mapinduzi, hata hivyo, wana jukumu kubwa katika masuala ya kisiasa na kiuchumi ya Iran, ambayo ni zaidi ya kazi za kijeshi

    Wanashiriki kikamilifu katika operesheni za nje ya nchi kuanzia Yemen hadi Levant, inayopakana na Israel, na walikabiliana vikali na maandamano ya kitaifa katika miaka ya hivi karibuni.

    Mohammad Mehdi Shahrokhifar alikuwa mmoja wa maafisa wawili wa jeshi la Iran waliouawa katika mashambulizi ya Israel.

    Chanzo cha picha, Hamshahri Newspaper

    Maelezo ya picha, Mohammad Mehdi Shahrokhifar alikuwa mmoja wa maafisa wawili wa jeshi la Iran waliouawa katika mashambulizi ya Israel.

    IRGC ina nguvu kubwa ndani ya Iran, na wanachama wanachukua majukumu yenye ushawishi katika serikali.

    Wamejikita zaidi katika miradi mikubwa ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na miradi ya mafuta na gesi hadi ujenzi wa barabara, jambo ambalo limechochea malalamiko ya umma dhidi yao baada ya kubainika kuwa wanaendekeza rushwa na ukiritimba wa rasilimali.

    Meja Hamzeh Jahandideh wa Jeshi la Iran pia aliuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran

    Chanzo cha picha, Hamshahri Newspaper

    Maelezo ya picha, Meja Hamzeh Jahandideh wa Jeshi la Iran pia aliuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran
  3. CAF yaiadhibu timu ya soka ya Libya kwa mechi iliyofutwa dhidi ya Nigeria

    Nembo ya CAF

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limetangaza uamuzi wake kuhusu mchezo uliofutwa kati ya Libya na Nigeria wa kufuzu kwa michuano ya AFCON mwaka 2025.

    CAF imelikuta Shirikisho la kandanda la Libya kuwa na kosa la kukiuka kifungu cha 31 cha kanuni za Kombe la Mataifa bingwa ya Afrika pamoja na vifungu 82 na 151 vya kanuni za nidhamu za CAF.

    Mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa tarehe 15 Oktoba 2024 mjini Benghazi ilikumbwa na utata kufuatia kuchelewa kwa timu ya Nigeria kwa saa 16 baada ya kuwasili nchini Libya. Hii ni baada ya timu hiyo kuelekezwa kutua katika mji wa Al-Aqrab ulio takriban kilomita 230 kutoka Benghazi ambapo ndio mji ambao mechi hiyo ingechezwa.

    Mechi hiyo sasa imefutwa, na timu ya Nigeria imepewa pointi zote tatu pamoja na mabao matatu.

    Shirikisho la Soka la Libya pia limeamrishwa kulipa faini ya $50,000, ambazo zinafaa kulipwa ndani ya siku 60 baada ya kutolewa kwa taarifa ya uamuzi huo.

    Uamuzi huo wa CAF unatokea siku chache baada ya rais wake, Patrice Motsepe, kusema kuwa shirika hilo limejitolea kuwajibika katika masuala kama hayo.

    Uamuzi huo unazima matumaini ya Libya ya kufuzu kwasababu wana pointi 1 pekee baada ya kucheza mechi nne, huku Nigeria, ambao waliibuka nambari mbili katika mashindano yaliyopita, wakiwa na pointi 10 na wanakaribia kufuzu kwa mashindano hayo ya soka ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili.

  4. Israel yaishambulia Iran, na kuzua onyo kutoka nchi nyingi kimataifa - nini kinaendelea?

    Israel yaishambulia Iran:Israel ilitekeleza kile ilichokitaja kuwa "mashambulizi yaliyo sahihi" dhidi ya maeneo ya kijeshi nchini Iran, ikisema ilikuwa ikijibu "mashambulizi ya mara kwa mara ya miezi kadhaa kutoka Iran". Jibu la Israel lilikuwa likitarajiwa kutekelezwa baada ya shambulio la makombora la Iran mnamo tarehe 1 Oktoba.

    Jibu la Iran: Iran imesema ilifanikiwa kuzuia mashambulizi katika kambi zake za kijeshi na kwamba kulikuwa na "uharibifu mdogo". Jeshi la Iran limesema wanajeshi wake wawili waliuawa, kwa mujibu wa shirika la habari la Iran IRNA. Ikijibu mashambulizi ya Israel, wizara ya mambo ya nje ya Iran ilisema Iran "ina haki na wajibu wa kujilinda".

