Ziara ya Rais Samia Suluhu: Kenya na Tanzania zimenufaika na nini katika ziara ya Rais Samia?

IKULU NAIROBI

Chanzo cha picha, IKULU NAIROBI

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Jumatano alikamilisha ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Kenya huku pakiwa na matumaini kati ya nchi hizi mbili kwamba ziara hiyo itafungua sura mpya katika undugu na ujirani .

Ziara ya Samia imeonekana kuwa imechangia sehemu kubwa kufungua milango ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili na kuondoa dhana na hofu zilizokuwepo kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulikuwa ukizidi kudorora . Kupitia kauli zake katika kila fursa aliyopata kuzungumza ,Rais Samia alisisitiza umuhimu wa mataifa hayo mawili kushirikiana bila kuwepo ushindani ,kauli au vitendo vya kukwazana .

Wakati akilihutubia Bunge la Kenya mara baada ya kumalizika kwa kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya Rais Samia alisema;

"Binafsi huwa nashangazwa sana na wale wanaodhani Kenya na Tanzania ni wapinzani, mbaya zaidi ni kule kuamini kwao kwamba hilo linawezekana tu mmoja wetu kumwangusha mwenzake, hawa ni watu wenye mioyo ya choyo, maono mafupi na akili mbovu."

"Ni bahati mbaya kuwa watu hawa wapo katika pande zote mbili, Kenya na Tanzania hutokea pia wachache wao wakawa ni watumishi wa Serikali zetu na hata wanasiasa wa pande mbili za nchi zetu. Bahati nzuri ni kuwa si wengi ndio maana uhusiano wa nchi zetu mbili unatimiza miaka 56 sasa," amesema Samia.

Ahadi ya ushirikiano

Samia ameahidi kwamba katika uongozi wake atahakikisha kuwa Kenya inabaki kuwa ndugu, jirani, mshirika wa mkakati ambao utafanya uhusiano kati ya nchi hizo mbili umefungwa katika mambo matatu.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni undugu wa damu ambao hauwezi kutenganishwa na mipaka ya kuchorwa kwenye ramani, suala la kihistoria na kijiografia.

"Ushirikiano wetu si wa hiari bali wa lazima kutokana na kanuni ya uasili wa undugu ambao Mwenyezi Mungu ameuumba, ushirika na ujirani yote yanatufanya tuwe pamoja na hatuna uwezo wa kulibadilisha kilichobaki ni tupendane au tuchukiane hatuwezi kukwepa kutokana na mambo haya matatu yaliyowekwa pamoja, tunategemeana kwa kila hali iwe kheri au shari."

KWAHERI

Chanzo cha picha, IKULU KENYA

Rais Samia alisema lengo lake ni kuhakikisha kwamba wawekezaji wa kigeni wanajenga imani ya kuwekeza nchini Tanzania na ili kurahisisha hilo serikali imeanzisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ya miundo mbinu kama barabara, reli , bandari na kawi ili kupunguza gharama ya kufanya biashara .

Rais Uhuru Kenyatta kwa upande wake amesema nchi zote mbili zitachukua hatua ya kuhakikisha kwamba makubaliano yote yaliyoafikiwa na mawaziri wa Biashara wa nchi zote yanatekelezwa . Kenyatta ameongeza kwamba mawaziri hao watakutana katika kipindi cha wiki nne zijazo ili kujadili kuondolewa kwa vikwazo visivyo vya kodi ambavyo vinaathiri biashara kati ya Kenya na Tanzania.

Akihutubia kongamano la wafanyabiashara mapema Jumatano kabla ya kwenda bungeni Rais aliwaambia wafanyabiashara hao kwamba ; "Mna bahati kwamba nchi zetu mbili upande mmoja kuna Uhuru wa kufanya biashara na upande mwingine kuna Suluhu ya kuondosha vikwazo vya biashara."

Kauli yake hiyo inaweza kutazamwa kama juhudi yake binafsi kuhakikisha kuwa vikwazo vilivyopo sasa vinavyoathiri ushirikiano kati ya Kenya na Tanzania vinashughulikiwa na kuondolewa ili pawepo biashara huru kati ya nchi hizo mbili .

Katika Bunge, Suluhu alifafanua kuwa ziara hiyo ya kiserikali ya siku mbili nchini Kenya ilikuwa yake ya kwanza tangu aapishwe kuwa Rais wa nchi hiyo jirani, akisema ziara ya mwezi uliopita nchini Uganda haikuwa ziara ya kiserikali bali ni ilikuwa ya kusaini mikataba ya kibiashara.

Samia anawarejeshea Watanzania yapi?

Vibali vya kazi

Kikubwa Zaidi ambacho kitawafurahisha wengi nchini Tanzania ni hatua ya Kenya kutangaza kwamba Watanzania sasa hawatalazimika kuwa vibali vya kuruhusiwa kufanya kazi nchini Kenya .

