Novak Djokovic: Sipingi chanjo lakini nitasalimisha mataji nikiambiwa lazima nipate chanjo

Novak Djokovic amesema afadhali kukosa mataji ya siku zijazo ya tenisi kuliko kulazimishwa kupata chanjo ya Covid.
Akizungumza na BBC katika mahojiano ya kipekee, alisema hapaswi kuhusishwa na vuguvugu la kupambana na chanjo yaani anti vaxxers , lakini aliunga mkono haki ya mtu binafsi ya kuchagua.
Djokovic aliulizwa kama angejinyima kushiriki katika mashindano kama vile Wimbledon na French Open kutokana na msimamo wake kuhusu chanjo hiyo.
"Ndiyo, hiyo ndiyo gharama ambayo niko tayari kulipa," alisema.
Mshindi huyo mara 20 wa Grand Slam alifukuzwa kutoka Australia mwezi uliopita baada ya serikali kufuta visa yake mfululizo kuhusu hali yake ya chanjo.
Djokovic, ambaye ni mchezaji nambari moja wa tenisi duniani kwa wanaume, alisema amepata msamaha wa kiafya ili aingie nchini kucheza michuano ya wazi ya Australia kwa vile alikuwa amepona Covid-19 hivi majuzi.

Chanzo cha picha, PA Media
Hata hivyo, waziri wa uhamiaji wa nchi hiyo, Alex Hawke, binafsi alifuta visa ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 34, kwa misingi kwamba uwepo wake unaweza kuchochea "machafuko ya kiraia" na kuhimiza hisia za kupinga chanjo.
"Sikuwa kamwe nikipinga chanjo," aliiambia BBC, akithibitisha kwamba alikuwa na chanjo alipokuwa mtoto, "lakini siku zote nimeunga mkono uhuru wa kuchagua unachoweka mwilini mwako."
Katika mahojiano mapana, ya kwanza tangu azuiliwe huko Melbourne mnamo Januari, Djokovic alizungumzia uvumi kuhusu wakati wa alipopatikana na Covid mnamo Desemba na akajadili mtazamo wake mwenyewe juu ya chanjo.

Chanzo cha picha, EPA
Djokovic alisema anatumai mahitaji ya chanjo katika mashindano fulani yatabadilika, akiongeza kuwa alikuwa na matumaini kwamba "anaweza kucheza kwa miaka mingi zaidi".
Lakini pia alithibitisha kuwa alikuwa tayari kuachana na nafasi hiyo ya kuwa mchezaji bora wa tenisi wa kiume kitakwimu kwa sababu ya msimamo wake. Mpinzani wa Djokovic, Rafael Nadal, ameshinda mataji 21 ya Grand Slam pekee - mengi zaidi ya mshindani yeyote wa kiume.
Alipoulizwa kwa nini, alijibu: "Kwa sababu kanuni za kufanya maamuzi juu ya mwili wangu ni muhimu zaidi kuliko cheo chochote au kitu kingine chochote. Ninajaribu kuwa sawa na mwili wangu kadri niwezavyo."












