Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Seneti ya Marekani kupiga kura ya kumdhibiti Trump kuhusu Venezuela

Siku chache zimepita baada ya vikosi vya Marekani kumkamata Rais wa Venezuela Nicolas Maduro katika shambulio la kijeshi lililotokea Caracas.

Muhtasari

Moja kwa moja

Mariam Mjahid & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

  2. Rais wa Ujerumani asema Marekani inaharibu utaratibu wa dunia

    Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amekosoa vikali sera ya kigeni ya Marekani chini ya Rais Donald Trump na kuhimiza ulimwengu kutoruhusu utaratibu wa dunia usambaratike na kuwa "sehemu ya wanyang'anyi" ambapo wasio waaminifu huchukua wanachotaka.

    Katika matamshi makali yasiyo ya kawaida, ambayo yalionekana kurejelea vitendo kama vile kuondolewa madarakani kwa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro mwishoni mwa wiki, waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje amesema demokrasia ya dunia inashambuliwa kuliko wakati mwingine wowote.

    Ingawa rais wa Ujerumani kwa kiasi kikubwa hana mamlaka makubwa kisiasa, maneno yake yana uzito fulani na ana uhuru zaidi wa kutoa maoni kuliko wanasiasa.

    Steinmeier amesema tabia ya Marekani inawakilisha mgawanyiko wa kihistoria.

    "Kuna kuvunjika kwa maadili ya mshirika wetu muhimu zaidi, Marekani, ambayo ilisaidia kujenga utaratibu huu wa dunia," Steinmeier amesema katika hotuba yake katika kongamano la Jumatano.

    "Ni kuhusu kuizuia dunia isigeuke kuwa sehemu la wanyang'anyi, ambapo wasio na adabu huchukua chochote wanachotaka, ambapo maeneo au nchi hutendewa kama mali ya mataifa machache makubwa," amesema.

    Uingiliaji kati ulio wazi unahitajika katika hali za kutishia na nchi kama vile Brazil na India lazima zishawishike kulinda utaratibu wa dunia, amesema.

  3. Maandamano yafanyika Marekani baada ya mwanamke kuuawa na afisa wa uhamiaji

    Maandamano yamefanyika huko Minneapolis, Marekani baada ya mwanamke mmoja kupigwa risasi na kuuawa na afisa wa uhamiaji.

    Mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Renee Nicole Good, mwenye umri wa miaka 37, alipigwa risasi wakati maafisa wa uhamiaji na forodha (ICE) wakilikaribia gari lake na yeye kuamua kuliondosha, milio miwili ya risasi imesikika.

    Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani Kristi Noem amesema Good alikuwa "akiwafuatilia na kuwazuia" maafisa na kujaribu "kutumia gari lake kama silaha."

    Lakini Baraza la Jiji la Minneapolis limesema Good alikuwa "akiwasaidia majirani zake" alipopigwa risasi na kuuawa Jumatano asubuhi.

    Mamia ya maafisa wa ICE wametumwa Minneapolis, katika jimbo la Minnesota, kama sehemu ya msako wa Ikulu dhidi ya uhamiaji haramu.

    Kufuatia tukio hilo, meya wa chama cha Democratic wa jiji hilo, Jacob Frey, ametumia kauli kali kuwataka maafisa wa ICE kuondoka.

    Noem anasema shughuli za ICE huko Minneapolis zitaendelea na FBI inachunguza.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Seneti ya Marekani kupiga kura ya kumdhibiti Trump kuhusu Venezuela

    Seneti ya Marekani inatarajiwa kupigia kura azimio siku ya Alhamisi ambalo litamzuia Rais Donald Trump kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Venezuela bila idhini ya bunge.

    Ni siku chache baada ya vikosi vya Marekani kumkamata Rais wa Venezuela Nicolas Maduro katika shambulio la kijeshi lililotokea Caracas.

    Kura ya mwisho kama hiyo ilikosa kupita kwa kura chache tu 49-51, huku maseneta wawili kutoka chama cha Trump wakijiunga na Wademokrat kuunga mkono azimio la mwezi Novemba.

    Maafisa wa utawala wa Trump wakati wa kura hiyo waliwaambia wabunge kwamba Marekani haina mpango wa kufanya mabadiliko ya utawala au mashambulizi ya kijeshi katika eneo la Venezuela.

    Baada ya kukamatwa kwa Maduro, baadhi ya wabunge wameishutumu serikali kwa kulipotosha Bunge, wakiwemo Wademokrat na baadhi ya Warepublican nyuma ya pazia.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Kanisa lenye ushawishi China laripoti kuzidi kukamatwa na kukandamizwa Wakristo

    Kanisa moja la Kiprotestanti lenye ushawishi mkubwa nchini China linasema viongozi mashuhuri wamekamatwa katika kile kinachoonekana kuwa msako unaoongezeka dhidi ya harakati za kanisa hilo.

