Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Wanajeshi wa Urusi waonekana wakiwapiga risasi raia wasio na silaha
Wakati Leonid Pliats na bosi wake walipopigwa risasi mgongoni na wanajeshi wa Urusi, mauaji hayo yalinaswa kwenye kamera za CCTV.
Picha hiyo ya video ambayo BBC wameipata sasa inachunguzwa na waendesha mashtaka wa Ukraine kama uhalifu wa kivita unaoshukiwa.
Ilikuwa ni katika mapigano karibu na Kyiv na barabara kuu za kuelekea mji mkuu zilikuwa uwanja wa vita, ikiwa ni pamoja na eneo la duka la baiskeli ambapo Leonid alikuwa akifanya kazi kama mlinzi.
Lakini hii haikuwa vita vya kurushiana risasi kwani video inaonyesha wazi wanajeshi wa Urusi wenye silaha nyingi wakiwapiga risasi Waukrene wawili wasio na silaha na kisha kupora biashara.
Tumekusanya pamoja mlolongo kamili wa matukio, kulingana na kile kilichorekodiwa kwenye kamera nyingi za CCTV karibu na tovuti na ushuhuda wa watu ambao Leonid aliwapigia simu siku hiyo, pamoja na wapiganaji wa kujitolea wa Ukraini waliojaribu kumwokoa.
Warusi walifika wakiwa kwenye gari lililoibwa lililopakwa alama ya V inayotumiwa na vikosi vya Urusi na maneno ya rangi nyeusi yanayosomeka Tank Spetsnaz . Wamevaa sare za kijeshi za Kirusi na wanakaribia na bunduki zao.
Leonid anawaendea askari huku mikono yake ikiwa juu kuonesha hana silaha wala tishio.
Warusi hapo awali walizungumza naye na bosi wake kupitia uzio.
Hakuna sauti kwenye picha lakini wanaume wanaonekana watulivu, hata wanavuta sigara.
Kisha Waukraine wanageuka na askari wanaanza kuondoka.
Ghafla wanageuka nyuma, wanainama kisha wanawapiga risasi watu hao wawili migongoni mwao.
Mmoja anauawa moja kwa moja lakini kwa namna fulani Leonid anafaulu kujikongoja kwa miguu yake.
Anajifunga hata mshipi wake kwenye paja ili kupunguza damu, kisha akajikwaa hadi kwenye kibanda chake ambapo anaanza kuomba msaada.
Vasyl Podlevskyi alizungumza na rafiki yake mara mbili siku hiyo, akiwa amekaa akivuja damu nyingi.
Leonid alimwambia askari walidai kuwa hawaui raia, kisha wakampiga risasi.
''Nilisema hata angalau unaweza kujifunga mwenyewe? Na akaniambia, Vasya, nilitambaa hapa kwa shida. Kila kitu kinaumiza sana. Ninajisikia vibaya sana,'' Vasyl anakumbuka simu hiyo.
''Kwa hiyo nilimwambia aingie pale na kuanza kupiga simu kwa ulinzi wa eneo.''
Wanaume aliowaita walikuwa wakiuza viyoyozi kabla ya vita.
Sasa wapiganaji wa kujitolea, Sasha na Kostya wananionyesha video kwenye simu zao za rununu za mizinga ya Kirusi ikipita kwenye nafasi zao.
Kazi yao ilikuwa kutuma habari za wakati halisi juu ya harakati za Urusi kwenye nafasi za kijeshi za Ukraine barabarani.
Leonid Pliats alipojeruhiwa walitwikwa jukumu la kuvuka barabara kuu hatari ya E40 ili kujaribu kumuokoa.
Hata leo, barabara imejaa mizoga iliyochomwa ya mizinga ya Kirusi, ukumbusho wa mapigano makali.
Askari wa usalama alipokuwa amelala akivuja damu, askari wa Urusi walikuwa bado wapo.
Kwenye CCTV unawaona wakipiga risasi vyumbani, wakiiba baiskeli na hata skuta na kurandaranda kwenye ofisi ya mkurugenzi, wakinywa whisky, na kuruka kabati zake.
Wakiwa na idadi kubwa na wakiwa na silaha kidogo tu, Sasha na Kostya walilazimika kungoja ingawa waligundua kuwa Leonid alikuwa anafariki dunia.
''Tulizungumza naye kwenye simu, tukajaribu kumtuliza. Tukamwambia, ni sawa. Kila kitu kitakuwa sawa. Utapona,'' Sasha ananiambia walijitahidi kumfariji.
''Tulisema tuko njiani. Labda hiyo ilimsaidia. Labda. Lakini kwa bahati mbaya, wakati tunafanikiwa, alikuwa amekufa.''
Hata walipokuwa wakikusanya miili ya watu hao wawili, wapiganaji wa kujitolea walilazimika kujificha huku kifaru cha Urusi kikipita
Kuna ushahidi wa kutosha dhidi ya watu waliohusika na mauaji haya.
Tumeichunguza kwa undani video hiyo na mwanajeshi wa Urusi ambaye tunaamini alikuwa mmoja wa wauaji anaonekana wazi, uso wake haujafunikwa.
Ni muda mrefu kabla ya marafiki zake kutambua kuwa wanarekodiwa na kuvunja moja ya kamera za usalama.
Tulionyesha kanda hiyo kwa mkuu wa polisi wa mkoa wa Kyiv na akatuambia miili ya raia 37, wote wakiwa wameuawa kwa kupigwa risasi, ilipatikana kando ya barabara ya kuelekea mji mkuu wa Ukraine baada ya vikosi vya Urusi kurudishwa nyuma.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka inathibitisha kwamba sasa inachunguza mauaji ya Leonid na mwenzake kama uhalifu wa kivita unaowezekana: moja ya kesi zaidi ya 10,000 ambazo wamesajili.
''Baba yangu hakuwa mwanajeshi hata kidogo. Alikuwa mstaafu. Walimuua mzee wa miaka 65. Kwa nini?''
Binti ya Leonid, Yulia Androshchuk, anataka kujua.
Yeye yuko nje ya nchi na hajaweza hata kumzika baba yake kwa sababu ya vita.
''Sina hasira sana kama nilivyojawa na huzuni - na hofu. Warusi hawa wa ajabu sasa hawezi kudhibitiwa, kinachoniogopesha ni nini wanaweza kufanya baadaye,'' aliniambia.
Yulia anatumai wale waliohusika watafikishwa mahakamani siku moja, kwa namna fulani.
Kwa sasa, anataka watu wajue ni nini hasa kilimpata babake na unyama huo ukome.