Kiongozi wa zamani wa Nigeria Muhammadu Buhari afariki dunia akiwa na umri wa miaka 82

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa zamani wa Nigeria Muhammadu Buhari, amefariki akiwa na umri wa miaka 82 katika kliniki ya London, alikuwa mtawala wa zamani wa kijeshi na aliyejiita mwanademokrasia alirejea madarakani kupitia uchaguzi lakini alijitahidi kuwashawishi Wanigeria kwamba angeweza kutekeleza mabadiliko aliyoahidi.
Kamwe hakuwa mwanasiasa wa asili, alionekana kama mtu asiye na hisia na mkali. Lakini alibaki na sifa ya uaminifu wa binafsi, jambo adimu kwa mwanasiasa nchini Nigeria.
Baada ya majaribio matatu kufeli, Buhari alipata ushindi wa kihistoria mwaka 2015, na kuwa mgombea wa kwanza wa upinzani nchini humo kushinda.
Mnamo 2019, alichaguliwa tena kwa muhula mwingine wa miaka minne.
Buhari mara zote amekuwa maarufu miongoni mwa maskini wa kaskazini (inayojulikana kama "talakawa" katika lugha ya Kihausa) lakini kwa kampeni ya 2015, alikuwa na faida ya kundi lililoungana la upinzani nyuma yake.
Wengi wa wale waliomuunga mkono walidhani historia yake ya kijeshi na sifa za kinidhamu ndizo ambazo nchi ilihitaji kukabiliana na uasi wa Kiislamu kaskazini. Buhari pia aliahidi kukabiliana na rushwa na upendeleo serikalini, na kuunda fursa za ajira kwa vijana wa Nigeria.
Lakini muda wake madarakani uliambatana na kuporomoka kwa bei ya mafuta duniani na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi nchini humo kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa.
Utawala wake pia ulishutumiwa kwa namna ulivyokuwa ukishughulikia ukosefu wa usalama. Wakati akifanya kampeni aliahidi kulishinda kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Boko Haram. Lakini kundi hilo linasalia kuwa tishio na moja ya mirengo yake sasa inahusishwa na kundi linalojiita Islamic State.
Pia kulikuwa na ongezeko la mapigano makali kati ya wakulima na wafugaji wa kabila la Fulani katikati mwa Nigeria.
Bw.Buhari, Mfula, alishutumiwa kwa kutochukua hatua za kutosha kwa wafugaji au kufanya vya kutosha kukomesha mzozo huo.
Shughuli za wanaojiita majambazi katika eneo la kaskazini-magharibi mwa nchi zilishuhudia kutekwa nyara kwa mamia ya wanafunzi wa shule za sekondari.
Chini ya uangalizi wake vikosi vya jeshi vilishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu kama vile kuwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakipinga ukatili wa polisi kwenye lango la tollgate la Lekki huko Lagos mnamo Oktoba 2020.
Muhammadu Buhari alikuwa nani?
Muhammadu Buhari alizaliwa Desemba 1942 huko Daura katika jimbo la Katsina kaskazini mwa Nigeria, karibu na mpaka na Niger. Wakati huo, Nigeria ilikuwa inadhibitiwa na Waingereza na ilikuwa miaka 18 zaidi kabla ya nchi hiyo kupata uhuru.
Baba yake Buhari, ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka minne, alikuwa kutoka jamii ya Fulani, wakati mama yake, aliyemlea, alikuwa kutoka jamii ya Kanuri.
Katika mahojiano ya 2012, Buhari alizungumza kuwa mtoto wa 23 wa baba yake na wa 13 wa mama yake.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kijana Buhari alisoma shule ya msingi huko Daura na kisha shule ya bweni katika mji wa Katsina. Baada ya kuacha shule, alipelekwa katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Nigeria, akijiunga na jeshi la Nigeria muda mfupi baada ya uhuru.
Buhari alichukua mafunzo ya afisa nchini Uingereza kuanzia 1962-1963 na kisha akaanza kupanda cheo mara kwa mara.