    Watu tisa walikamatwa Jumanne baada ya polisi kuvamia nyumba zao na ofisi ya kanisa huko Chengdu, limesema Kanisa la Early Rain Covenant. Watano kati yao wameachiliwa huru kufikia Jumatano.

    Zaidi ya maili 1,000 kutoka Wenzhou, mamlaka zimeanza kubomoa jengo la Kanisa la Yayang, kwa mujibu wa ChinaAid, shirika linalofuatilia ukandamizaji wa kidini.

    Wimbi hili la hivi karibuni la kukamatwa, baada ya wimbi la mwaka jana, linaonyesha azimio la Chama cha Kikomunisti la kuangamiza makanisa ambayo hayaendani na itikadi yake, yanasema makundi ya Kikristo.

    BBC imewasiliana na ubalozi wa China nchini Uingereza kwa ajili ya kutoa maoni. Serikali ya China pia bado haijatoa taarifa yoyote kuhusu kukamatwa kwa watu hao, au ubomoaji huko Wenzhou.

    Hadi kufikia 2028 Serikali ya China ilisema kuna Wakristo milioni 44 huku Chama cha Kikomunisti kikiwashinikiza Wakristo kujiunga na makanisa yaliyoidhinishwa na serikali na wachungaji walioidhinishwa na serikali.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Watu 39 wamefariki baada ya boti ya wahamiaji kuzama Gambia

    Idadi ya vifo baada ya boti iliyokuwa imewabeba wahamiaji wanaoelekea Ulaya kuzama pwani ya Gambia katika mkesha wa Mwaka Mpya imeongezeka hadi 39, maafisa wawili wa serikali wameiambia Reuters.

    Manusura wamesema chombo hicho "kilijaa kupita kiasi na chakavu."

    Wiki iliyopita, wizara ya ulinzi ya Gambia ilisema idadi ya vifo ilikuwa saba na kusema zaidi ya watu 200 walikuwa ndani ya boti hiyo.

    Jumla ya watu 112 wameokolewa kufikia Jumatano, amesema Sima Lowe, afisa wa uhusiano wa umma wa Idara ya Uhamiaji ya Gambia.

    Afisa mkuu wa wizara ya ulinzi ambaye aliomba asitajwe jina lake kwa kuwa hana ruhusa ya kuzungumza na waandishi wa habari, ametoa idadi sawa na hiyo.

    Manusura waliohojiwa na Reuters baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini nchini Gambia wiki hii wamesema boti hiyo ilikuwa ikielekea Ulaya.

    Kati ya waliokufa 39, 24 walipatikana katika eneo la Gambia, huku 15 wakipatikana katika eneo la Senegal, amesema afisa wa ulinzi.

    Abiria waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni pamoja na raia wa Gambia, Senegal, Guinea, Mali, Ivory Coast, Burkina Faso na Sierra Leone, amesema afisa huyo.

    Serikali ya Gambia imesema imewakamata zaidi ya wahamiaji 2,700 mwaka 2025.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Marekani yasitisha misaada kwa Somalia ikidai chakula cha msaada kilizuiliwa kinyume cha sheria

    Marekani imesitisha misaada yote kwa serikali ya Somalia, ikidai maafisa waliharibu ghala la Shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) na kushikilia "msaada wa chakula unaofadhiliwa na wafadhili."

    "Utawala wa Trump una sera ya kutovumilia kabisa uharibifu, wizi, na kuvuruga misaada ya kuokoa maisha," imesmea taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

    Ujumbe huo, uliochapishwa kwenye akaunti ya waziri msaidizi wa misaada ya kigeni, unasema tuna ripoti kuhusu maafisa kukamata kinyume cha sheria tani 76 za chakula kilichokusudiwa "Wasomali walio katika mazingira magumu."

    Kurejesha tena msaada wowote kutategemea serikali ya Somalia "kuwajibika kwa vitendo vyake visivyokubalika na kuchukua hatua zinazofaa za kurekebisha," imesema taarifa.

    Ingawa Marekani imejiondoa katika mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa chini ya Rais Donald Trump, inasalia kuwa mchangiaji mkubwa zaidi kwa WFP, imetoa dola bilioni 2 mwaka 2025 - karibu theluthi moja ya jumla ya ufadhili wake.

    Serikali ya Somalia, imekuwa katika vita dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu wenye uhusiano na al-Qaeda, vita hivyo vimesababisha uharibifu mkubwa na miaka mingi ya ukame.

    Nchi hiyo bado haijatoa maoni yoyote.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Bobi Wine asema atapitia upya mikataba ya mafuta ikiwa atachaguliwa kuwa rais

    Bobi Wine, mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa rais wa Uganda wiki ijayo, amesema atapitia upya makubaliano ya nchi hiyo na makampuni ya mafuta ya kimataifa ikiwa atashinda na kurekebisha yale ambayo hayana maslahi kwa Waganda.

