Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege ya Rais ya Air Force One Ijumaa jioni, Trump alisema: “Tutawashtaki kwa chochote kati ya dola bilioni 1 hadi 5, pengine wiki ijayo.”
Muhtasari
Iran yaikamata meli ya mafuta katika mlango bahari wa Hormuz
Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha ujumbe wa kuchunguza ukweli kuhusu mauaji ya Sudan
Iran yaikamata meli ya mafuta katika mlango bahari wa Hormuz
Chanzo cha picha, EPA
Jeshi la Iran (IRGC) limethibitisha
kuikamata meli ya mafuta jana Ijumaa katika mlango bahari wa Hormuz.
Meli ya mafuta ya Talara, iliyokuwa
ikipeperusha bendera ya Visiwa vya Marshall ilikuwa ikisafiri kutoka Falme za
Kiarabu (UAE) kwenda Singapore.
IRGC lilisema iligundulika kuwa meli hiyo
"inakiuka sheria kwa kubeba mizigo isiyoruhusiwa", lakini haikutoa
maelezo zaidi kuhusu ukiukaji huo.
Ripoti zinaonyesha kuwa ilikuwa ikibeba kwa
wingi gesi ya salfa.
Iran mara kwa mara imekuwa ikikamata meli
za mafuta na meli za mizigo zinazosafiri ndani na karibu na Ghuba yake, ambayo
ni njia muhimu ya dunia kwa usafirishaji wa mafuta na gesi asilia
iliyoyeyushwa.
Mara nyingi imetaja ukiukwaji wa safari za
baharini kama vile biashara za magendo au haramu.
Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha ujumbe wa kuchunguza ukweli kuhusu mauaji ya Sudan
Chanzo cha picha, Getty Images
Wajumbe wa baraza la haki za binadamu la
Umoja wa mataifa wamepitisha azimio la ujumbe huru wa kuchunguza ukweli kuhusu
mauaji ya halaiki yaliyoripotiwa huko Al-Fashir, Sudan.
Katika kikao maalum cha baraza huko Geneva
kuhusu hali ya jiji la Darfur ambalo lilidhibitiwa kijeshi mnamo Oktoba,
hatua hiyo ilipitishwa bila kura ikiwa ni ishara ya kuungwa mkono
kimataifa.
Jopo hilo pia litachunguza na kutambua
wahusika wa ukiukwaji unaodaiwa kutekelezwa na vikosi vya Rapid Support Forces
na washirika wao huko Al-Fashir.
Balozi wa ujumbe wa kudumu wa Uingereza
huko Geneva alisema ujumbe wa kutafuta ukweli utaandika na kuhifadhi ushahidi
wa ukiukwaji huo, ambao utaweka msingi wa haki na uwajibikaji wa siku zijazo.
Katika hotuba ya ufunguzi kwa wajumbe, mkuu
wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa alihimiza jumuiya ya kimataifa kuchukua
hatua.
RSF imekanusha kuwalenga raia au kuzuia
misaada, ikisema vitendo hivyo vinatekelezwa na makundi ya wahalifu.
Maaskofu wakatoliki Marekani walaani utekelezaji wa sera ya uhamiaji ya Trump
Chanzo cha picha, Getty Images
Mkutano wa maaskofu wakatoliki wa Marekani
umelaani msako mkali uliotekelezwa na idara ya uhamiaji nchini ambao rais wa Marekani
Donald Trump anatetea kwa kile alichokiita "mageuzi ya msingi ya uhamiaji."
"Tunasumbuliwa na vitisho dhidi ya
utakatifu wa nyumba za ibada na hali maalum ya hospitali na shule,"
maaskofu walisema katika ujumbe maalum, wa kwanza wa aina yake katika kipindi
cha miaka 12.
Idara ya usalama wa ndani, ambayo
inasimamia shughuli za uhamiaji, haikutoa maoni yoyote kuhusu hili.
Ujumbe huo unarejelea ukosoaji kama huo
uliotolewa na Papa Leo, ambaye ametoa wito wa "tafakari ya kina"
kuhusu namna wahamiaji wanavyotendewa nchini Marekani chini ya utawala wa Trump.
Utawala wa Trump umeendeleza ajenda kali ya
uhamiaji tangu alipoingia madarakani mapema mwaka huu.
Trump amefuta sera ambayo inaweka kikomo
cha kukamatwa kwa wahamiaji karibu na maeneo nyeti, ikiwa ni pamoja na
makanisa, hospitali na shule, na kupeleka maafisa wa shirikisho kote Marekani
ili kuimarisha zoezi la ukamataji huko.
Katika ujumbe wao, maaskofu walionyesha
wasiwasi kuhusu kile walichokielezea kama "hali ya hofu na wasiwasi kuhusu
maswali ya utambulisho" na utekelezaji wa sheria za uhamiaji.
