Tanzania:Uchumi wa Tanzania umestahimili vipi athari za corona?

Chanzo cha picha, EAC
- Author, Alli Mutasa
- Nafasi, BBC Swahili
Ikiwa uchumi wa nchi zote sita za wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki , zikivumilia athari za janga Covid-19, uchumi wa Tanzania waonekana kuongezeka,.
Lakini hayo ni matokeo ya ukuaji endelevu wa miongo miwili mfululizo, mpaka Tanzania kutangazwa nchi ya mapato ya wastani kutoka mapato ya chini, mnamo Julai 2020.
Ni kwa muda mrefu Kenya imevishwa kilemba cha uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki, jambo ambalo lina uhalisia. Takwimu zinaonesha Zao Ghafi la Ndani la Kenya lilikuwa zaidi ya $100; Tanzania, kasoro ya $65, huku Uganda kasoro ya $38 kwa mwaka 2020.
Kuna habari njema kuwa Tanzania itatwaa hadhi ya uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki mnamo mwongo mmoja hivi kutokana na uchumi wake kukua kwa kasi kubwa; sasa ina mamilionea wengi zaidi kuishinda Kenya.
Zipi sababu zilizoipelekea Tanzania kuipiku Kenya katika biashara za Afrika Mashariki?

Sababu ni nyingi na tofauti, lakini moja kubwa ni mafao linganishi baina ya nchi hizo mbili; na pili, historia ya kiuchumi.
Punde baada ya uhuru, mnamo miaka ya 1960 na 1970, nchi hizo mbili zilienda njia tofauti za maendeleo. Kenya iliamua kufuata mfumo wa kibepari, na hivyo kuweka uchumi mbele, siasa nyuma, sekta binafsi ikakita mizizi.
Tanzania ilienda kinyume chake, ilifuata sera za kujitegemea, uchumi dhibiti - kuweka siasa mbele, uchumi nyuma chini ya mfumo wa ujamaa. Tanzania iliweka kipaumbele kusaidia nchi za kusini mwa Afrika kupata uhuru wao. Hivyo kupelekea nchi za magharibi kama Uingereza na Marekani kutovutiwa na msimamo wa Tanzania na kuisusa kwa vikwazo vya kiuchumi; ilhali Kenya ilipendelewa kwa misaada ikasonga mbele na hasa katika sekta ya viwanda.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kati ya mwaka 1982 hadi 1984, kwa mujibu wa Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF), uchumi wa Tanzania ulikuwa mkubwa kuliko wa Kenya. Mnamo mwaka 1986, Nairobi iliipiga kikumbo Dar es Salaam, na kuanzia 1987 Kenya kurudia nafasi ya kwanza kiuchumi na kuvutia uwekezaji wa mashirika ya kimataifa. Hata hivyo, Mwalimu Julius Nyerere, alisisitiza Kenya ni nchi inayoendelea mbele tu kama Tanzania.
Ukombozi wa Afrika Kusini ulipopatikana, mkakati wa uchumi wa Tanzania ukaanza kufanyiwa mageuzi, ikiweka uchumi mbele, siasa nyuma - hususan enzi ya Benjamin Mkapa, zaidi ya miaka 10 tangu Mwalimu ang'atuke madaraka. Sekta binafsi ikaruhusiwa kufukuta. Uchumi wa Tanzania ulipata ukuaji wa haraka, kipindi cha miaka 20 hadi 2020, karibu mara saba; wakati Kenya ulikua mara tano.
Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah, aliwahi kusema muhimu si tu ulipofika lakini pia wapi umeanzia. Kwa mfano, takwimu za IMF zinaonesha zao ghafi la ndani la Kenya katika 1997 lilikuwa kasoro ya $14bn ilhali la Tanzania zaidi ya $6bn, yaani uchumi wa Kenya ulikuwa mkubwa kwa 114%, zaidi ya uchumi wa Tanzania.
Leo uchumi wa Kenya, kwa mujibu wa tarakimu za sasa, unazidi wa Tanzania kwa 37% tu. Na IMF inatabiri mwakani 2022, uchumi wa Kenya utakuwa $113bn kwa $78bn wa Tanzania; wa Kenya ukizidi kwa 30% - kwa makadirio lakini ni inaweza kupunguka.