    Uganda inatarajia kuanza uzalishaji wa mafuta ghafi kwa ajili ya biashara baadaye mwaka huu kwa kushirikiana na makampuni ya TotalEnergies ya Ufaransa (TTEF.PA), CNOOC ya China na Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Uganda, kwa msingi wa makubaliano ya kugawana uzalishaji na serikali.

    "Tutasoma makubaliano yote," Wine, nyota wa zamani wa muziki ambaye anapambana na Museveni kwa uchaguzi wa pili mfululizo baada ya kushinda 35% ya kura mwaka 2021, aliambia Reuters wakati wa mahojiano wiki iliyopita katika mji mkuu wa Kampala.

    "Na sehemu yoyote katika mikataba hiyo ambayo haiwapendelei Waganda hakika itarekebishwa."

    Waziri wa habari wa Uganda, TotalEnergies na CNOOC hawakujibu maombi ya kutoa maoni.

    Akiba ya mafuta ya Uganda inakadiriwa kuwa mapipa bilioni 6.65. Iligundua mafuta hayo miaka 20 iliyopita lakini uzalishaji umecheleweshwa mara kwa mara kutokana na kutokubaliana kati ya makampuni ya kimataifa na serikali na upinzani kutoka kwa wanaharakati wa mazingira.

    Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi anapambana na rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, ambaye ameitawala Uganda kwa miaka 40.

    Wapinzani wake na wanaharakati wa haki za binadamu mara kwa mara wanaishutumu serikali yake kwa kuwakandamiza wakosoaji wake, madai ambayo yamepuuzwa na serikali.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Waziri wa zamani wa Ghana azuiliwa na maafisa wa uhamiaji Marekani

    Waziri wa zamani wa Fedha wa Ghana, Ken Ofori-Atta, amekamatwa na Maafisa wa Uhamiaji na Forodha wa Marekani (ICE) kutokana na masuala yanayohusiana na hadhi yake ya uhamiaji.

    Mawakili wake wa Ghana, katika taarifa yao Jumatano wanasema anatoa ushirikiano kwa mamlaka ya Marekani, na timu yake ya kisheria ya Marekani inafanya kazi ili kuachiliwa kwake.

    "Bw. Ofori-Atta anasubiri marekebisho ya hadhi yake ya ukaazi, ombi hilo la marekebisho linampa mtu hadhi ya kukaa Marekani baada ya kipindi cha uhalali wa viza yake," imesema taarifa hiyo.

    Nchini Ghana, Ken Ofori-Atta anakabiliwa na mashtaka 78 ya ufisadi na mashtaka mengine, ikiwa ni pamoja na kula njama ya kufanya udanganyifu katika ununuzi na kusababisha hasara ya kifedha kwa serikali.

    Waziri huyo wa zamani wa Fedha anadaiwa kusimamia mchakato wa ununuzi wa Strategic Mobilisation Ghana Limited (SML), kampuni binafsi na kufanya malipo ya zaidi ya dola milioni 1 (GHC 18,556,390.28) kwa ajili ya huduma za ukaguzi wa hesabu za serikali lakini hakuna ushahidi wa kampuni hiyo kufanya kazi hiyo.

    Mwezi Februari 2025, mwendesha mashtaka wa Ghana alitangaza kuwa Ofori-Atta amekimbia nchi.

    "Ofori-Atta aliondoka Ghana ili kukwepa uchunguzi, na hatua zote muhimu zitachukuliwa ili kumrudisha," alisema Mwendesha Mashtaka Maalum wa kesi hiyo.

    Waendesha mashtaka walisema Ken Ofori-Atta, mwenye umri wa miaka 66 aliondoka Ghana mwezi Januari 2025.

    Ghana imepeleka ombi rasmi kwa Marekani kutaka arejeshwe, lakini mawakili wake wanapinga hilo.

    Ghana ina uhusiano mzuri na Marekani, na nchi hizo mbili hivi karibuni zilishirikiana kuwarudisha raia wa Afrika Magharibi nyumbani. Ghana haiko kwenye orodha ya vikwazo vya Marekani juu ya viza.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Alichokisema Arteta huku Arsenal wakitarajiwa kuwinda ushindi dhidi ya Liverpool

    Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amezungumza na waandishi wa habari kuelekea mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Liverpool itakayopigwa usiku wa Alhamisi kwenye Uwanja wa Emirates (kuanza saa 2:00 usiku kwa saa za GMT).

    Haya ni mambo muhimu kutoka kwenye mkutano wake na waandishi wa habari:

    Mabeki Riccardo Calafiori na Cristhian Mosquera bado hawatakuwa lakini Arteta amesema wako katika hatua za mwisho za kurejea uwanjani.

    Kai Havertz alirejea mazoezini Jumatano, na Arteta ana matumaini kuwa atakuwa tayari kwa mechi ya Alhamisi.

