Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump anaweza kuwania muhula wa tatu wa urais Marekani?
- Author, Graeme Baker
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Donald Trump amesema kuwa hatanii kuhusu kutaka kuhudumu kwa muhula wa tatu kama rais wa Marekani.
Katiba ya Marekani inasema kwamba "hakuna mtu... atakayechaguliwa zaidi ya mara mbili", lakini baadhi ya wafuasi wa Trump wamependekeza kuwa huenda kukawa na namna ya kufanya kwenye hilo.
Kwa nini Trump anazungumzia muhula wa tatu?
Trump aliulizwa katika mahojiano na NBC kuhusu uwezekano wa kuwania muhula wa tatu na akasema, "kuna mbinu ambazo unaweza kuzitumia."
"Sifanyi utani... watu wengi wanataka nifanye hivyo," aliongeza. "Lakini, kimsingi huwaambia kwamba bado tuna safari ndefu, unajua, ni mapema sana katika utawala huu."
Trump, ambaye atakuwa na umri wa miaka 82 ifikapo mwisho wa muhula wake wa pili, aliulizwa ikiwa angependa kuendelea kuhudumu katika "kazi ngumu zaidi nchini" (kazi ya urais wa Marekani).
"Naam, napenda kufanya kazi," alijibu.
Haya si maoni yake ya kwanza kuhusu suala hili. Mnamo Januari, aliwaambia wafuasi wake kuwa itakuwa "heshima kubwa zaidi ya maisha yangu kuhudumu si mara moja tu, bali mara mbili au tatu au hata nne". Hata hivyo, baadaye alisema kuwa alikuwa anatania kwa ajili ya "vyombo vya habari feki".
Katiba ya Marekani inasemaje?
Kimsingi, katiba ya Marekani inaonekana kuzuia mtu yeyote kuhudumu kwa mihula mitatu. Marekebisho ya 22 ya Katiba yanabainisha:
"Hakuna mtu atakayechaguliwa kushika wadhifa wa rais zaidi ya mara mbili, na hakuna mtu ambaye ameshikilia wadhifa wa rais, au kukaimu majukumu ya rais, kwa zaidi ya miaka miwili ya muhula ambao mtu mwingine alichaguliwa kuwa rais, atachaguliwa kuwa rais (lakini) zaidi ya mara moja."
Kubadilisha katiba kunahitaji idhini ya theluthi mbili kutoka kwa Bunge la Seneti na Baraza la Wawakilishi, pamoja na kuidhinishwa na theluthi tatu ya serikali za majimbo nchini humo.
Chama cha Republican cha Trump kinadhibiti mabunge yote mawili lakini hakina idadi ya kutosha kuweza kufanya mabadiliko ya katiba. Zaidi ya hayo, Chama cha Democratic kinadhibiti mabunge ya majimbo 18 kati ya 50.
Kwa namna gani Trump anaweza kuwa rais kwa muhula wa tatu?
Wafuasi wa Trump wanasema kuna mwanya katika katiba ambao haujawahi kujaribiwa mahakamani.
Wanadai kuwa Marekebisho ya 22 yanakataza mtu tu "kuchaguliwa" kwa zaidi ya mihula miwili ya urais - lakini hayasemi chochote kuhusu "kurithi madaraka".
Kwa mujibu wa nadharia hii, Trump anaweza kuwa mgombea mwenza wa mgombea mwingine - labda makamu wake wa rais, JD Vance - katika uchaguzi wa 2028.
Iwapo watafanikiwa kushinda, mgombea huyo anaweza kula kiapo cha kuingia Ikulu ya White House kisha kujiuzulu mara moja na kumruhusu Trump kuchukua madaraka kwa njia ya kurithi.
Steve Bannon, mtangazaji na mshauri wa zamani wa Trump, alisema anaamini Trump "atagombea na kushinda tena", akiongeza kuwa kuna "njia mbadala" za kufanikisha hilo.
