Je, Ruto ndiye rais anayechukiwa zaidi katika historia ya Kenya?

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images
William Ruto wa Kenya aliingia madarakani kwa kujenga matumaini makubwa miongoni mwa watu wa kawaida ambao walitarajia angetimiza ahadi zake za kuboresha maisha yao. Badala yake, anakabiliwa na ukosoaji usiokoma - unaoonekana kuwa mkubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Akionekana kukasirishwa na nguvu ya upinzani, aliuliza Jumatano wiki hii kwa nini hasira kama hiyo ya umma haikuwahi kuelekezwa kwa watangulizi wake, akiwemo Daniel arap Moi, ambaye alitawala kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miongo miwili iliyoadhimishwa na ukandamizaji wa kisiasa na ukiukaji wa haki za binadamu, na wengine walioondoka baada ya uongozi wao kukumbwa na masuala utata.
Jumatano Julai 9, Ruto aliuliza: "Machafuko haya yote, kwa nini hayakuelekezwa kwa (marais wa zamani) Moi, Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta…Kwa nini kuna dharau na kiburi?"
Wachambuzi wanaelezea wimbi la sasa la hasira ya umma dhidi ya Rais Ruto, ambalo limeshuhudia zaidi ya watu 100 wakiuawa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kuwa "lisilo na kifani", na kuwaunganisha Wakenya katika migawanyiko ya kikabila, kidini na kitabaka.
Maandamano dhidi ya utawala wake yalianza mwaka mmoja tu baada ya kuingia madarakani. Miaka mitatu baadaye, Wakenya wengi waliokasirika sasa wanataka aondoke - huku kukiwa na maandamano yasiyoisha na wito wa "Ruto lazima aondoke" na "Ruto Wantam" (Ruto kwa muhula mmoja).
Ruto alipokuwa akiwania urais, alijidhihirisha kuwa mtu wa kawaida, aliyetoka katika maisha ya utotoni yenye umaskini na ustahimilivu. Alitoa wito kwa watu wa kawaida kama mtu ambaye wanaweza kupata msukumo kutoka kwake - baada ya kuinuka kutoka kuwa muuza kuku hadi rais.
Tofauti na hali hiyo na mwanzoni mwa mwaka huu, wakati gazeti moja lilipoandika kichwa cha habari kikiuliza ikiwa Ruto alikuwa "rais anayechukiwa zaidi wa Kenya", hisia ambayo mara nyingi imekuwa ikijitokeza kwenye mitandao ya kijamii na mijadala ya umma.
Inaashiria mabadiliko ya ajabu katika siasa za Kenya, mara nyingi huchangiwa na uaminifu wa kikabila na migawanyiko ya kitabaka. Jinsi Ruto alivyoonekana kuvuka vizuizi hivyo ili kunyakua urais, mienendo hiyo hiyo sasa inaonekana kuwa dhidi yake.

Chanzo cha picha, Gamma-Rapho via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Juma hili msemo "Sisi sote ni Wakikuyu," ulivuma kwenye mitandao ya kijamii huku vijana wakikataa majaribio ya kurejesha migawanyiko ya kikabila ambayo imekuwa ikizikumba siasa za Kenya kwa muda mrefu. Simulizi ya kupingana na "Sisi sote ni Wakenya" iliibuka lakini haikufaulu kupata mvuto sawa - huku wengine wakiiona kama jaribio la kufifisha usemi wa mshikamano katika ujumbe wa kwanza.
Wakikuyu, kabila kubwa zaidi nchini Kenya kutoka eneo la Mlima Kenya, walimuunga mkono kwa kiasi kikubwa Ruto katika uchaguzi wa 2022, pamoja na Rigathi Gachagua, anayetoka eneo hilo, kuwa naibu wake.
Lakini hatua ya kumuondoa Gachagua ofisini mwaka jana kupitia mchakato mkali wa kuondolewa madarakani, ambao aliutaja kama usaliti, ulizua kutoridhika katika eneo hilo. Kufuatia hali hiyo, baadhi ya wanasiasa wanaoegemea upande wa Ruto wamewashutumu Wakikuyu kwa kuchochea upinzani dhidi ya rais.
Mchambuzi wa kisiasa Mark Bichachi anasema upinzani dhidi ya rais hausukumwi kikabila, lakini unafanyika katika jamii mbalimbali mijini na vijijini.