    Arteta amesema mashabiki wa Emirates “huinua motisha ya timu nzima”, na kuwafanya wachezaji kucheza kwa “ushupavu, dhamira kubwa na kujiamini” ikiwa ni mambo muhimu katika mbio za ubingwa.

    Akizungumza kuhusu Leandro Trossard, ambaye amekuwa akipewa sifa kwa kiwango chake msimu huu, Arteta alisema: “Ana uwezo mkubwa, lakini uthabiti anaouonyesha msimu huu ni wa kipekee. Anaelewana vizuri na timu katika kila eneo la mchezo na huleta kitu tofauti.” Arteta alisema ni rahisi kudumisha umakini kambini kwa sababu “kila mmoja anatamani mafanikio kwa kiwango kilekile, na hiyo ndiyo inayowasukuma wote”.

    Akizungumzia ushirikiano wa Declan Rice, Martin Ødegaard na Martin Zubamendi, Arteta aliutaja kuwa “wa kipekee”, akisema ni wazi kuwa wanaelewana vyema na wanakamilishana kikamilifu.

    Kuhusu Liverpool, Arteta alisema ni timu inayoweza kucheza kwa mitindo tofauti, hivyo Arsenal lazima iwe makini katika maandalizi.

    Alihitimisha kwa kusema: “Tunalenga kushinda kila mechi. Mechi muhimu zaidi ni ya leo. Tunajua tunachotakiwa kufanya ili kuwafunga Liverpool sasa ni suala la kuthibitisha hilo uwanjani.”

    Arsenal wakishinda Liverpool wataweka pengo la alama nane kileleni mwa jedwali.

    Soma pia:

  11. Australia kufanya uchunguzi wa kina kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi baada ya shambulio la Bondi

    Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese ametangaza tume, yenye nguvu zaidi ya uchunguzi huru nchini humo, kuchunguza kiini cha ufyatuaji risasi wa mwezi uliopita kwenye ufukwe wa Bondi.

    Shambulio hilo lililolenga tamasha la Wayahudi lilisababisha vifo vya watu 15, na hivyo kuwa moja ya matukio mabaya zaidi katika historia ya nchi hiyo.

    Albanese hapo awali alipendekeza kuwa mageuzi kuhusu umiliki wa bunduki na matamshi ya chuki, hatua za kukabiliana na chuki dhidi ya Wayahudi na kutathmini upya mashirika ya kijasusi na kutekeleza sheria yalitoa jibu la haraka zaidi kuhusu yaliyochochea shambulio hilo.

    Lakini kufuatia wiki za shinikizo la umma, alisema Alhamisi kwamba tume huru ya uchunguzi ilikuwa njia bora zaidi baada ya kuchukua "wakati wa kutafakari" na kukutana na jamii ya Wayahudi.

    "Nimesema mara kwa mara kwamba kipaumbele cha serikali yetu ni kukuza umoja na mshikamano wa kijamii, na hili ndilo ambalo Australia inahitaji kuponya, kujifunza, kuja pamoja katika roho ya umoja wa kitaifa," aliwaambia waandishi wa habari huko Canberra.

    "Ni wazi kwangu kwamba tume ya uchunguzi ni muhimu kufanikisha hili", aliongezea.

    Tangu shambulio la Disemba 14, familia za waathiriwa, pamoja na kikundi cha watu mashuhuri wa umma, wakiwemo wanasheria, wafanyabiashara na wanariadha walikuwa wameongoza kampeni ya karibu kila siku kumtaka abadilishe mwelekeo na kuzindua tume ya uchunguzi.

    Tume ya uchunguzi ina mamlaka makubwa ya kuchunguza, uwezo wa kuwaita mashahidi na kulazimisha mashirika kutoa hati. Inaweza pia kutoa ulinzi wa kisheria kwa watoa taarifa zitakazosaidia kujua kiini cha shambulizi hilo.

    Katika siku chache baada ya shambulio hilo, viongozi wa serikali na shirikisho walikubaliana kuimarisha udhibiti wa bunduki, ikiwa ni pamoja na mipaka juu ya idadi ya silaha zinazomilikiwa na mtu yeyote na aina za bunduki zinazoweza kumilikwa, pamoja na mpango wa kununua tena.

    Albanese pia aliahidi mageuzi ya matamshi ya chuki ikiwa ni pamoja na adhabu kwa wahubiri na viongozi wanaoendeleza vurugu na kosa jipya la shirikisho la "matamshi ya chuki yaliyokithiri".

    Soma Pia:

  12. Trump aiondoa Marekani katika mkataba muhimu wa Tabianchi na mashirika kadhaa ya kimataifa

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kujiondoa kwa Marekani kutoka katika mashirika kadhaa ya kimataifa, yakiwemo mengi yanayohusika moja kwa moja na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

    Hatua hiyo imezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jumuiya ya kimataifa, hasa kutokana na athari zake kwa juhudi za pamoja za kukabiliana na ongezeko la joto duniani.

