Lamine Yamal mashakani kuhusiana na mzozo wa walemavu

Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya Haki za Kijamii ya Uhispania imeitaka ofisi ya mwendesha mashtaka wa nchi hiyo kumchunguza winga wa Barcelona Lamine Yamal baada ya kuripotiwa kuwaajiri watu wenye ulemavu kutumbuiza kwenye sherehe yake ya kutimiza miaka 18.
Lamine Yamal aliandaa karamu siku ya Jumapili katika nyumba iliyokodishwa huko Olivella, mji mdogo ulio kilomita 50 kaskazini magharibi mwa Barcelona, na wageni wakiwemo WanaYouTube, washawishi, na wachezaji wenzake kadhaa wa Barcelona.
Inadaiwa Lamine Yamal alikodisha kikundi cha watumbuizaji walio na ulemavu, jambo ambalo Chama cha Watu wenye Achondroplasia na Dysplasias nyingine za Mifupa nchini Uhispania (ADEE) kilieleza kuwa "halikubaliki katika karne ya 21".
Ilipowasiliana na BBC Sport, Kurugenzi Kuu ya Watu Wenye Ulemavu - sehemu ya Wizara ya Haki za Kijamii, Masuala ya Watumiaji, na Agenda ya 2030 - ilisema: "ADEE imewasilisha malalamiko ya kisheria.
“Kwa hiyo, Kurugenzi Kuu imeitaka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kufanya uchunguzi ili kubaini iwapo sheria na hivyo haki za watu wenye ulemavu zimekiukwa.
ADEE ilisema "inashutumu hadharani uajiri wa watu wenye ulemavu wa ngozi kama sehemu ya burudani," na ikasema itachukua hatua za kisheria kwani "inaendeleza dhana potofu, inachochea ubaguzi, na inadhoofisha taswira na haki" za watu wenye ulemavu.
Katika taarifa ilisema: "Vitendo hivi vinakiuka sio tu sheria za sasa lakini pia maadili ya kimsingi ya jamii inayotaka kuwa na usawa na heshima.
"Sheria ya jumla juu ya haki za watu wenye ulemavu inakataza kwa uwazi vitendo vifuatavyo: 'Maonyesho au shughuli za burudani ambazo watu wenye ulemavu au hali zingine hutumiwa kuchochea dhihaka, au kejeli kutoka kwa umma kwa njia inayopingana na heshima inayostahili utu ni marufuku'."
Hata hivyo, kituo cha redio cha Uhispania RAC1, external kilitangaza mahojiano na mtu aliyedai kuwa mmoja wa waburudishaji waliokuwepo kwenye tafrija hiyo ambaye alimtetea Lamine Yamal.
“Hakuna aliyetudharau, tulifanya kazi kwa amani,” alisema msanii huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina. "Sielewi kwa nini kuna hype nyingi. Sisi ni watu wa kawaida, ambao hufanya tunachotaka, kwa njia ya kisheria kabisa. "Tunafanya kazi kama watumbuizaji. Kwa nini hatuwezi kufanya hivyo? Kwa sababu ya hali yetu ya kimwili? "Tunajua kikomo chetu ni nini na hatutawahi kuvuka: sisi sio nyani."
Mwigizaji huyo alisema ilichukua saa moja, na baadaye watumbuizaji wakajiunga na tafrija hiyo.
"Tunacheza, tunasambaza vinywaji, tunafanya uchawi ... kuna aina nyingi za maonyesho. Kila mtu alikuwa na wakati mzuri."

