Katika miaka ya baadaye, Buhari alihusisha mwelekeo wake wa nidhamu na kutumia miaka yake ya kielimu katika shule ya bweni, ambapo adhabu ya viboko ilikuwa ya kawaida, na katika jeshi. Alikuwa na "bahati" kupata uzoefu wa mazingira magumu kama haya, ambayo yalimfundisha kufanya kazi kwa bidii, alisema.
Mnamo 1966, kulikuwa na mapinduzi ya kijeshi na kisha kukabiliana na mapinduzi nchini Nigeria , wakati wa msukosuko kwa maafisa wa jeshi lakini Buhari daima alishikilia kuwa alikuwa mdogo sana kuwa na jukumu lolote muhimu.
Chini ya miaka 10 baadaye, chini ya serikali ya kijeshi, Buhari aliinuka na kuwa gavana wa kijeshi wa kaskazini-mashariki, eneo ambalo wakati huo lilikuwa na majimbo sita.
Baada ya chini ya mwaka mmoja, Buhari, ambaye wakati huo akiwa na umri wa kati ya miaka 30, alipandishwa cheo tena, na kuwa kamishna wa shirikisho wa petroli na maliasili (kama waziri wa mafuta) mwaka 1976 chini ya Olusegun Obasanjo katika kipindi chake cha kwanza kama mkuu wa nchi wa Nigeria.
Utovu wa nidhamu na ufisadi
Kufikia 1978, Buhari, wakati huo kanali, alikuwa amerejea kuwa kamanda wa kijeshi. Msimamo wake mkali mwaka 1983, wakati baadhi ya visiwa vya Nigeria vilipochukuliwa katika Ziwa Chad na wanajeshi wa Chad, bado unakumbukwa kaskazini-mashariki, baada ya kulizingira eneo hilo na kuwatimua wavamizi.
Mwishoni mwa 1983 kulitokea mapinduzi mengine, dhidi ya Rais mteule Shehu Shagari, na Buhari, ambaye wakati huo alikuwa meja jenerali, akawa mtawala wa kijeshi wa nchi hiyo.
Kwa maelezo yake mwenyewe, hakuwa mmoja wa wapanga njama lakini aliwekwa (na hatimaye kutupwa) na wale waliokuwa na mamlaka halisi.
Ripoti nyingine zinaonesha alikuwa na jukumu kubwa katika kumwondoa Shagari kuliko alivyokuwa tayari kukiri.
Buhari alitawala kwa muda wa miezi 20, kipindi ambacho kinakumbukwa kwa kampeni dhidi ya utovu wa nidhamu na ufisadi, pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Takribani wanasiasa 500, maafisa na wafanyabiashara walifungwa jela kama sehemu ya kampeni dhidi ya ubadhirifu na ufisadi.
Wengine waliona huu kama ukandamizaji mzito wa utawala wa kijeshi. Wengine wanakumbuka kama jaribio la kusifiwa la kupambana na ufisadi ulioenea ambao ulikuwa unarudisha nyuma maendeleo ya Nigeria.
Buhari alidumisha sifa adimu ya uaminifu miongoni mwa wanasiasa wa Nigeria, wanajeshi na raia, hasa kwa sababu ya kampeni hii.
Kama sehemu ya "vita vyake dhidi ya utovu wa nidhamu", aliamuru Wanigeria kupanga foleni nadhifu kwenye vituo vya mabasi, chini ya macho makali ya askari wanaotumia mijeledi. Watumishi wa umma waliochelewa kazini walidhalilishwa hadharani kwa kulazimishwa kurukaruka kichura.
Baadhi ya hatua zake zinaweza kuonekana kuwa za kificho tu. Lakini nyingine zilikuwa za ukandamizaji wa kweli, kama vile amri ya kuzuia uhuru wa vyombo vya habari, ambapo waandishi wa habari walifungwa.
Serikali ya Buhari pia ilimfungia gwiji mkubwa wa muziki wa Nigeria, Fela Kuti - mwiba kwa viongozi waliofuatana, kwa madai ya uwongo yanayohusiana na mauzo ya fedha nje ya nchi.