    Kati ya mashirika 66 yaliyoathiriwa, takriban nusu ni ya Umoja wa Mataifa, yakiwemo Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), ambao ndio mhimili wa mikakati yote ya kimataifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

    Ikulu ya Marekani (White House) ilieleza kuwa uamuzi huo ulitokana na tathmini iliyoonyesha kuwa mashirika hayo “hayatumikii tena maslahi ya Marekani” na badala yake yanaendeleza ajenda “zisizo na ufanisi au zenye mwelekeo unaoathiri maslahi ya taifa”.

    Iliongeza kuwa kuendelea kushiriki katika mashirika hayo ni matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za walipa kodi wa Marekani.

    Rais Trump, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mkosoaji wa mashirika ya kimataifa, tayari amesitisha au kupunguza ufadhili wa taasisi kadhaa za kimataifa.

    Aidha, amewahi kupinga makubaliano ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na shughuli za binadamu, akiyataja kama “hila”.

    Hati rasmi ya kujiondoa ilisainiwa Jumatano kufuatia mapitio ya sera ambayo Ikulu ilisema yalibaini matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

    Katika taarifa yake, White House ilisema kuwa hatua hiyo “itakomesha ufadhili na ushiriki wa walipa kodi wa Marekani katika taasisi zinazotanguliza ajenda za utandawazi kuliko vipaumbele vya kitaifa vya Marekani”.

    Taarifa hiyo iliongeza kuwa baadhi ya mashirika hayo yanahamasisha “sera kali za tabianchi, mifumo ya utawala wa kimataifa na programu za kiitikadi zinazokinzana na uhuru wa Marekani na uthabiti wake wa kiuchumi”.

    Miongoni mwa taasisi zilizoathiriwa ni Jopo la Kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), chombo cha kitaalamu kinachotathmini na kutoa miongozo kuhusu sayansi ya tabianchi duniani.

    Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yanayojihusisha na amani na demokrasia, upangaji uzazi, afya ya mama na mtoto, pamoja na kupambana na ukatili wa kijinsia katika maeneo ya migogoro pia yamejumuishwa katika orodha hiyo.

    Kisheria, ingawa Katiba ya Marekani inaruhusu rais kujiunga na mikataba ya kimataifa kwa idhini ya thuluthi mbili ya Seneti, haielezi bayana utaratibu wa kujiondoa.

    Hali hiyo inafungua uwezekano wa hatua ya Trump kupingwa mahakamani.

    Hatua hiyo imekosolewa vikali na wadau wa sayansi na mashirika ya kiraia.

    Mwakilishi wa shirika la Union of Concerned Scientists alielezea uamuzi huo kama “hatua ya kushuka kwa kiwango cha chini kabisa”.

    Mkurugenzi mwandamizi wa sera wa shirika hilo, Rachel Cleetus, aliambia shirika la habari la AFP kuwa hatua hiyo inaashiria msimamo wa utawala aliouelezea kama “unaopinga sayansi na wenye mwelekeo wa kiimla”, unaohatarisha ustawi wa binadamu na kudhoofisha ushirikiano wa kimataifa.

    Mwaka jana, Trump aliiondoa tena Marekani kutoka Mkataba wa Tabianchi wa Paris, juhudi muhimu zaidi duniani za kupunguza ongezeko la joto na pia alikataa kutuma ujumbe wa Marekani katika mkutano wa COP30 wa tabianchi uliofanyika Brazil, hatua iliyozidisha hofu kuhusu mustakabali wa uongozi wa Marekani katika masuala ya mazingira duniani.

    Soma pia:

  13. Uchaguzi Uganda 2026: EC yawasilisha daftari rasmi la wapiga kura siku 7 kabla ya uchaguzi

    Tume ya uchaguzi ya Uganda EC imeanza mchakato wa kuwakabidhi wagombea wa Urais nakala rasmi za sajili ya kitaifa ya wapiga kura siku moja baada ya malalamiko kutoka kwa wagombea.

    Maafisa wa chama tawala Nationa Resistance Movement (NRM) walikuwa wakwanza kupokea nakala hizo asubuhi, huku wenzao wa chama cha National Unity Platform (NUP) wakizipokea Alasiri.

    Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi kifungu cha 19 sehemu ya 176, inawashurutisha Tume ya Uchaguzi ya Uganda kutoa sajili ya wapiga kura kwa vyama vya kisiasa na wagombea wao watakaowania Urais angalau wiki mbili kabla ya uchaguzi.

    Lakini mchakato huo umefanyika siku saba kabla ya uchaguzi utakaofanyika Alhamisi ya Januari 15, 2026.

    “Tume imeanza kukabidhiana nakala za sajili za wapiga kuta kwa wagombwa urais kama sheria inavyoaijisha.Mchakato huo unajumuisha kutathmini sajili zitakazotumika kwa vituo vya kupigia kura 50,000 na zimepangwa kwa mafungu ya kieneo na madiwani” anasema afisa wa EC.