    Taarifa hizi zimepokewaje kimataifa? Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar zimelaani mashambulizi hayo na kuonya dhidi ya mzozo kuzidi kuwa mkubwa. Ikulu ya White House ya Marekani imesema inachukulia shambulizi la Israel kama "hatua ya kujilinda", na afisa mmoja mkuu wa Marekani ameitaka Iran kutolipiza kisasi.

    Maelezo zaidi:

  5. Mataifa ya Kiarabu yalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran

    Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Qatar na Misri zimetoa kauli zao kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yaliyofanyika usiku kucha.

    Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) unasema unalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran na kusisitiza kuhusu umuhimu wa "kujizuia na kufanya maamuzi kwa kuzingatia kuzuia hatua zinazoweza kutanua mgogoro uwe mkubwa ".

    Saudi Arabia pia inalaani mashambulizi hayo, ikielezea kuwa ni ukiukaji wa "sheria na kanuni za kimataifa", na kuwataka "wahusika wote kujizuia kabisa na kupunguza hatua zinazoweza kufanya mzozo uwe mkubwa zaidi".

    Qatar imesema "inalaani vikali" mashambulizi ya Israel, na kuyataja kama "uvunjaji ulio wazi" wa sheria za kimataifa na kuwataka "wahusika wote kujizuia".

    Misri inasema ina hofu kubwa kuhusu kuendelea kwa mizozo katika eneo la Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran, na inalaani hatua zote zinazotishia usalama na utulivu wa kikanda.

    Maelezo zaidi:

  6. Beyoncé awaomba Wamarekani kumuunga mkono Kamala Harris

    Beyoncé

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wagombea wa urais wa Marekani Kamala Harris na Donald Trump walipeleka kampeni zao tofauti katika jimbo la Texas siku ya Ijumaa.

    Texas haijamuunga mkono rais kupitia chama cha Democratic tangu mwaka 1976, na Trump wa chama cha Republican ana imani kubwa ya kunyakua ushindi katika jimbo hili.

    Mwimbaji nyota wa Marekani Beyoncé alipanda jukwaani katika mkutano wa kampeni wa Kamala Harris mjini Houston, Texas, sio kwa ajili ya kutumbuiza lakini kujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza katika kipindi hiki muhimu cha uchaguzi kumuunga mkono mgombea huyo wa urais kupitia chama cha Democratic.

    Beyoncé, ambaye ni mzaliwa wa Houston, alishangiliwa na umati wa watu 30,000 waliohudhuria mkutano huo uliokuwa na mada kuu ya ‘haki ya utoaji mimba’, akiwa pamoja na msanii mwenzake Kelly Rowland ambao wote zamani walikuwa wanachama wa kundi la Destiny's Child.

    Badala ya kuimba, alihutubia umati kwa dakika kadhaa, akisema hakuwepo hapo kama mtu mashuhuri au mwanasiasa, lakini kama mama.

    "Uhuru wako ni haki yako uliyopewa na Mungu, ni haki yako ya kibinadamu," alisema.

    Kisha akamtambulisha Harris, ambaye aliingia jukwaani huku wimbo wa "Freedom" ukicheza, ambao umeonekana kuwa wimbo wake wa kampeni na ambao umetoka kwa albamu ya Beyoncé ya mwaka 2016 kwa jina "Lemonade."

    Beyoncé alimkumbatia makamu huyo wa rais kwa muda mrefu kabla ya kuondoka.

    Soma pia:

  7. Mashambulizi dhidi ya Iran yanaashiria huenda Israel imezingatia onyo la Marekani

    Marekani, mojawapo ya washirika wa karibu wa Israel, inasema shambulio la Jumamosi dhidi ya Iran lilikuwa "zoezi la kujilinda"

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Marekani, mojawapo ya washirika wa karibu wa Israel, inasema shambulio la Jumamosi dhidi ya Iran lilikuwa "zoezi la kujilinda"

    Mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yamekuwa yakitarajiwa tangu Iran iliporusha karibu makombora 200 dhidi ya Israel karibu mwezi mmoja uliopita.

    Katika taarifa iliyotangaza kuwa operesheni hiyo inaendelea siku ya Jumamosi, msemaji wa jeshi la Israel alisema Israel ina "haki na wajibu" wa kujibu.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimethibitisha kuwa milipuko imesikika katika eneo la magharibi mwa Tehran.