Hilo hata hivyo huenda likaleta manung'uniko kidogo kwa upande wa Wakenya endapo Tanzania nayo haitajibu kwa kuondoa hitaji la vibali vya kazi kwa raia wa Kenya wanaofanya kazi ama biashara nchini Tanzania .

Rais Samia katika hotuba yake na wafanyibiashara wa Kenya alisema taifa lake litathmini mambo yote yanayofaa kufanywa ili kuhakikisha kwamba utaratibu wa kuwekeza ama kufanya kazi nchini Tanzania unarahisishwa .

Rais Samia alisema Tanzania kwa sasa imetekeleza mageuzi yafuatayo ili kuhakikisha kwamba biashara inaboreshwa ;

  • Inatathmini upya kodi na vikwazo visivyo vya kodi
  • Kurahisisha utoaji wa vibali vya kufanya kazi kwa wawekezaji wa kigeni
  • Kutathmini kodi na ada zinazotozwa kwa biashara na watu
  • Usimamizi mzuri wa mfumo wa kodi
  • Kuimarisha vita dhidi ya ufisadi hasa katika sekta ya utumishi wa umma
  • Kufanikisha oparesheni za afisi ya pamoja ya kushughulikia biashara na uwekezaji
  • Kupeana ardhi ya kutumiwa kwa uwekezaji

Miradi ya pamoja

Walikubaliana, pamoja na mipango mingine, maendeleo ya mradi wa usafirishaji wa gesi asilia kutoka Tanzania hadi Kenya, vizuizi visivyo vya ushuru kati ya nchi hizi mbili kuondolewa ili kurahisha biashara na urahisi wa kusafiri katika kukuza utalii.

Viongozi hao pia walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa mtandao wa usafiri wa anga, reli, baharini na wa barabara, na pia kuongeza ushirikiano katika utamaduni, sanaa, ujumuishaji wa kijamii na urithi wa kitaifa.

mna Uhuru na Suluhu

Marais hao pia walizungumzia kuboresha miundombinu ya barabara, hususan ujenzi wa barabara ya kutoka Malindi katika pwani ya Kenya mpaka Bagamoyo katika pwani ya Tanzania.

"Pia tumesema tutaweka kipaumbele cha kuharakisha barabara kutoka Malindi, Lungaluunga mpaka tufike Bagamoyo. Pia tutaanzisha safari za Ziwa Victoria wakati wananchi na mizigo inayopita kutoka Jinja, Kisumu, Mwanza Bukoba, ili kurahisisha biashara za wananchi wetu," amesema rais Kenyatta.

"Wakuu wa nchi walisisitiza kujitolea kwao kuendelea kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika sekta mbalimbali kama biashara na uwekezaji, madini, nishati, mifugo, uchukuzi, ulinzi na usalama, pamoja na kupambana na ugaidi na uhalifu uliopangwa kimataifa, kwa faida ya pande mbili za nchi hizi na watu wao, "taarifa ya pamoja imesema .

Mahindi kuruhusiwa Kenya

Rais Uhuru Kenyatta katika hatua ya kumhakikishia mgeni wake nia yake ya kuzuia kabisa uwezekano wa biashara kati ya nchi hizo kuvurugika aliagiza maafisa wa serikali kuhakikisha kwamba mahindi yaliyozuiliwa mipakana kutoka Tanzania yanaruhusiwa kuingia Kenya .

''Hayo mahindi yaliyozuiliwa mpakani, Waziri mimi nakupatia wiki mbili…yote yafunguliwe na hayo maneno yaishe'' amesema.

Mahindi

Chanzo cha picha, Ntv

Rais Kenyatta aliwapa maafisa hao wiki mbili kushughulikia tatizo hilo bila kuchelewa. Bila shaka uamuzi huo wa Kenyatta utapokelewa vyema nchini Tanzania ambako wakulima na wafanyabiashara wametegema soko la Kenya kuuza nafaka yao.

Mapema mwezi Machi, Kenya ilipiga marufuku ununuzi wa mahindi kutoka mataifa jirani ya Tanzania na Uganda.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya uchunguzi kubaini kwamba mahindi kutoka mataifa hayo mawili sio salama kwa matumizi ya chakula cha binadamu.

Ushirikiano katika vita dhidi ya Corona

Rais Samia aliliambia Bunge la Kenya kuwa Tanzania itashirikiana na nchi jirani ikiwemo Kenya katika mapambano dhidi ya mlipuko wa corona.

Rais Samia amewaambia wabunge na maseneta wa Kenya kuwa tayari Tanzania imeshaanza kuchukua hatua ya tahadhari juu ya corona ikiwemo kusitisha safari za moja kwa moja na nchi zenye kasi ya maambukizo ya corona.