    Bwana Mucunguzi amesema kuwa kila mgombea au mwakilishi wake atahitaji takriban saa tatu kutathmini na kuhakiki sajili hiyo.

    “Kila mwakilishi wa mgombea atahitajika kutathmini nakala za sajili za wapiga kura watakazokabidhiwa.Sajili hiyo ina kurasa milioni na kila kurasa ina maelezo ya wapiga kura kama vile picha zao.”

    Hata hivyo, Alex Rovans, msaidizi wa katibu mkuu katika chama cha NUP amekosoa Tume ya uchaguzi kwa kuchelewesha kuwakabidhi sajili, akisema hili linapunguza muda wa kuzipitia na kutoa maoni kuhusu dosari zinazoweza kupatikana.

    “Tumeibua malalamiko mengi na Tume ya Uchaguzi haijatamka jibu kuhusu dai la wapigaji kura kusajiliwa zaidi ya mara moja katika sajili. Katibu mkuu ametambua zaidi ya wapiga kura 1500 wamesajiliwa zaidi ya mara moja katika eneo bunge la Kampala ya kati pekee.Hata hivyo, tutaendelea kuihakiki sajili haraka iwezekanavyo na kuibua dosari zaidi tutakazozitambua,” alisema.

    Mnamo Novemba 26,2025, Tume ya Uchaguzi ya Uganda ilisambaza sajili ya wapiga kura ikionyesha kuwa idadi ya wapiga kura waliosajiliwa waliongezeka kutoka milioni 18.1 katika chaguzi za 2021 hadi milioni 21.6 ambao wanatarajiwa kupiga kura wiki ijayo katika vituo vya kupiga kura 50,739 kote nchini Uganda.

    Kinyang’anyiro cha urais nchini Uganda kimevutia wagombea 8, na wanajumuisha Robert Kyagulajyi wa chama cha NUP, rais aliye madarakani Yoweri Museveni wa NRM na Nathan Nandala Mafabi wa chama cha Forum For Democratic Change(FDC).

    Wengine ambao pia wanawania kuongoza Uganda ni Meja Jenerali Gregory Mugisha Muntu wa chama cha National Transformation (ANT), Robert Kasibante wa chama cha National Peasant’s Party(NPP), ELton Joseph Mabirizi wa chama cha Conservative Party (CP), Frank Bulira wa chama cha Revolutionary People’s Party (RPP) na Mubarak Munyagwa wa chama cha Common Man’s Party (CMP).

    Soma pia:

  14. Rubio kukutana na viongozi wa Denmark, ikionekana Trump hajaondoa wazo lake la kudhibiti Greenland

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alitangaza Jumatano kwamba atakutana na viongozi wa Denmark wiki ijayo, huku akibainisha kwamba hatarudi nyuma katika lengo la Rais Donald Trump la kuchukua udhibiti wa Greenland.

    Wakati huo huo, washirika waliokuwa na wasiwasi, ikiwa ni pamoja na Ufaransa na Ujerumani, wameshajitahidi kuandaa majibu.

    Operesheni ya kijeshi ya Marekani iliyofanyika Jumapili iliyomkamata kiongozi wa Venezuela imezua tena hofu kuhusu nia za Marekani kwa Greenland, huku maafisa wa Marekani wakishindwa kupunguza wasiwasi huo.

    Rubio alibainisha kwamba Trump bado ana chaguo la kufanikisha lengo lake kwa njia za kijeshi, lakini alisisitiza kuwa “kama mwana diplomasia, ambayo ndiyo nafasi yangu sasa, tunapendelea kutatua masuala kwa njia nyingine hii ni pamoja na kesi ya Venezuela.”

    Kutuma vikosi vya kijeshi kwa kisiwa tajiri cha madini cha Aktiki kutoka Denmark, aliyechukuliwa kama mshirika wa muda mrefu wa Marekani, ungeleta mshtuko mkubwa ndani ya NATO na kuongeza mgawanyiko kati ya Trump na viongozi wa Ulaya.

    Kauli hiyo ya Trump pia imekabiliwa na upinzani wa wabunge wa Marekani, ambapo seneta wa Kidemokratic na Kirepublican walibainisha Jumatano kwamba Senati hatimaye itapiga kura juu ya muswada unaolenga kupunguza uwezo wa Rais kujaribu kuchukua Greenland.

    Pia uanweza kusoma:

  15. Mashambulizi ya Urusi yanasababisha ukosefu wa umeme katika mikoa miwili - Ukraine

    Mashambulizi ya Urusi yamesababisha mikoa ya kusini-mashariki mwa Ukraine, Dnipropetrovsk na Zaporizhzhia, kukosa umeme kwa kiasi kikubwa, kwa mujibu wa Wizara ya Nishati ya nchi hiyo Jumatano usiku.