Walisema wamesikitishwa na mjadala na
kashfa za wahamiaji, na wanapinga "kuhamishwa kwa watu wengi bila
ubaguzi."
Maandamano Tanzania: Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wote wawajibike, yasema TEC
Chanzo cha picha, TEC
Maelezo ya picha, Rais wa baraza la maaskofu Tanzania Wolfgang Pisa
Baraza la maaskofu wa Kanisa katoliki
nchini Tanzania limetaka mamlaka zinazohusika ziendelee kulaani mauaji
yaliyofanyika na kukiri waliouawa ni watanzania.
Rais wa baraza la maaskofu, Wolfgang Pisa akisoma
tamko hilo kuhusu maandamano yaliyoshuhudiwa hivi karibuni, amesema Kuuawa kwa
watu hovyo, ukosefu wa demokrasia ni miongoni mwa sababu za watu kuandamana.
“Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wote
wawajibike, au kuwajibishwa na mamlaka zao za uteuzi. Hasira ya Wananchi ipo
katika kuona hakuna anayewajibika kwa matendo maovu waliyofanyiwa raia”. Askofu Wolfgang Pisa, Rais wa TEC.
Amesema kwakuwa jambo hilo limesababisha
maafa, baraza linashauri ufanyike uchunguzi utakaowashirikisha wadau wa ndani na
nje ya nchi likipendeza wadau kutoka tume huru isiyofungamana na upande wowote
kama jumuiya na taasisi za kimataifa,dini na asasi za kiraia na wataalamu wa
haki na mambo ya kidemokrasia na serikali iwe tayari kupokea na kufanyia kazi
ripoti watakayotoa.
Hapo jana akizungumza na BBC John Heche makamo
mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA alisema “Tunahitaji tume huru,kutoka
Umoja wa mataifa au Umoja wa Afrika au SADC lakini kwanza tunataka kujua idadi
ya watu waliouawa, majeruhi na baadhi ambao hawajulikani walipo’’.
Akihutubia
bunge, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitangaza kuwa serikali imeunda
tume maalumu kuchunguza matukio yaliyotokea wakati wa maandamano hayo.
"Serikali
imechukua hatua ya kuunda tume itakayochunguza kwa undani kilichotokea ili
tujue kiini cha tatizo. Taarifa ya tume hiyo itatuongoza katika mazungumzo ya
kuleta maridhiano na kudumisha amani," alisema.
Aidha alitangaza msamaha kwa vijana
waliokamatwa kufuatia maandamano ya siku tatu yaliyofanyika kuanzia siku ya
uchaguzi, Oktoba 29, 2025.
Wizara ya Afya nchini Ethiopia
imethibitisha kwamba mlipuko wa hivi karibuni wa homa ya kutokwa na damu ambayo
uliosababisha vifo vya watu sita
katika eneo la kusini mwa nchi, unasababishwa na virusi vya Marburg.
Taarifa hiyo
imefafanua kwamba aina ya virusi waliyoigundua inafanana na ile iliyoripotiwa
hapo awali katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.
Mgonjwa wa kwanza
kuripotiwa katika mlipuko huu alianza kwa kupata homa kali, akafuatiwa na
kutokwa damu na kushindwa kwa viungo mwilini ndani ya muda mfupi.
Baadhi ya wahudumu wa
afya na wanajamii waliokuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na mgonjwa huyo pia
waliambukizwa.
Kufikia sasa, watu
takribani tisa wanakadiriwa kuwa wameambukizwa virusi hivyo.
Huu ni mlipuko wa
kwanza wa Marburg kuwahi kuripotiwa nchini Ethiopia.
Ethiopia imesema kuwa
timu maalumu za kukabiliana na hali ya dharura zimeanzishwa katika maeneo
mbalimbali nchini humo ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
Trump apunguza ushuru wa bidhaa 200 za vyakula huku wasiwasi wa mfumuko wa bei ukiongezeka
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump ameondoa
ushuru wa bidhaa zaidi ya 200 za chakula, ikiwa ni pamoja na vyakula vikuu kama
vile kahawa, nyama ya ng'ombe, ndizi na sharubati ya machungwa, huku wasiwasi
ukiongezeka miongoni mwa watumiaji nchini Marekani kuhusu gharama kubwa ya mahitaji
hayo muhimu.
Msamaha huo mpya ambao ulianza kutekelezwa usiku
wa Alhamisi unaashiria mabadiliko makubwa kwa Trump, ambaye kwa muda mrefu
amesisitiza kwamba ushuru mkubwa wa uagizaji bidhaa alioweka mapema mwaka huu
hautachochea mfumuko wa bei.
Aidha Trump alisisitiza kwamba kwa ujumla,
Marekani "haina mfumuko wowote wa bei."
