Uchaguzi wa Nigeria 2023: Chati zinazoelezea changamoto za taifa hilo
Kama nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika na yenye watu wengi zaidi - watu milioni 214 - kinachotokea Nigeria kina athari kubwa.
Wapiga kura wanatazamiwa kumchagua rais mpya baada ya miaka minane chini ya Muhammadu Buhari lakini yeyote atakayeshinda atakabiliwa na changamoto kali.
Katika chati zifuatazo, ni baadhi ya changamoto zinazowazonga wapiga kura.


Mwaka jana, Wanigeria - kama watu duniani kote - wameathiriwa na kupanda kwa bei za vyakula kulikosababishwa na mzozo unaoendelea nchini Ukraine.
Lakini bei zilikuwa zikipanda kabla ya mapigano hayo kuanza - kulikosababishwa na kufungwa kwa mpaka kulikozuia bidhaa nyingi kutoka nje kuingia ndani na uhaba wa fedha za kigeni.
Kwa ujumla, mfumuko wa bei mnamo 2022 ulikuwa chini ya 19%, ikiwa ni juu zaidi katika kipindi cha miongo miwili.
Chakula kikuu - vipande vya muhogo - imekuwa moja ya bidhaa zilizoathiriwa kidogo, lakini kupanda kwa bei ya bidhaa nyingine muhimu kama vile nyanya na mafuta ya kupikia kunasababisha athari kubwa kwa familia.


Iwapo rais mpya anataka kuwasaidia watu kwa kuzingatia gharama ya vitu vya msingi, watakabiliwa na tatizo ambalo tayari serikali inatumia zaidi ya inavyopokea.
Kiasi kikubwa kinatumika katika kutoa ruzuku ya petroli na taifa linalozalisha mafuta halijaweza kutumia fursa ya bei ya juu ya mafuta kwa kuwa ina uwezo mdogo wa kusafisha mafuta na inabidi kuagiza tena petroli.
Wachambuzi wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu uendelevu wa deni la umma huku gharama ya kulipa riba yake ikizidi mapato ya serikali mara kwa mara katika 2022.


Kama mojawapo ya wazalishaji wakuu wa mafuta barani Afrika, Nigeria imetegemea dhahabu nyeusi kwa mapato ya serikali na pia chanzo cha fedha muhimu za kigeni.
Hata hivyo, nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta haijafanikiwa kutumia fursa ya fedha zinazozalishwa - nyingi zimeibiwa au kutumika vibaya.
Na uzalishaji wa mafuta umekuwa ukipungua katika miaka kumi iliyopita. Mnamo 2022 ilishuka hadi kiwango cha chini kabisa katika miaka 30.
Wizi wa mafuta na uharibifu umelaumiwa kwa upotevu wa pato.
Hii, pamoja na uwekezaji mdogo wa miaka mingi na umri wa maeneo yenye mafuta, ina maana kwamba Nigeria iko nyuma ya mataifa mengine ya Afrika yanayozalisha mafuta.


Huku nusu ya Wanigeria wakiwa chini ya umri wa miaka 18, viongozi wa nchi hiyo wanakabiliwa na changamoto ya jinsi ya kuwatumia vijana hawa.
Wanahitaji kusaidia uchumi kukua ili kutimiza mahitaji na matarajio ya vijana hao wote.
Hata kukiwa na watu wengi wadogo mno kuweza kupiga kura, asilimia 40 ya wapigakura waliojiandikisha wako chini ya umri wa miaka 35, na kuwafanya kuwa muhimu katika uchaguzi. Kuwavutia moja kwa moja kunaweza kuathiri matokeo ya uchaguzi.


Jambo la kwanza ambalo vijana wengi wa Nigeria wanataka ni kazi.
Hivi sasa thuluthi moja ya Wanigeria wanaotaka kufanya kazi hawana ajira.
Linapokuja suala la vijana, zaidi ya nusu ya wale kati ya 15 na 24 wanatafuta ajira.
Hatua za kukabiliana na janga la Covid hakika zilikuwa na athari lakini viwango vya ukosefu wa ajira vilikuwa vikiongezeka kabla ya kuzuka kwa virusi hivyo.
Uchumi umekua tangu 2015, lakini sio haraka vya kutosha kuchukua watu wote wapya wanaotafuta kazi.
Ukosefu wa usalama umetajwa kuwa moja ya sababu za ukuaji mdogo, lakini wanauchumi pia wamelaumu hatua zingine kama vile vikwazo vya sarafu na kufunga mipaka kuzuia bidhaa nyingi za nje kuingia nchini humo kama kukatisha tamaa uwekezaji.


Kiwango cha ufikiaji wa baadhi ya miundombinu ya kimsingi ambayo inaweza kuboresha urahisi wa kufanya biashara, pamoja na maisha ya kila siku, ni ya chini.
Hali mbaya ya mtandao wa umeme kwa muda mrefu imekuwa chanzo cha ukosoaji na ni karibu 55% tu ya watu wanapata umeme, kulingana na takwimu za Benki ya Dunia.
Na linapokuja suala la matumizi ya mtandao, ni 36% tu ya Wanigeria wanaotumia mtandao, jambo ambalo linaiweka katikati ya kundi la nchi za Afrika Magharibi.

Kukabiliana na kuongezeka kwa viwango vya ghasia nchini Nigeria kutakuwa kipaumbele kikuu kwa rais ajaye.
Wakati Rais Buhari alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015, tishio kutoka kwa kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Boko Haram kaskazini-mashariki ndilo lililokuwa wasiwasi mkubwa zaidi.
Ingawa hawadhibiti tena eneo kubwa, ongezeko la utekaji nyara, mashambulizi yanayochochewa kisiasa, mivutano ya wakulima na wafugaji, ghasia za uhalifu, pamoja na ukatili wa polisi, hudhoofisha imani katika serikali kuweka watu salama.
Hili si suala tena ambalo kwa kiasi kikubwa linatatiza kaskazini-mashariki - tatizo sasa limeenea kote nchini.

Mmoja kati ya watoto watano duniani ambao hawako shuleni wako Nigeria, kulingana na shirika la watoto wa Umoja wa Mataifa, Unicef.
Ingawa hii ni taswira ya ukubwa wa idadi ya vijana nchini humo, ukweli kwamba karibu 40% ya watoto kati ya miaka 5-11 hawako shuleni, hilo ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa.
Hili ni suala la nchi nzima lakini viwango vya mahudhurio, kwa ujumla, ni vibaya zaidi kaskazini. Baadhi ya maeneo haya yameathiriwa na ukosefu wa usalama, lakini jinsia na umaskini pia ni sababu.

Soma zaidi:
- https://www.bbc.com/swahili/articles/c4ne3lyk5rro
- https://www.bbc.com/swahili/articles/c1vn93gxe4lo
- Ni nani yuko kwenye kinyang'anyiro cha kuiongoza Nigeria?