    Miundombinu muhimu “inafanya kazi kwa kutumia jenereta za dharura,” ilisema taarifa iliyotolewa kwenye Telegram, huku maafisa wakisema kuwa usambazaji wa maji na mtandao wa intaneti pia umeathirika.

    Hivi karibuni, Urusi imezidisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine, kwa lengo la kuzidisha ukosefu wa umeme wakati wa baridi kali.

    “Mfumo wa nishati wa Ukraine unakabiliwa na mashambulizi ya adui kila siku, na wafanyakazi wa nishati wanafanya kazi katika hali ngumu sana kuhakikisha watu wanapata mwanga na joto,” aliandika Waziri Mkuu wa Ukraine, Yulia Svyrydenko, kwenye Telegram.

    “Hali mbaya ya hewa inaongeza mzigo kwa miundombinu muhimu,” aliongeza. Usumbufu wa umeme na joto umekuja wakati joto linapungua. “Kazi za dharura za kurekebisha umeme katika mikoa iliyoathirika na shambulio zitaanza mara moja pale hali za usalama zitakaporuhusu,” kampuni ya umeme ya taifa, Ukrenergo, ilisema kwenye Telegram.

    Iliongeza: “Kazi kuu ya wafanyakazi wa nishati ni kurekebisha miundombinu muhimu.” Meya wa jiji la Dnipro, Borys Filatov, alisema kwenye Telegram kuwa hospitali zote za jiji zimeunganishwa kikamilifu na jenereta.

    “Kuna usambazaji wa maji unaohitajika, na mchakato wa matibabu haujasitishwa.

    Mfumo wa kutolea maji majumbani pia unasaidiwa na vyanzo mbadala vya umeme,” Filatov alisema.

    Aliongeza kuwa likizo za shule zitaendelea hadi Januari 9 kutokana na ukosefu wa umeme.

    Kiongozi wa mamlaka ya mkoa wa Zaporizhzhia, Ivan Fedorov, alisema kuwa kila jitihada zinafanywa kurekebisha umeme.

    “Kwa sasa, wafanyakazi wa huduma za maji wamerudisha usambazaji wa maji majumbani kwetu, licha ya kuwa mkoa mzima uko bila umeme kabisa,” Fedorov alisema katika ujumbe wa video uliochapishwa kwenye Telegram.

    Baada ya mazungumzo Paris Jumatatu, Uingereza na Ufaransa zilisaini tamko la nia la kupeleka majeshi nchini Ukraine iwapo makubaliano ya amani yatafikiwa na Urusi.

    Moscow imetahadharisha mara kadhaa kuwa majeshi yoyote ya kigeni nchini Ukraine yatakuwa “lengo halali.”

    Soma pia:

  16. Afisa wa uhamiaji wa Marekani amuua kwa kumpiga risasi mwanamke huko Minneapolis

    Afisa mmoja wa kitengo cha uhamiaji wa Marekani alimpiga risasi na kumuua mwanamke mwenye umri wa miaka 37 siku ya Jumatano katika mji wa Minneapolis, lakini maelezo kuhusu kilichosababisha tukio hilo yameleta tofauti kubwa kati ya maafisa wa serikali ya shirikisho na viongozi wa mitaa.

    Maafisa wa utawala wa Trump wanadai kuwa mwanamke huyo, aliyetambuliwa kama Renee Nicole Good, alikuwa "mzushi" akijaribu kuwavamia maajenti wa Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha (ICE) wakati ajenti mmoja alipofyatua "risasi za kujihami" kwenye gari lake.

    Lakini viongozi wa miji na majimbo, na Wanademokrasia kitaifa, wanatilia shaka maelezo hayo.

    Meya wa Minneapolis Jacob Frey anadai kwamba "huyu alikuwa ajenti akitumia mamlaka bila kujali jambo ambalo lilisababisha mtu kufa", akiwaambia maajenti wa ICE: "Toka nje ya jiji letu."

    Video nyingi zilizopakiwa kwenye mitandao ya kijamii na mashahidi zinaonyesha tukio la risasi, lililotokea karibu saa 10:25 asubuhi kwa muda wa eneo hilo.

    Kutoka pembe mbalimbali, gari aina ya SUV ya rangi ya maruni inaonekana ikizuia barabara ya makazi.

    Umati wa watu, ambao unaonekana wakipinga, umejitokeza kando ya barabara. Magari kadhaa ya polisi pia yanaonekana karibu. Maafisa wa uhamiaji walifika kwenye gari lililokuwa limeegeshwa katikati ya barabara, wakiwa wanatoka kwenye barabara na kumuamuru mwanamke aliyekuwa kwenye kiti cha dereva aondoke kwenye gari hilo.

    Afisa mmoja alishika kiti cha dereva, huku mwingine akiwa mbele ya gari. Afisa huyo alipiga risasi wakati SUV hiyo ilipojaribu kuondoka. Zilisikika risasi tatu, na gari hilo linaonekana kupoteza udhibiti na kugongana na gari jeupe lililokuwa limeegeshwa barabarani.