Katika hatua nyingine wabunge wa democrats wameshinda
katika uchaguzi wa majimbo na mitaa huko Virginia, New Jersey na New York City,
ambapo wasiwasi unaoongezeka miongoni mwa wapiga kura kuhusu gharama za maisha,
ikiwa ni pamoja na bei kubwa za chakula, ikiwa miongoni mwa agenda muhimu.
Trump pia aliwaambia waandishi wa habari akiwa
ndani ya ndege ya rais Air Force One kwamba angeendelea na malipo ya $2,000 kwa
Wamarekani wenye kipato cha chini na cha kati ambayo yangefadhiliwa na mapato
ya ushuru mwaka ujao.
"Ushuru huo unaturuhusu kutoa gawio
ikiwa tunataka kufanya hivyo. Sasa tutafanya gawio na pia tunapunguza
deni," alisema.
Serikali
ya Tanzania inapanga kuanzisha treni za kisasa za mijini katika Dar es Salaam
na Dodoma, hatua inayolenga kupunguza msongamano na kuboresha usafiri wa umma
katika miji hiyo mikubwa.
Rais
Samia Suluhu Hassan amesema mpango huo unazingatia ongezeko la kasi la wakazi,
hasa jijini Dar es Salaam ambalo linatarajiwa kufikia takriban milioni 10
ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa Bunge jijini Dodoma Novemba 14, 2025, Rais Samia alisema
mipango ya usafiri wa mijini inaenda sambamba na ujenzi na ukamilishaji wa njia
kuu za reli katika nchi nzima.
Alisema
Serikali inaendelea kukamilisha vipande vilivyosalia vya reli ya kisasa ya SGR
katika ushoroba wa kati, ikiwemo Makutupora–Tabora, Tabora–Isaka, Isaka–Mwanza
na Tabora–Kigoma. Ujenzi wa reli ya Uvinza–Musongati kuelekea Burundi pia
utaendelezwa.
Serikali
imepanga kuanzisha miradi mipya ya SGR kutoka Tanga hadi Musoma, na reli
nyingine kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay inayogusa maeneo ya Mchuchuma na
Liganga.
Kwa
upande wa reli zilizopo, Serikali inatekeleza maboresho ya TAZARA ambayo
yanatarajiwa kuanza kupitia uwekaji wa jiwe la msingi nchini Zambia. Reli ya
zamani ya Meter Gauge (MGR) itafanyiwa ukarabati katika vipande vya
Tabora–Kigoma, Kaliua–Mpanda, Tanga–Arusha na Ruvu–Mruazi.
Rais
Samia alisema sekta binafsi itashirikishwa katika uendeshaji wa baadhi ya reli,
hatua itakayoanza na kuingizwa kwa mwendeshaji binafsi kwenye reli ya TAZARA
ili kupunguza gharama za usafirishaji.
Katika
sekta ya anga, Serikali imepanga kuongeza ndege nane kufikia mwaka 2030 ili
kukuza uwezo wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na kupanua safari za ndani
na nje ya nchi. Aidha, Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere kinapangwa kuwa
kitovu cha safari za kimataifa.
Ujenzi
wa viwanja vya ndege vya Msalato, Mwanza, Iringa na Mpanda unaendelea kama
sehemu ya mpango wa kufungua nchi na kuimarisha miundombinu ya uchumi.
Trump athibitisha rasmi kuishtaki BBC
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema atachukua hatua za kisheria dhidi ya
BBC kufuatia jinsi hotuba yake ilivyohaririwa na kipindi cha Panorama, baada ya shirika hilo kuomba msamaha
lakini kukataa kumlipa fidia.
Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya Air
Force One Ijumaa jioni, Trump alisema: “Tutawashtaki
kwa chochote kati ya dola bilioni 1 hadi 5, pengine wiki ijayo.”
BBC imesema uhariri wa hotuba ya tarehe 6
Januari 2021 ulipelekea “taswira isiyo sahihi kwamba Rais Trump alitoa wito wa
moja kwa moja wa kuchochea vurugu.”
Ingawa shirika hilo liliomba msamaha, limesisitiza halitalipa fidia ya kifedha.
Sakata hilo limesababisha kujiuzulu kwa
Mkurugenzi Mkuu wa BBC Tim Davie na Mkuu wa Habari Deborah Turness.
Trump aliwaambia waandishi kuwa anaamini hana
budi kuwashtaki: “Walidanganya. Walibadilisha
maneno yaliyotoka mdomoni mwangu.”
Alisema hakuzungumzia suala hilo na Waziri
Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer, lakini Starmer ameomba kuzungumza naye, na
atampigia simu mwishoni mwa wiki.
Mapema wiki hii, mawakili wa Trump walitishia
kuishtaki BBC kwa fidia ya dola bilioni 1 iwapo haitatoa ufafanuzi wa wazi,
kuomba msamaha rasmi na kumlipa fidia.