Ni nchi gani zenye silaha za nyuklia na zilizipataje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Miaka 80 baada ya Marekani kulipua bomu la kwanza la nyuklia, mpango wa nyuklia wa Iran umekuwa katikati ya ongezeko kubwa la uhasama katika Mashariki ya Kati.
Tarehe 2 Julai, rais wa Iran alitia saini sheria ya kusitisha ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), baada ya Israel na Marekani kushambulia vituo vyake vya nyuklia mwezi Juni.
Israel na Marekani zote zimesema mashambulizi hayo yalikuwa muhimu ili kuzuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.
Bado haijafahamika ni kiasi gani hasa cha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi hayo na matokeo yake yanaweza kuwa nini kwa eneo hilo na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia Uenezi (NPT), ambao ulianza kutekelezwa miaka 55 iliyopita na umesaidia kupunguza kuenea kwa silaha za nyuklia.
Nchi tisa zinajulikana kuwa na silaha za nyuklia. Walizipataje na wengine je wanaweza kuzipata?

Chanzo cha picha, Getty Images
Nani ana silaha za nyuklia?
Marekani, Urusi, Uingereza, China, Ufaransa, India, Pakistan, Israel, na Korea Kaskazini zinajulikana kumiliki silaha za nyuklia, ingawa Israel ndiyo pekee kati ya hizi ambayo haijawahi kuthibitisha rasmi hili.
Marekani imekuwa nchi ya kwanza yenye nguvu za nyuklia baada ya kutengeneza silaha hizo kwa siri kama sehemu ya Mradi wa Manhattan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Marekani ilipeleka silaha hizo kwa madhara makubwa mwaka 1945, kwa kurusha mabomu ya atomiki huko Hiroshima na Nagasaki nchini Japan, ambayo ilikuwa moja ya nguvu za Axis - muungano wa kijeshi ambao pia ulijumuisha Ujerumani ya Nazi na Italia na ambao majeshi washiriki walikuwa wakipigana nao.
Milipuko hiyo inakadiriwa kuua watu wasiopungua 200,000. Huu ndio wakati pekee ambapo silaha za nyuklia zimetumika katika migogoro.
Mtaalamu wa udhibiti wa silaha Dkt. Patricia Lewis anasema hii ilikuwa "safari halisi ya harakati za silaha za nyuklia", na kuzifanya nchi nyingine, hasa Umoja wa Kisovieti, kutafuta kwa haraka kuunda silaha zao za nyuklia, kama njia ya kuzuia dhidi ya mashambulizi na kuendeleza nguvu yake kikanda na kimataifa.
Nini kilitokea baadaye?
Chini ya miaka miwili baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kumalizika, Vita Baridi vilianza - pambano la kuwania madaraka duniani kote kati ya Marekani na Muungano wa Kisovieti na washirika wa pande zote mbili ambalo lilidumu kwa zaidi ya miaka 40 na nyakati fulani kutishia kuzidi kuwa mzozo wa nyuklia.
Wanasovieti walikuwa wameanza majaribio ya kutengeneza bomu la atomiki wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kufaulu mwaka wa 1949 walipofanya jaribio la mafanikio, na kumaliza ukiritimba wa Marekani juu ya silaha za nyuklia. Baada ya hayo, pande zote mbili zilitafuta kutengeneza silaha za nyuklia ambazo zilikuwa hatari zaidi.
Katika kipindi cha miaka 15 iliyofuata, nchi tatu zaidi zikawa nguvu za nyuklia.
Mnamo 1952, Uingereza, ambayo ilishirikiana na Marekani katika utengenezaji wa silaha za nyuklia wakati wa Vita vya Kidunia vya pili, ikawa ya tatu, ikifuatiwa na Ufaransa mnamo 1960 na Uchina mnamo 1964.
Ni lini nchi zingine zilipata silaha za nyuklia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kufikia miaka ya 1960, mataifa matano yenye nguvu za nyuklia - Marekani, Umoja wa Kisovieti, Uingereza, Ufaransa, na Uchina - yalikuwa imara. Lakini hofu iliongezeka kwamba idadi ya mataifa yenye silaha za nyuklia inaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kwa kujibu, Umoja wa Mataifa ulianzisha Mkataba wa Kuzuia Uenezaji (NPT), uliopangwa kuzuia kuenea zaidi kwa silaha za nyuklia, kukuza upokonyaji silaha, na kuwezesha matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.