Chanzo cha picha, AFP
Rais Samia Suluhu Hassan amerithi kiti cha urais mnamo Machi 2021, baada ya kifo cha hayati John Magufuli lakini pia uchumi unaokua na wenye mbinu zinazostahili - kupaumbele ikiwa ni juhudi za kupiga vita ufisadi na ubadhirifu, kuimarisha mifumo ya miundombinu, utawala wa umma na uwajibikaji na uendeshaji bora wa raslimali za umma kwa manufaa ya kijamii.
Ni katika mpango wa Maendeleo ifikapo 2025, kama nchi ya mapato-wastani, ikiwa na moyo wa maisha bora, amani, utulivu, na utawala bora, jamii inayosoma na kuelimika vyema, sekta binafsi inayohimili ukuaji endelevu kijamii, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza mpango kabambe wa kukuza uwekezaji na mazingira mazuri kwa biashara - uchumi mbele, siasa nyuma.
Akilihutubia bunge kwa mara kwanza kama rais, Mama Samia alisema: "Serikali itachukua hatua mahsusi kukuza uwekezaji kwa kuzihakiki sera, sheria na kanuni za uwekezaji, kuondoa masharti yanayokawiza uwekezaji zikiwemo sera zinazobabaisha, mfumo dhaifu wa kodi, na utawala usiofaa". Na papo kuonya katu serikali yake haitovumilia mwenendo mbaya, uzembe, wizi, na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Sera hizo zina lengo la kuelekea katika kile wachumi hukiita mafao na gharama linganishi; hususan katika soko la Afrika Mashariki, bila kuzibia macho na masikio masoko mengine ng'ambo za Afrika na nje.

Soko moja la Afrika Mashariki ni jungu kuu, halikosi ukoko. Uzuri wake ni biashara huria kwa nchi wanachama kuondoa ushuru kabisa au kuwa na ushuru wa chini kwa bidhaa fulani. Lakini pia jambo hilo lina kero zake, vizuizi visovyo na-ushuru vinaweza kusababisha mahusiano mabaya, vita vya biashara, kutatanisha mmiminiko wa bidhaa na huduma.
Tanzania na Kenya zimepitia kitambo hicho sio tu miaka ya nyuma lakini hata miaka ya karibuni, enzi ya Rais John Magufuli. Upande wa biashara, Tanzania ilisitisha kuagiza bidhaa kutoka Kenya na, hadi hivi karibuni, zikilumbana na kupigana marufuku juu ya bidhaa mbalimbali mfano gesi, ngano na maziwa. Lakini sasa mahusiano ya biashara baina ya nchi hizo mbili yameongezeka, kwa manufaa ya Tanzania.
Maduhuli ya Kenya kutoka Tanzania, mkiwemo nafaka, mbao na mboga, yaligonga $3.4bn kwa tarakimu za Benki Kuu ya Kenya. Huo ukiwa ukuaji wa zaidi ya 70% kulingana na mwaka uliopita hadi Juni 2020. Kwa upande wake thamani ya maduhuli ya Tanzania kutoka Kenya ilikuwa $3.1bn, ongezeko la 21% na zaidi; ziada kwa Tanzania ya $273m.
Huku nyuma, pia Tanzania ilifarajika kwa malumbano ya kibiashara kati ya Kenya na Uganda; ilisafirisha bidhaa za thamani ya $400m, na Kenya iliuzia Uganda bidhaa za thamani ya $220m.

Chanzo cha picha, BBC/peter njoroge
Misukumo miwili inahusishwa na ufanisi huo wa Tanzania. Kwanza, data rasmi zinaonesha, Uganda na Tanzania si masoko makuu tena kwa bidhaa za Kenya bali ni Pakistan na Marekani. Na pili, mahusiano mabaya ya kibiashara baina ya Kenya na Uganda yameinua njia kwa Tanzania kuipiku Kenya katika soko la Uganda.
Ingawaje, chini ya uongozi wa Mama Samia mambo yamezidi kunoga. Kiini cha ziara zake katika nchi jirani hakikuwa na kusudi la kujuliana hali tu, bali biashara na kuipiga jeki sekta binafsi ya Tanzania - hofu iondoe, badala ya kuiogopa sekta binafasi ya Kenya, ishirikiane nayo.
Mnamo mwezi Mei, wakati akihutubia baraza la wadau wa kibiashara kutoka Kenya na Tanzania, mjini Nairobi, Mama Samia alidokeza wadhamini wao maana halisi kibiashara ni sawa na majina ya marais.

Chanzo cha picha, Ikulu Kenya
Alisema: bahati ilioje, "… Nchi zetu mbili, upande mmoja kuna Uhuru wa kufanya biashara, na upande mwingine kuna Suluhu ya kuondosha vikwazo vya biashara". Sasa ni juu yao wadau kushindwa.