Anataja "malalamiko ya umma dhidi ya rais na serikali" "isiyo na kifani" na "kihistoria", hata kupita misukosuko ya kisiasa ya miaka ya 1980 na 1990 wakati Moi alipoiongoza serikali ya chama kimoja.
Kipindi hicho kilikuwa na dhuluma za kikatili na vita vya umwagaji damu vya demokrasia ya vyama vingi, lakini Bw Bichachi aliiambiambia BBC kwamba hali hiyo haikusababisha shinikizo kama la sasa linalomkabili Rais Ruto, akiongeza kuwa mivutano hiyo ilihusishwa na Vita Baridi na ilionekana kote barani Afrika.
Lakini mwanazuoni Dkt Njoki Wamai anasema ukosoaji unaomlenga rais si jambo la kawaida, lakini ni sehemu ya utamaduni wa kisiasa wakati wa migogoro.
"Marais wote, wanapokwenda kinyume na katiba, kinyume na matakwa ya watu wa Kenya, daima wamekabiliwa na ukosoaji mwingi," aliiambia BBC.
Anaashiria viongozi wa zamani kama vile rais mwasisi Jomo Kenyatta na mrithi wake Moi - ambao wote walikabiliwa na upinzani mkali na kupoteza imani ya umma wakati wa nyakati ngumu - ikiwa ni pamoja na baada ya mauaji ya viongozi wakuu wa kisiasa na jaribio la mapinduzi dhidi ya Moi mwaka wa 1982.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Kilicho tofauti (wakati huu) ni kwamba kiwango cha kuenea kwa habari ni kikubwa," anasema, akibainisha athari za vijana wa Kenya wenye ujuzi wa kidijitali, hivyo upatikanaji wa mkubwa wa mitandao ya kijamii na zana za kidijitali umeongeza majadiliano ya umma.
Pia anaelezea Ruto kama siku zote amekuwa "mtu mwenye msimamo mkali," akipendekeza kuwa mtazamo wake wa kisiasa unakinzana na maadili huria yanayokumbatiwa na Wakenya wengi - hasa vijana.
Tofauti hii ya kiitikadi, anasema, imechangia kuongezeka kwa mvutano.
Kampeni za sasa za upinzani kwa kiasi kikubwa zinaongozwa na vijana, msingi wa mtandaoni, zilizogatuliwa na kuonekana kama zisizo na viongozi, nyingi zinazojitokeza nje ya tabaka la kisiasa lililoanzishwa. Tangu mwaka jana, wamekuwa wakiongozwa na hasira juu ya gharama kubwa ya maisha, kodi kubwa, ufisadi na ukatili wa polisi.
Lakini akiashiria siasa za kikabila na uchochezi kuwa ndizo zinazochochea machafuko ya hivi karibuni zaidi, rais alisema Jumatano: Tuache migawanyiko ya kikabila, chuki, kiburi na dharau. Sisi sote ni Wakenya".
Aliapa kutumia "njia zozote muhimu" kudumisha amani na utulivu. Alitoa wito kwa polisi kuwapiga risasi miguuni waandamanaji waliokuwa wakilenga biashara, badala ya kuwaua. Matamshi yake yalizua hasira na dhihaka zaidi.

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images
Tangu mwaka jana, serikali ya Kenya imejibu maandamano na kutokubaliana na ukandamizaji wa kikatili, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa watu wengi na madai ya kutekwa nyara na maafisa wa usalama.
Ni mkakati ambao mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema umezidisha hasira za umma na kuwatenganisha raia na serikali, huku polisi wakishutumiwa kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano.
Zaidi ya watu 100 wameuawa katika wimbi la maandamano ya kupinga serikali mfululizo tangu Juni mwaka jana. Jumatatu Julai 7 maisha ya watu 38 yaliangamia, ikiashiria siku mbaya zaidi ya machafuko kuwahi kutokea.
Badala ya kutumika kama kichocheo cha mageuzi ya polisi au kushinikiza juhudi za kutuliza waandamanaji, vifo mara nyingi vimetumika kama cheche kwa maandamano yaliyofuata, na kugeuza huzuni kuwa ghadhabu.
Serikali imewalaumu waandamanaji kwa kusababisha ghasia hizo, ikiwashutumu kuvishambulia vituo vya polisi na hata kujaribu kufanya mapinduzi.