    Tukio hili limetokea huku utawala wa Trump ukifanya msako mkubwa wa wahamiaji Minneapolis.

    Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Kristi Noem, alisema kitendo cha mwanamke huyo kinatajwa kama ''ugaidi wa ndani.” Aliongeza kuwa operesheni za ICE katika jiji hilo zinaendelea.

    Rais Trump katika chapisho lake kwenye Truth Social alisema afisa wa ICE alikumbwa na gari “kwa ghadhabu,” na kuongeza: “Ni vigumu kuamini kuwa yupo hai, lakini sasa anapona hospitalini.”

    Soma pia:

  17. 'Watu 100 wafariki dunia katika shambulio la Marekani nchini Venezuela' - waziri wa Usalama

    Waziri wa usalama wa Venezuela, Diosdado Cabello, alisema usiku wa Jumatano kwamba watu 100 walifariki katika shambulio la Marekani lililoondoa Rais Nicolás Maduro madarakani siku ya Jumamosi.

    Hapo awali, mamlaka ya Venezuela hayakuwa yametoa idadi rasmi ya waliouawa, ingawa jeshi lilichapisha orodha ya majina 23 ya wanajeshi wake waliopoteza maisha.

    Maafisa wa Venezuela wamesema kuwa sehemu kubwa ya kikosi cha ulinzi wa Rais Maduro kiliuawa “kwa damu baridi,” huku Cuba ikithibitisha kuwa wanajeshi wake pamoja na maofisa wa ujasusi waliokuwa nchini Venezuela pia walifariki.

    Cabello alisema kuwa mke wa Maduro, Cilia Flores, ambaye alikamatwa pamoja naye, alipata jeraha la kichwa wakati wa shambulio hilo, huku Maduro mwenyewe akipata jeraha mguuni. haya ni kwa mujibu wa Reuters.

    Venezuela, ambayo Cabello aliisifu kama “jasiri” katika kipindi chake cha kila wiki kwenye runinga ya taifa, ilitangaza Jumanne wiki ya maombolezo kwa heshima ya wanajeshi waliouawa katika shambulio hilo.

    Soma pia:

  18. Uchaguzi Uganda 2026: 'Uganda iko tayari kumchagua Rais wa kiraia' - NRM

    Msemaji wa chama tawala cha Uganda, National Resistance Movement (NRM) amesema kuwa wapiga kura wa nchi hiyo wako tayari kumuunga mkono mgombea wa urais kutoka katika mazingira yoyote, mradi aonyeshe sifa zinazokubalika za uongozi.

    Katika mahojiano ya kipekee na BBC, Emmanuel Lumala Dombo alisema kuwa historia ya mgombea, iwe ya kiraia au kijeshi, si kigezo pekee kinachoamua uamuzi wa wapiga kura.

    Msemaji huyo wa NRM amesema kuwa kama wapiga kura wa Uganda wangekuwa wanazingatia wagombea wenye historia ya kijeshi pekee, basi wagombea wa aina hiyo wangekuwa wakipata uungwaji mkono mkubwa kila mara kuliko wengine.

    Alitolea mfano mwanasiasa wa upinzani, Dkt. Kizza Besigye, ambaye aliwahi kuwania urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni katika chaguzi zilizopita.

    “Wakati Dkt. Kizza Besigye alipojitokeza kuwania urais dhidi ya Rais Museveni, baadhi ya watu walidhani angekuwa mgombea bora kutokana na historia yake ya kijeshi, lakini bado alishiriki uchaguzi na hakushinda,” alisema Dombo.

    Kwa sasa, mmoja wa wagombea wanaoonekana kutoa changamoto kubwa katika uchaguzi ni mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa, Robert Kyagulanyi, anayefahamika zaidi kwa jina lake la kisanii, Bobi Wine.

    Akizungumzia uvumi unaodai kuwa Rais Museveni anamuandaa mwanawe kama mrithi wake, Dombo alisema kuwa chama hicho kina taratibu zake za ndani kuhusu uongozi na urithishaji.

    Aliongeza kuwa iwapo Jenerali Muhoozi Kainerugaba ataonyesha nia ya kuwania wadhifa wa kisiasa kupitia NRM, atalazimika kufuata taratibu na mchakato uliowekwa ndani ya chama hicho.

    “Ikiwa Jenerali Muhoozi ataamua kutumia nafasi au uzoefu wake wa kijeshi, bado atalazimika kuthibitisha sifa nyingine zinazohitajika ili aonekane kama kiongozi anayestahili kuchaguliwa,” alisema.

    Wananchi wa Uganda wanatarajiwa kupiga kura tarehe 15 Januari kuwachagua rais na wabunge wa bunge la taifa.

    Soma pia:

  19. Hujambo natumai umzima

    Karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ya tarehe 08 Januari 2026.