Mkataba huo ulianza kutumika mnamo 1970, lakini sio nchi zote zilitia saini, na silaha za nyuklia zilienea.
India ikawa nchi yenye nguvu ya nyuklia mwaka wa 1974 na Pakistan mwaka 1998. Hakuna nchi iliyotia saini mkataba huo, kwa sehemu kwa sababu ya wasiwasi wa usalama kila mmoja alikuwa na mwenzake.
Israel pia haijawahi kutia saini mkataba huo.
Maafisa wa Israel wamekuwa wakiashiria vitisho na mivutano ya kikanda na uadui wa majirani zake wengi dhidi yake kama sababu za kutotia saini mkataba huo. Imedumisha sera ya utata wa nyuklia - yaani, kutothibitisha au kukataa umiliki wa silaha za nyuklia.
Awali Korea Kaskazini ilitia saini makubaliano hayo, na kujiondoa mwaka 2003, ikilaumu mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini.
Mnamo 2006, ililipuwa silaha ya nyuklia katika jaribio. Sudan Kusini, ambayo ilianzishwa mwaka 2011, ni nchi nyingine pekee mwanachama wa Umoja wa Mataifa ambayo haijatia saini mkataba huo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, Iran ina silaha za nyuklia?

Chanzo cha picha, Getty Images
"Tunachojua" Iran bado haijatengeneza bomu, anasema Andrew Futter, profesa wa siasa za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Leicester nchini Uingereza na kuongeza: "Lakini kiufundi au kiteknolojia, hakuna sababu ya kweli kwa nini hawawezi kufanya hivyo."
Iran ambayo ilitia saini Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa silaha za nyuklia imekuwa ikisema kila mara mpango wake wa nyuklia ni wa amani na kwamba haijawahi kutaka kutengeneza silaha za nyuklia.
Hata hivyo, uchunguzi wa muongo mzima wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, ulipata ushahidi kwamba Iran ilifanya "shughuli mbalimbali zinazohusiana na utengenezaji wa silaha za nyuklia" kutoka mwishoni mwa miaka ya 1980 hadi 2003, wakati miradi chini ya kile kilichojulikana kama "Project Amad" ilisitishwa.
Mnamo mwaka wa 2015, Iran ilikubali makubaliano na mataifa sita yenye nguvu duniani ambapo ilikubali vikwazo katika shughuli zake za nyuklia na kuruhusu ufuatiliaji wa wakaguzi wa IAEA ili kupata msamaha kutoka kwa vikwazo vya kimataifa.
Lakini Rais wa Marekani Donald Trump aliachana na makubaliano hayo wakati wa muhula wake wa kwanza mwaka 2018, akisema IAEA ilifanya kidogo sana kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia, na akarejesha vikwazo. Iran ililipiza kisasi kwa kukiuka mara kwa mara vikwazo vya IAEA, hasa vile vinavyohusiana na kurutubisha uranium.
Mnamo tarehe 12 Juni 2025, bodi ya magavana wa IAEA ya mataifa 35 ilitangaza Iran, kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20, kwamba ilikiuka majukumu yake ya kutoeneza nguvu za kinyuklia.
Siku iliyofuata, Israel ilianzisha mfululizo wa mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran na kijeshi. Baadaye iliungwa na mshirika wake wa karibu, Marekani, ambayo ilishambulia vituo vitatu vya nyuklia vya Iran, ikiwa ni pamoja na kituo cha chini ya ardhi cha Fordo.
Je, Israel ina silaha za nyuklia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Israel haijawahi kuthibitisha rasmi kuwa inamiliki silaha za nyuklia lakini inaaminika kuwa ina silaha kubwa.
Mnamo Oktoba 1986 fundi wa nyuklia wa Israel, Mordechai Vanunu, alitoa maelezo kwa gazeti la Uingereza la Sunday Times kwamba Israel ilikuwa na mpango mkubwa zaidi wa silaha za nyuklia kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.
Kwa hili alifungwa gerezani huko Israeli kwa miaka 18, na akaachiliwa mnamo 2004.
Kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), taasisi ya wataalam, Israel inaboresha silaha zake za kisasa.
Mnamo 2024, Israeli ilifanya jaribio la mfumo wa kusukuma kombora "ambalo linaweza kuhusishwa na familia yake ya Yeriko ya makombora yenye uwezo wa nyuklia" na inaonekana kuboresha eneo lake la uzalishaji wa plutonium huko Dimona, SIPRI inasema.
Israel imechukua hatua za kijeshi kuzuia wapinzani wa kikanda kupata uwezo wa nyuklia.