    Lakini bado haijabainika wazi kuhusu maeneo yaliyolengwa na iwapo Israel imefanikiwa kuyashambulia kwa ufasaha.

    Pentagon (makao makuu ya jeshi la Marekani) imetoa taarifa ikisema kwamba Marekani ilifahamishwa kuhusu mipango ya Israel kabla ya kutekelezwa kwake, na kwamba Marekani haikushiriki katika operesheni hiyo.

    Hiyo ni hatua muhimu katika juhudi za Washington za kujaribu kuzuia mzozo kati ya Israel na Iran kuzidi kuongezeka na kuwa makabiliano ambayo yanaweza kugeuka kuwa vita.

    Marekani pia itakuwa inasubiri hali itulie ili kubaini kuwa mashambulizi ya Israel yalilenga tu maeneo ya kijeshi au yalivuka mipaka na kujumuisha vituo vya mpango wa nyuklia wa Iran - jambo ambalo linaweza kusababisha Tehran kulipiza kisasi.

    Kwa sasa - kutokana na ushahidi mdogo uliopo ni kwamba - Israel inaweza kuwa imezingatia onyo la Washington na kukosa kutekeleza baadhi ya mipango yake ambapo ilitaka kusababisha maumivu makali kwa Iran.

    Maelezo zaidi:

  8. Zaidi ya watu 300 wakamatwa kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi Msumbiji

    Msumbiji

    Chanzo cha picha, Screen Grab

    Polisi nchini Msumbiji wamewakamata zaidi ya watu 300 wakati wa maandamano baada ya chama tawala cha Frelimo kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wenye utata uliofanyika wiki mbili zilizopita.

    Kulikuwa na maandamano na ghasia katika miji kadhaa nchini humo Alhamisi usiku kufuatia tangazo hilo, baada ya mgombea mkuu wa upinzani Venancio Mondlane kutoa madai ya udanganyifu katika upigaji kura - jambo ambalo pia liliripotiwa na waangalizi huru wa uchaguzi.

    Hali ya utulivu imerejea nchini Msumbiji baada ya maandamano hayo ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

    Polisi walithibitisha kuwakamatwa takriban watu 370 kote nchini kufuatia makabiliano na waandamanaji na watu wanaodaiwa kupora mali.

    Angalau mtu mmoja alithibitishwa kufariki. Uchaguzi huo umeongeza utawala wa miaka 49 wa chama cha Frelimo na kumchagua mgombea wake Daniel Chapo kuwa rais.

    Kiongozi wa upinzani Vanencio Mondlane alipata asilimia 20 ya kura, na ameitisha maandamano ya siku 25 kuadhimisha mauaji ya maafisa wawili wa upande wa upinzani.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Shambulio la Israel dhidi ya Iran: Taarifa za hivi punde

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ikiwa ndio mwanzo unajiunga nasi haya ndio matukio yanayojiri:

    • Israel inasema imekamilisha "mashambulio maalum" nchini Iran usiku kucha, ikilenga kambi za kijeshi magharibi na kusini magharibi mwa Tehran - kulingana na shirika la habari la Iran.
    • Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vinasema kuwa mashambulizi hayo hayajasababisha uharibifu wowote - Mwandishi wa BBC Idhaa ya Kiajemi Bahman Kalbasi anaelezea hili ni jibu la kihistoria kutoka kwa Iran baada ya mashambulizi kama hayo.
    • Rais wa Marekani Joe Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris wamefahamishwa kuhusu shambulio hilo, Pentagon inasema Marekani ilifahamishwa kuhusu mipango ya Israel lakini haikuhusika.
    • Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer anasema Iran haipaswi kulipiza kisasi mashambulizi ya Israel, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari huko Samoa
    • Milipuko pia iliripotiwa nchini Syria, kulingana na runinga ya serikali. Wanajeshi wa Israel hawajatoa maoni yoyote.
  10. Iran imelipa gharama ya mashambulizi ya hivi karibuni - msemaji wa jeshi la Israel

    Daniel Hagari

    Chanzo cha picha, IDF

    Maelezo ya picha, Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Daniel Hagari

    Karibu tena kwa matangazo haya ya moja kwa moja.

    Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Daniel Hagari anasema Iran "imelipia gharama" kwa mashambulizi yake ya hivi majuzi dhidi ya Israel.

    Anasema Israel ilifanya "mashambulio sahihi na yaliyolenga shabaha katika maeneo tofauti nchini Iran".

    Malengo haya yalijumuisha vituo vya kutengeneza makombora, maeneo ya kurusha makombora kutoka ardhini na uwezo mwingine wa angani, anasema.

