Rais Samia na Kenyatta wakubaliana kutatua vikwazo vya kibiashara baina ya Tanzania na Kenya

Rais Samia

Chanzo cha picha, IKULU, KENYA

Marais wa Tanzania na Kenya wametangaza hii leo kuwa nchi hizo mbili zimeingia makubaliano ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka jiji la Dar es Salaam mpaka Mombasa.

Katika hotuba zao kwa waandishi wa habari baada ya kufanya kikao cha faragha katika Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta pamoja na mgeni wake Rais Samia wa Tanzania wamesema kuwa bomba hilo litakuwa muhimu katika maendeleo ya nchi zote mbili.

Hata hivyo, marais hao hawakutoa taarifa za ndani zaidi juu ya mradi huo ikiwemo thamani yake na utaanza lini.

"Mradi huu utasaidia sana kuboresha upatikanaji wa kawi (nishati) na kushusha maradufu gharama ya gesi nchini pamoja na kuboresha uzalishaji wa viwandani," ameeleza rais Kenyatta.

x

Chanzo cha picha, Ikulu, Kenya

Kwa upande wake Rais Samia ameeleza kuwa baada kuingia mkataba huo kilichofuata sasa ni kusimamia utekelezaji wa makabaliano hayo kwa pande zote mbili.

Tanzania imegundua gesi katika mikoa yake ya pwani ya kusini ya Lindi na Mtwara na tayari gesi hiyo imefikishwa katika jiji la Dar es Salaam ambapo imeunganishwa na viwanda kadhaa lakini pia inatumika kuzalisha umeme unaoingia moja kwa moja katika gridi ya taifa.

Kutatua vikwazo vya kibiashara

Samia na Uhuru

Chanzo cha picha, IKULU, KENYA

Marais hao wawili pia wameeleza kuwa wamejadiliana kuhusu kurahisisha ufanyaji wa biashara baina ya nchi hizo mbili.

Rais Kenyatta amesema kuwa wamekubaliana kuwa Tume ya Pamoja ya mawaziri wa nchi hizo mbili iwe inakutana mara kwa mara ili kutatua changamoto za kibiashara na uhusiano zinatazotokea.

"Wanapofanya biashara wakati wawekezaji wanakuja ama kutoka Tanzania au Kenya, tuhakikishe kwamba tumeimarisha masuala ya kibiashara, kiuchumi na kitamaduni ambayo yatatusaidia kujenga Taifa letu la Kenya na Tanzania kwa manufaa yetu sote," amesema Rais Kenyatta.

Rais Samia amesema katika eneo hilo wamekubaliana kuondosha vikwazo visivyo vya kikodi katika biashara ya mpakani.

Marais hao pia wamezungumzia azma yao ya kuboresha biashara baina ya mataifa hayo jirani.

"...Kenya ni nchi ya tano kwa kuwekeza nchini Tanzania na ya kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki. Makampuni zaidi ya 400 ya Kenya yamewekeza dola bilioni 1.7," ameeleza Rais Samia na kusema kuwa makampuni ya Kitanzania yamewekeza Shilingi za Kenya Bilioni 19 na kuahidi kuwa kampuni kutoka Tanzania zitaongeza nguu zaidi kuwekeza Kenya.

Kuhusu wastani wa biashara wa baina ya nchi hizo ambao ni dola milioni 450 kwa mwaka, Rais Samia ameeleza kuwa wamekubaliana kuongeza wigo zaidi ya hapo.

Corona, miundombinu na EAC

Kuhusu mapambano dhidi ya maambukizi ya corona, Rais Samia amesema wamekubaliana rais Kenyatta kwa mawaziri wa afya wa nchi hizo wakutane kuangalia namna ya kurahisisha mfumo kupima na kutangamana katika mipaka ya nchi hizo mbili.

Mwaka jana, suala la corona lilitikisa uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara baina ya nchi hizo mbili ambapo mipaka ilifungwa na madereva wa malori kuzuiwa kuingia nchi nyengine.

Marais hao pia wamezungumzia kuboresha miundombinu ya barabara, mathalani ujenzi wa barabara ya kutoka Malindi katika pwani ya Kenya mpaka Bagamoyo katika pwani ya Tanzania.

"Pia tumesema tutaweka kipaumbele cha kuharakisha barabara kutoka Malindi, Lungaluunga mpaka tufike Bagamoyo. Pia tutaanzisha safari za Ziwa Victoria wakati wananchi na mizigo inayopita kutoka Jinja, Kisumu, Mwanza Bukoba, ili kurahisisha biashara za wananchi wetu," amesema rais Kenyatta.

Rais Samia amesema wamekubaliana kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikiwa pamoja na kuhamasisha nchi wanachama kulipa michango yao.