Mtaalamu wa mawasiliano ya kisiasa Dkt Hesbon Owilla anayataja machafuko hayo "pengine hasira kali zaidi dhidi ya serikali" katika historia ya Kenya. Anasema imewaleta watu wa tabaka mbalimbali kuungana kwa ukaidi.
Anaelezea jinsi rais anavyowasiliana na wananchi. Anasema ahadi za Ruto za kuinua ustawi wa watu wa kawaida zilikuwa "halisi, halisi kabisa" na kuhamisha kampeni kutoka kwa uhamasishaji wa kikabila kuelekea siasa za msingi.
"Kisha akawa rais. Bado tunasubiri. Yale ambayo Wakenya wanapitia ni mabaya zaidi," anaiambia BBC, akibainisha hisia kubwa za kusikitisha miongoni mwa Wakenya wengi.
Anasema tofauti na serikali zilizopita ambazo zilitoa ahadi za tahadhari, Ruto alitoa na anaendelea kutoa, na kusababisha kupotea kwa matarajio.
"Kukatishwa tamaa kunasababisha hasira," anasema
Akitoa mfano wa agizo la kuwafyatulia risasi waandamanaji, pia anasema kuwa rais mara nyingi huzungumza wakati ukimya unaweza kumsaidia vyema - akijiweka wazi kupita kiasi na kuyafanya masuala mazito ya kitaifa kuhisi kuwa ya kibinafsi.
Matokeo yake, kunapokuwa na ukosoaji, huwa unaelekezwa kwake, badala ya kuhusishwa na kushindwa kwa mifumo ya utawala.
Hata hivyo, Ruto ameangazia mara kwa mara juhudi za utawala wake kuboresha maisha ya Wakenya wote, akiashiria mradi wa serikali wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, mpango wa afya kwa wote, kazi za kidijitali, na mpango wa ajira za ng'ambo kama mafanikio muhimu.
Alipokuwa akikagua mojawapo ya maeneo ya makazi wiki hii, alikiri ukubwa wa ukosefu wa ajira kwa vijana lakini akasisitiza kuwa tatizo hilo lilikuwepo kabla ya urais wake.
Alisisitiza kuwa serikali yake ilikuwa ya kwanza kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na mzozo huo, akitaja mipango ya serikali kama vile mradi wa nyumba ambao anasema umeunda mamia kwa maelfu ya nafasi za kazi.
Rais aliomba subira, kwani tatizo hilo lingechukua muda kutatuliwa.
Hata hivyo, subira haswa huku kukiwa na gharama ya juu ya maisha, matarajio ambayo hayajatimizwa, na kukata tamaa kunakoongezeka, si jambo ambalo Wakenya wengi wanahisi wanaweza kulimudu.
Baadhi ya programu hizo kuu na za mfano zimekuja kwa gharama kubwa kwa Wakenya, ambao sasa wana asilimia 1.5 ya ushuru wa nyumba na ushuru wa bima ya afya wa 2.75% inayokatwa kwenye mapato yao ya kila mwezi. Maumivu ya kulipa baadhi ya kodi hizi za juu yametawala mazungumzo ya kila siku, hasa kwa maoni kwamba ushuru wa juu haujaonekana katika huduma bora za umma.
Kwa sifa ya serikali, Dk Owilla anasema baadhi ya mipango, kama vile mradi wa huduma ya afya kwa wote, imekuwa na matokeo makubwa, na mingine inaweza hatimaye kuwa na faida kwa wengi.
Lakini Bw Bichachi anahoji kuwa serikali "imepoteza jinsi watu wanavyohisi", na sauti yake imesalia bila kubadilika licha ya chuki ya umma kuongezeka.
Anasema suala hilo haliwezi kubadilika kulingana na jinsi serikali inavyofanya kazi - akielezea kama "uhusiano wa upendo na chuki " kati ya watu na urais.
Hivyo ndivyo "tunajukuta hapa tulipo", anamalizia, akirejelea chuki kali ambayo sasa inakabiliwa na rais, ambaye wakati mmoja alikuwa mmoja wa "viongozi waliopongezwa na kusifiwa sana waliowahi kutokea nchini Kenya".
Imetafsiriwa na Florian Kaijage