    Anasema Israel ilichagua maeneo hayo miongoni mwa "maeneo makubwa yanayolengwa", na kwamba huenda "ikuchagua shabaha za ziada kutoka kwayo na kuzishambulia ikiwa itahitajika".

    "Huu ni ujumbe wazi - wale wanaotishia Taifa la Israel watalipa gharama kubwa," anaongeza.

  11. Iran yarejelea safari za ndege baada ya shambulio la Israel

    Ripoti zinaashiria kuwa Iran iko tayari kurejesha safari za ndege baada ya mashambulizi ya Israel kwenye maeneo kadhaa ya kijeshi nchini humo.

    Shirika la Usafiri wa Anga la Iran limetangaza kuwa safari za ndege "zitarejelea kama kawaida kutoka 09:00 saa za ndani (06:30 BST).

    Hapo awali, tuliripoti kwamba Iran imefunga anga zake.

    Tunavuta pumzi kidogo tutaendelea baadaye na matangazo haya. Endelea kuwa nasi.

  12. Biden aliionya Israel kuepuka maeneo ya nyuklia na mafuta ya Iran

    Utawala wa Biden umesema Israel ina haki ya kujilinda na kujibu mashambulizi ya Iran mapema mwezi huu.

    Lakini rais aliiambia Israel kuwa hataunga mkono shambulio linalolenga vituo vya nyuklia vya Iran kwa kuhofia kwamba linaweza kusababisha kuongezeka kwa mzozo huo unaozidi kufukuta.

    Pia alisisitiza kuwa Marekani haitaunga mkono shambulio la Israel dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Iran.

    "Kama ningelikuwa katika hali yao [Israel], ningekuwa nikifikiria kuhusu njia nyingine badala ya kushambulia maeneo ya mafuta ya Iran," alisema tarehe 4 Oktoba.

    Mwezi huu aliitaka Israel kuwa sawia katika kukabiliana na mashambulizi kutoka Iran.

    Israel imesema mashambulizi yanayofanyika yanalenga kijeshi nchini Iran.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Katika picha: Muonekano wa anga ya Iran baada ya shambulio la usiku kucha la Israel

    Siku imeanza kwa msukosuko katika mji mkuu wa Iran Tehran, kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel.

    Ni vigumu kubainisha ukubwa wa uharibifu, lakini picha chache za anga za jiji hilo zinaashiria kuwa hakuna jambo lolote lisilo la kawaida.

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

  14. Marekani yatoa wito kwa Iran kutolipiza kisasi

    Marekani imeitaka Iran kutolipiza kisasi mashambulizi ya hivi punde ya Israel dhidi yake.

    "Iwapo Iran itaamua kujibu kwa mara nyingine, tutakuwa tayari, na hatua hiyo itakuwa na madhara kwa Iran kwa mara nyingine," taarifa ya maafisa wakuu wa utawala ilisema.

    Iliongeza kuwa Marekani haitaki kuona hilo likitokea. "Hii inapaswa kuwa mwisho wa makabiliano haya ya moja kwa moja kati ya Israel na Iran," taarifa hiyo ilisema.

    Pia iliongeza kuwa Washington iko tayari "kuongoza juhudi za kuhitimisha vita vya Lebanon" na kujaribu kufikia usitishaji mapigano nchini Lebanon na Gaza, pamoja na kurudishwa kwa mateka wa Israel.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Iran inasema Israel ilishambulia kambi zake za kijeshi

    Hapo awali Israel ilisema mashambulizi yake yalilenga shabaha za kijeshi nchini Iran, na sasa Tehran inaonekana kuthibitisha hilo.

    Vikosi vya ulinzi wa anga vya Iran vimesema katika taarifa yake kwamba kambi katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam zilishambuliwa.

    Vilisema mashambulizi hayo yamezuiliwa kwa mafanikio lakini kulikuwa na "uharibifu mdogo" katika baadhi ya maeneo.

    Dalili za mapema zinaweza kuashiria kuwa Iran inajaribu kupunguza uwezekano wa kuendelea kwa mzozo huo, mtaalam anasema

  16. Habari za hivi punde, Mashambulio dhidi ya malengo ya kijeshi ya Iran yamekamilika - jeshi la Israel

    Vikosi vya ulinzi vya Israel vinasema kuwa mashambulizi dhidi ya maeneo yanayolengwa na jeshi la Iran yamekamilika.