Mbali na mashambulizi yake dhidi ya Iran, ililipua kinu cha nyuklia nchini Iraq mwaka 1981 na eneo linaloshukiwa kuwa la nyuklia nchini Syria mwaka 2007.
Ni nchi gani zilizoacha programu za nyuklia?
Nchi nyingine, kama vile Brazili, Uswidi na Uswizi, zilianza kufanya kazi katika kuunda silaha za nyuklia na baadaye kuachana na programu zao kwa hiari au kutokana na shinikizo kutoka nje.
Afrika Kusini ndiyo nchi pekee duniani iliyofanikiwa kutengeneza silaha za nyuklia na kisha kuzisambaratisha ..
"Hilo bado linaonekana kuwa jambo muhimu sana katika enzi ya nyuklia - ya serikali ambayo iliunda silaha zake za nyuklia na kisha ikaamua kuziharibu ," anasema Futter.
Uamuzi huo ulisukumwa na mchanganyiko wa mambo, ikiwa ni pamoja na kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi, kupungua kwa migogoro ya kikanda, na mabadiliko ya mienendo ya kisiasa duniani.
Baada ya kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti mwaka wa 1991, nchi tatu mpya zilizokuwa huru - Ukraine, Belarus, na Kazakhstan - zilirithi silaha za nyuklia lakini zikaacha. Ukraine ilitoa silaha zake kama malipo ya dhamana ya usalama kutoka Marekani, Uingereza, na Urusi chini ya Mkataba wa Budapest wa 1994.
Lakini Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amerudia mara kwa mara kwamba amepata usaidizi mchache licha ya kuacha silaha zake za nyuklia .

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuna silaha ngapi za nyuklia?
Kwa sababu ni nadra serikali kufichua maelezo kamili ya silaha zao za nyuklia, ni vigumu kujua ni silaha ngapi kila nchi inazo.
Lakini kwa mujibu wa shirika la wataalam la SIPRI, mataifa yenye nguvu za nyuklia duniani yalikuwa na jumla ya vichwa 12,241 vinavyokadiriwa kufikia Januari 2025, huku Urusi na Marekani zikishikilia takriban 90% ya hifadhi ya kimataifa.
Ingawa kuvunjwa kwa vichwa vya vita vilivyostaafu kwa ujumla kumepita kasi ya kutuundwa kwa vichwa vipya, mwelekeo huu unaweza kurudi nyuma "katika miaka ijayo", kundi la wataalam linasema.
Je, nchi zaidi zinaweza kutengeneza silaha za nyuklia?
Kinachotokea kwa mpango wa nyuklia wa Iran huenda kikaathiri iwapo mataifa mengine yatazingatia kuunda silaha za nyuklia, wataalam wanasema.
Kufuatia mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran mwezi Juni, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa mpango wa nyuklia wa Iran umerudishwa nyuma kwa "miongo kadhaa".
Mwezi Julai, Pentagon ilisema mashambulizi ya Marekani yameshusha hadhi ya mpango wa nyuklia wa Iran kwa hadi miaka miwili.
Iwapo Iran hatimaye itatengeneza silaha za nyuklia, nchi nyingine za Mashariki ya Kati, hasa Saudi Arabia, zinaweza kutafuta kutengeneza silaha zao wenyewe, anasema Futter.
"Nadhani Saudi Arabia imekuwa wazi kwamba kwa sasa hawataki uwezo wa nyuklia, lakini Iran yenye silaha za nyuklia ingebadilisha uamuzi huo kabisa," anasema.
"Jinsi ya kufanya hivyo kwa haraka ni swali lingine."
Dkt. Lewis anasema kuna "hatari kubwa" ya Iran kujiondoa kutoka NPT, ambayo kwa upande wake itaongeza uwezekano wa wengine kuondoka. Hili litakuwa "pigo kwa shirika hilo" lakini sio mbaya, anasema.
Lakini hata kama mataifa mengine yataamua kujaribu kuunda silaha za nyuklia, Dkt Lewis anasema kuna changamoto kubwa, hasa kupata urani iliyorutubishwa au plutonium ya kiwango cha silaha, ambayo yote yanadhibitiwa kikamilifu.
Pia anaangazia mzigo wa kifedha.
"Ni ghali na inachukua miaka - hasa ikiwa inafanywa kwa siri. Lakini hilo halijazuia nchi maskini kama vile Korea Kaskazini na Pakistan."
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