Akihutubia mkutano maalumu ulioandaliwa kwa ajili yake, amesisitiza kuwa Tanzania si kisiwa katika mapambano dhidi ya corona, na wakati ikisubiriwa mapendekezo kutoka kamati maalumu aliyoiunda, kitu ambacho ana hakika nacho ni lazima kushirikiano na majirani.

"Lazima tushirikiane na majirani katika vita dhidi ya corona, lazima tushirikiane na kenya katika hili," amesema Rais Samia.

Mwezi uliopita, Suluhu alitangaza kuunda kamati ya ufundi ya Covid-19 kumshauri juu ya hatua za kuchukua kama nchi kulinda Tanzania dhidi ya janga hilo.

Alibainisha kuwa utawala wake utatekeleza mapendekezo ya kikosi kazi katika kupambana na janga hilo.

Aliongeza pia kuwepo umuhimu wa ushirikiano katika upimaji na uzuiaji wa kusambaa kwa virusi hivyo katika maeneo ya mipakani bila kuathiri biashara na utangamano wa watu kutoka nchi hizo mbili .

Hatua hiyo huenda sasa ikarahisisha shughuli za wafanyibiashara wa mipakani na madereva wa malori ya bidhaa ambao waliathiriwa sana na baadhi ya masharti ya kupmbana na Corona kwa sababu ya kutokuwepo kwa mpango wa pamoja wa nchi hizo mbili kukabiliana na janga la Corona.

Utangamano wa kila mara

Rais Kenyatta alisema kuwa walikubaliana kuwa Tume ya pamoja ya mawaziri wa nchi hizo mbili iwe inakutana mara kwa mara ili kutatua changamoto za kibiashara na uhusiano zinatazotokea.

"Wanapofanya biashara wakati wawekezaji wanakuja kutoka Tanzania au Kenya, tuhakikishe kwamba tumeimarisha masuala ya kibiashara, kiuchumi na kitamaduni ambayo yatatusaidia kujenga mataifa yetu kwa manufaa yetu sote," amesema Rais Kenyatta.

Suluhu pia alimwalika Rais Kenyatta kuwa mgeni rasmi wakati wanasherehekea miaka 60 ya Uhuru mnamo Disemba.

Aidha aliwapongeza wabunge kwa kuanza kutumia lugha ya kiswahili;

'Tulifurahishwa sana na uamuzi wenu wa kuanza kutumia lugha ya Kiswahili bungeni. Hiyo ndiyo inayonifanya nisikilize vikao vya bunge la Kenya. Ninapenda Kiswahili chenu...ni burudani ya kutosha. Nilikuwa nikisikiliza wakati spika akijitahidi kutaja nambari za mwaka kwa Kiswahili.'

Kuiboresha Jumuiya ya Afrika Mashariki

Katika ziara yake rais Samia aliweka wazi kwamba dhamira yake ilikuwa kuboresha uhusiano sio tu wa taifa lake na Kenya bali pia kuboresha ushirikiano wao kupitia jumuiya ya Afrika mashariki .

"Kila mara panapotokea kutoelewana kati yetu tunadhoofisha uhusiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, bila kukusudia pia tunaathiri umoja wa Afrika Mashariki, hivyo hatuna budi kuendelea kuelewana."

Rais Samia amesema kuwa kuna kipindi Jumuiya hiyo ilijaribiwa kufuatia, maneno na vitendo ambavyo vilipima uimara wa dhamira za nchi wananchama wa jumuiya hiyo kuendelea na safari ya utangamano.

rais kenyatta na Samia

Chanzo cha picha, IKULU NAIROBI

"Niwahakikishie, mimi na wenzangu nchini Tanzania tutahakikisha kuwa uhusiano wetu unang'ara na kwa kufanya hivyo tung'arishe uhusiano wa Afrika Mashariki. Tanzania itaendelea kuwa jirani mwaminifu wa Kenya na mwanachama muadilifu wa Afrika Mashariki," amesisitiza Rais Samia.

Rais huyo alisisitiza umuhimu wa kila mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoa mchango wake ili kufanikisha shughuli za jumuiya hiyo .

Endapo kuna kipimo cha kufahamu iwapo ziara ya rais Samia nchini kenya itakuwa na manufaa kwa nchi zote mbili ,basi muda ndio utakaohitajika kukadiria utekelezwaji wa kauli ,ahadi na sera ambazo viongozi hao wawili waliahidiana wakati wa mkutano wao wa siku mbili .

Wengi wanangoja kwa hamu kuona kasi itakayotumiwa na kila serikali ili kufanikisha urahisishaji wa taratibu za kufanya biashara na ushirikiano wa watu na serikali za Tanzania na Kenya .