    "Muda mfupi uliopita, IDF imekamilisha mashambulio dhidi ya malengo ya kijeshi katika maeneo kadhaa nchini Iran," ilisema taarifa.

    "Ndege zetu zimerejea nyumbani salama."

  17. Iran yafunga anga zake

    Iran imefunga anga zake kufuatia mashambulizi ya Israel, Reuters inaripoti, ikinukuu shirika la habari la nchi hiyo Irna.

    Nchi hiyo imesitisha safari zote za ndege hadi ilani nyingine itakapotolewa, msemaji wa Shirika la Usafiri wa Anga la Iran aliiambia Irna.

    Wakati huo huo Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amezungumza na mwenzake wa Israel, Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant, kwa mujibu wa maafisa wawili wa ulinzi waliozungumza na kituo cha CBS News, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani.

  18. Shambulio la Israel dhidi ya Iran: Tunachojua kufikia sasa

    xx

    Chanzo cha picha, reu

    • Israel imethibitisha kufanya "mashambulizi dhidi ya ngome za kijeshi nchini Iran". Haijabainika ni maeneo gani yaliyolengwa na kiwango cha uharibifu hakijulikani.
    • Hapo awali Marekani iliionya Israel kutoshambulia maeneo ya nyuklia na mafuta ambayo yanaweza kuzua mzozo mkubwa katika eneo hilo.
    • Mashambulizi hayo yanakuja baada ya Iran kurusha takribani makombora 200 ya balestiki dhidi ya Israel mapema mwezi huu. Israel ilikuwa imesema italipiza kisasi lakini haikueleza kwa undani ni lini itafanya hivyo.
    • Iran ilifanya mashambulizi dhidi ya Israel kama hatua ya kulipiza kisasi mauaji kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh, kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah na kamanda wa operesheni wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran Brigedia Generali Abbas Nilforoushan.
    • Kufikia sasa, vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimepuuza mashambulizi hayo, jambo ambalo wataalam wanaimbia BBC ni jibu la kawaida Iran baada ya matukio kama hayo. Lakini, wataalam wanaonya, hali inaweza kubadilika ikiwa ripoti za uharibifu mkubwa au vifo zitaibuka.
    • Milipuko pia imeripotiwa nchini Syria lakini Israel haijadai kuhusika na mashambulizi hayo.
    • Vikosi vya ulinzi wa anga vya Syria vilinasa makombora na kuyaangusha, kulingana na Reuters huku shirika la habari ya AFP, likinukuu vyombo vya habari vya serikali ya Syria.
    • Marekani haikuhusika katika shambulio hilo, kulingana na Pentagon. Ikulu ya White House iliitaja shambulio hilo kuwa "zoezi la kujilinda".
    • Rais wa Marekani Joe Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris wamefahamishwa kuhusu shambulio hilo wanafuatilia matukio hayo.
  19. Israel yafanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Israel imefanya mashambulizi kadhaa ya anga dhidi ya Iran mapema Jumamosi, kujibu kile jeshi lake linakiita "miezi ya mfululizo wa mashambulizi " kutoka Tehran na washirika wake.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema kuwa linafanya "mashambulizi mahususi dhidi ya malengo ya kijeshi" nchini Iran, ambayo inaishutumu kwa "kuishambulia Israel" tangu tarehe 7 Oktoba 2023.

    Uthibitisho wa IDF wa kuishambulia Iran ulifuatia ripoti za awali za vyombo vya habari vya Iran kuhusu milipuko kadhaa ndani na karibu na mji mkuu, Tehran.

    Inakuja baada ya Tehran kurusha takriban makombora 200 ya balistiki kuelekea Israel tarehe 1 Oktoba, katika kile nchi hiyo ilisema ni kulipiza kisasi mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas katika ardhi ya Iran mwezi Julai.

    Msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari, alisema Israel ina "haki na wajibu" wa kujilinda na "uwezo wake wa kujihami na kushambulia" "umehamasishwa kikamilifu".

    Marekani, mojawapo ya washirika wa karibu wa Israel, ilisema shambulia la Jumamosi dhidi ya Iran ni "zoezi la kujilinda".

    Maelezo zaidi:

  20. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja.

    Ikiwa ndio mwanzo unajiunga nasi, jiji la Tehran limeamkia milipuko huku jeshi la Israel likisema kuwa linafanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya malengo ya kijeshi. Tutakufahamisha yote yanayojiri huko katika matangazo hayo ya moja kwa moja.