Andy Ogles, Mwakilishi wa Republican kutoka Tennessee katika Baraza la Wawakilishi, aliwasilisha azimio mnamo Januari akitaka marekebisho ya katiba ili kuruhusu rais kuhudumu hadi mihula mitatu mradi tu isiwe ya mfululizo.
Hii ingemaanisha kuwa Trump pekee kati ya marais waliopita wangekuwa na sifa. Barack Obama, Bill Clinton, na George W. Bush wote walihudumu kwa mihula miwili mfululizo, wakati Trump alishinda mwaka 2016, akashindwa mwaka 2020, kisha akashinda tena mwaka 2024.
Hata hivyo, ugumu wa marekebisho ya katiba unafanya pendekezo la Ogles kuwa ndoto isiyowezekana, ingawa limeanzisha mjadala.
Trump supporters say there is a loophole in the c
Kina nani wanapinga Trump kuongoza muhula wa tatu?
Democrats wanapinga vikali.
"Hii ni hatua nyingine ya wazi katika juhudi zake za kuteka serikali na kuvuruga demokrasia yetu," alisema Daniel Goldman, Mwakilishi wa New York ambaye aliwahi kuwa mshauri mkuu wa kesi ya kwanza ya kumfungulia mashitaka Trump.
"Iwapo Warepublican wa Congress wanaamini katika Katiba, wataingia kwenye rekodi ya kupinga matamanio ya Trump ya kuongoza muhula wa tatu."
Ken Martin, mmoja wa vigogo wa chama cha Democrat alisema kwenye X: "Hivi ndivyo madikteta hufanya."
Baadhi ya wanachama wa chama cha Trump pia wanaona kuwa ni wazo mbaya.
Seneta wa Republican Markwayne Mullin wa Oklahoma alisema mwezi Februari kuwa hataunga mkono jaribio lolote la kumrudisha Trump Ikulu.
"Kwanza kabisa, siibadilishi katiba, labda kama Wamarekani waamue wenyewe kufanya hivyo," Mullin aliambia NBC.
Wataalamu wa sheria wanasemaje?
Derek Muller, profesa wa sheria za uchaguzi katika Chuo Kikuu cha Notre Dame, alisema Marekebisho ya 12 ya Katiba yanasema kuwa "hakuna mtu asiye na sifa za kikatiba kuwa rais atakayestahiki kuwa makamu wa rais wa Marekani".
Hii ina maana kuwa kuhudumu kwa mihula miwili kunamzuia mtu yeyote kugombea kama mgombea mwenza, kwa mtazamo wake.
"Sidhani kuna 'mbinu ya ajabu' ya kukwepa mipaka ya mihula ya urais," alisema.
Jeremy Paul, profesa wa sheria ya katiba katika Chuo Kikuu cha Northeastern cha Boston, aliambia CBS News kuwa hakuna "hoja yoyote halali" ya muhula wa tatu.
Je, kuna mtu yeyote aliyewahi kuhudumu zaidi ya mihula miwili?
Franklin Delano Roosevelt ndiye rais pekee wa Marekani aliyehudumu kwa zaidi ya mihula miwili.
Alishinda mara nne na alifariki miezi mitatu baada ya kuanza muhula wake wa nne, Aprili 1945.
Mdororo Mkubwa wa Uchumi na Vita vya Pili vya Dunia vilitawala uongozi wa Roosevelt , na mara nyingi hutajwa kama sababu ya kuongoza kwa muda mrefu kama Rais wa Marekani.
Wakati huo, hakukuwa na sheria ya kikatiba inayopiga marufuku mihula mingi ya urais, ilikuwa ni desturi tu iliyoanzishwa tangu George Washington alipokataa kugombea muhula wa tatu mnamo 1796.
Uongozi wa muda mrefu wa Roosevelt ulisababisha desturi hiyo kuandikwa rasmi katika Marekebisho ya 22 ya Katiba mwaka 1951.