Mzozo wa Ukrainne: Mfahamu Mwanajeshi wa Urusi mwenye miaka 21 ambaye alikiri kuua raia Ukraine

Mwanajeshi wa Urusi mwenye umri wa miaka 21 amekiri kosa la kumuua raia asiye na silaha katika kesi ya kwanza ya uhalifu wa kivita nchini Ukraine tangu vita kuanza nchini humo.

Vadim Shishimarin alikiri kumpiga risasi mzee wa miaka 62 siku chache baada ya uvamizi huo kuanza.

Anakabiliwa na kifungo cha maisha jela.

Shishimarin alizaliwa Ust-Ilimsk katika Wilaya ya Irkutsk nchini Urusi.

Mfungwa huyo aliingizwa kwenye chumba kidogo cha mahakama ya Kyiv akiwa amefungwa pingu, huku pembeni yake akiwa na walinzi waliokuwa na silaha nzito.

Alionekana kuwa na wasiwasi na kuweka kichwa chake chini huku mita chache tu kutoka kwake, mjane wa mtu aliyeuawa alikuwa amekaa.

Mjane huyo alijifuta machozi wakati askari huyo akiingia ndani ya chumba cha mahakama, kisha akakaa huku akiwa ameshikana mikono wakati mwendesha mashitaka akitoa maelezo yake na kueleza jinsi mume wa Kateryna alivyopigwa risasi ya kichwa.

"Je, unakubali hatia yako?" hakimu aliuliza.

"Ndiyo," Shishimarin alijibu.

"Kabisa?" "Ndiyo," alijibu kimya kimya kutoka nyuma ya kizimba cha kioo cha kizimba chake cha kioo

Waendesha mashtaka wanasema Shishimarin alikuwa anaongoza kitengo cha mizinga wakati msafara wake uliposhambuliwa.

Yeye na askari wengine wanne waliiba gari na, walipokuwa wakisafiri karibu na Chupakhivka, walimkuta mzee huyo wa miaka 62 kwenye baiskeli, walisema.

Kulingana na waendesha mashtaka, Shishimarin aliamriwa kumuua raia huyo na alitumia bunduki ya kivita ya Kalashnikov kufanya hivyo.

Kremlin hapo awali ilisema haijui chochote kuhusu kesi hiyo.

Kesi ya Shishimarin iliahirishwa muda mfupi baada ya mjane wa raia huyo kusikia kwa mara ya kwanza askari huyo wa Urusi akikiri mauaji hayo.

Usikilizwaji wa Kesi hii ya hadhi ya juu utaanza tena Alhamisi katika chumba kikubwa zaidi.

"Kwa kesi hii ya kwanza, tunatuma ishara wazi kwamba wahalifu wote, watu wote ambao waliamuru au kusaidia katika kutenda uhalifu nchini Ukraine, hawataweza kukwepa kuwajibika," Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Ukraine Iryna Venediktova aliandika katika ukurasa wake wa twitter.

Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita

Venediktova hapo awali alisema ofisi yake ilikuwa ikitayarisha kesi za uhalifu wa kivita dhidi ya wanajeshi 41 wa Urusi.

Moscow imekanusha kuwa wanajeshi wake wamewashambulia raia.

Kesi ya Shishimarin inaangaliwa kwa karibu huku wachunguzi wakikusanya ushahidi wa uhalifu wa kivita unaoweza kuwasilishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huko The Hague.

ICC inatuma timu ya wachunguzi 42, wataalam wa mahakama na wafanyakazi wa usaidizi nchini humo.

Ukraine pia imeunda timu ya kuhifadhi ushahidi kwa majaribio yajayo.