Bajeti Afrika Mashariki ni utamu mchungu

Chanzo cha picha, EAC
- Author, Beatrice Kimaro
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Juni 14, 2022 ilikuwa siku ya bajeti kwa nchi za Afrika Mashariki, Tanzania na Uganda zikiwasilisha makadirio ya bajeti zao kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Kenya iliwasilisha nyuma kidogo kutokana na maandalizi ya uchaguzi.
Bajeti hizi zinawasilishwa wakati mgumu wa vita vya Ukraine na Urusi, huku janga la Corona likiendelea kuathiri shughuli na watu katika maeneo mengi duniani.
Bajeti za mwaka huu katika nchi karibu zote za Afrika Mashariki, zimekusanya mambo matamu yanaofurahisha na yanayogusa watu wengi, lakini pia zina misumari ya moto, inayoweza kuchoma, na kukumiza.
Tanzania
Bajeti ya Tanzania ni ya kihistoria, ikitajwa kuwa ni bajeti ya kipekee kutokana na muelekeo wake achilia mbali kiwango chake kikubwa cha shilingi trilioni 41 za kitanzania. Bajeti hii imejikita kwenye kupunguza matumizi ya serikali na kwenye sera ya mapato ikitaka kuongeza mapato yake yatakayotumika kwenye maendeleo na huduma za kijamii.

Kila mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea atapewa namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) na atakadiriwa kodi zake na kutumiwa kwa njia ya mtandao na kulipa kulingana na kipato chake. Hili lina uchungu kwa baadhi ya watanzania.
'ni jambo jema, lakini halifurahishi masikioni kwa wasiotaka kulipa kodi, litaisaidia kuongeza kipato, wako wengi wasiolipa kodi kwa kutokuwa na TIN,'.
Mbali na hili, bajeti ya sasa imelenga kupunguza matumizi ya serikali, kwa kuleta mfumo wa kuwakopesha magari watumishi wa umma, zoezi linalo kwenda kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 500 za kitanzania. Hili si jema kwa maafisa wa serikali waliokuwa 'mabosi' wa magari.
Elimu bure mpaka kidato cha 6, ni jambo lililo furahisha wengi Tanzania, lakini kufumuliwa kwa mfumo wa manunuzi na mapendekezo ya kurekebisha sheria ya manunuzi, kupunguza udanganyifu na wizi katika zabuni za serikali, linakwenda kuliza maafisa wengi na wafanyabiashara wadanganyifu.
Uganda
Uganda iliyopoteza zaidi ya watu 3,000 kwa ugonjwa Covid-19 imeongeza bajeti yake kwa asilimia 7%. Waziri wa fedha wa Uganda, Matia Kasaija aliwasilisha bajeti ya shilingi za Uganda trilioni 48.1 sawa na dola bilioni 12.8$, bajeti iliyojielekeza kwenye kurekebisha uchumi wake ulioathiriwa na janga la Corona lakini pia kushughulikia ugonjwa huo.

Utamu wa bajeti ya nchi hii, ni kutokuwepo kwa kodi yoyote mpya itakayo ongezwa katika mwaka ujao wa fedha ili kutoa unafuu kwa wafanyabiashara na wananchi wake kwa ujumla.
Pamoja na hilo, bajeti ya Uganda haionekani kubana matumizi ya serikali kama ilivyojionyesha kwa bajeti ya Tanzania ya mwaka huu.
Kiasi kikubwa cha fedha kilichotengwa kwa matumizi ya Ikulu na taasisi nyingi za serikali zinaitofautisha bajeti hii na ile ya Tanzania, ambayo inazitoa fedha kwenye matumizi yasiyo ya lazima ya maafisa wa serikali na kuzielekeza kwenye huduma za kijamii
Hofu ya waganda wengi ni uhuru wa kuhoji, uhuru wa maafisa kutumia taaluma zao, lakini halijaifanya serikali ya nchi hiyo kusema mipango yake ni ya kuwasaidia wananchi.
Kenya
Kenya yenyewe iliwasilisha bajeti yake mapema kidogo kwa sababu ya shughuli za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Bajeti ya shilingi za Kenya trilioni 3.3 ikiwa ni ongezeko la 4.8% ukilinganisha na bajeti iliyopita ya 2.9%, inaonyesha kushughulikia kupanda kwa gharama za maisha, tatizo la ajira kwa vijana, utofauti wa kipato, na deni la taifa.

Chanzo cha picha, SOPA IMAGES
Uchungu wa bajeti hii ya Kenya ni kwamba, kiasi kikubwa cha fedha zinazokadiriwa kufikia Sh2.01 trillion za Kenya zitakwenda kutumika kwenye shughuli za kawaida za serikali, badala ya miradi ya maendeleo.
Lakini kutengwa kwa Sh24.7 billion kama ruzuku ya mafuta ili kupunguza mzigo wa bei , ni jambo la kufurahisha kwa wakenya ambao katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, wanashuhudia ongezeko kubwa la bei ya mafuta hasa ya petrol na diezeli.
Lingine la kufurahisha ni bajeti hiyo kujali hali ya ukame inayoyakumba mara kwa mara maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Mwaka jana zaidi ya wakenya milioni mbili walikumbwa na janga hili.
Je ni bajeti zinazogusa maisha ya watu au kama zilizotangulia?
Mchumi, Barnos Willium kutoka chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, anasema, 'kuwasilisha bajeti ni suala moja, kuitekeleza na kufikia malengo kwa ufanisi ni jambo lingine'.
Mtazano wa mchumi huyu, ni mitazamo ya wafuatiliaji wengi wa masuala ya bajeti. Kila mwaka katika kila nchi, huwasilishwa bajeti, lakini utekelezaji wake huwa ni wa kusuasua sana.
'Zinavutia kwa masikio, lakini hazitakuwa na maana kama hazitatekelezwa, naiona bajeti ya Tanzania ni tofauti sana na miaka yote, kama itatekelezwa, inaweza kuleta utofauti mkubwa wa ukusanyaji wa mapato na katika uwekezaji', alisema Willium.
Bajeti ya Tanzania mwaka huu kama ilivyo ya Kenya, inajikita kwenye sera ya mapato na uwekezaji. Uwekezaji unaoonekana kwenye bajeti ya kilimo iliyoongezwa kwa karibu asilimia 10% kwa lengo la kuongeza mashamba makubwa na kuongeza eneo la umwagiliaji.
Kama itatekelezwa inavoonekana inaweza kuongeza ajira mpaka milioni 3 katika kipindi cha mwaka mmoja tu. Huku ile ya Uganda ikiongeza ajira mpaka milioni 1.
Pamoja na utamu wa uchungu wa bajeti za sasa za nchi za Afrika Mashariki, ukakasi wa ongezeko la deni la taifa kwa nchi zote, inaleta wasiwasi. Tanzania deni limefikia trilioni 69, Uganda 73.5 trilioni za Uganda na kule Kenya ni trilioni 8.
Madeni haya yanaleta kigugumizi kwenye jitihada zinazoonekana kupitia bajeti zao katika kukuza uchumi wa mataifa hayo na kuboresha maisha ya wananchi.















