Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Majasusi wa Iran wanaoungwa mkono na Saudi Arabia wakutwa na hatia Denmark
Mahakama ya Denmark imewapata na hatia wanachama watatu wa kundi la upinzani la Iran ya kufanya ujasusi kwa Saudi Arabia.
Wanaume hao watatu walizuiliwa na polisi mnamo Februari 2020 na ni wanachama wa Vuguvugu la Movement for the Liberation of Ahvaz (ASMLA).
Pia walipatikana na hatia ya "kuchochea ugaidi" kwa kuunga mkono mrengo wake wa kijeshi nchini Iran.
Wanakabiliwa na hukumu mwezi ujao, na uwezekano wa vifungo vya hadi miaka 12 na kufukuzwa nchini.
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo kwa muda mrefu katika Mahakama ya Wilaya ya Roskilde ya Denmark, baraza la majaji lilisema kwamba kati ya 2012 na 2020 watu hao watatu walikuwa wamefikisha taarifa kuhusu watu na mashirika mbalimbali ya Denmark, pamoja na masuala ya kijeshi ya Iran, kwa maafisa wa kijasusi wa Saudia ili wapate malipo.
Wanaume hao, wenye umri wa kati ya miaka 41 na 50, walipokea kroner milioni 15 (£1.27m) kutoka kwa maafisa wa kijasusi wa Saudia. Mmoja ni raia wa Denmark.
Waendesha mashtaka walisema kwamba pesa hizo zilisaidia kufadhili shughuli za tawi la ASMLA nchini Iran, linaloitwa Brigedia ya Mohiuddin Nasser Martyrs.
ASMLA ni vuguvugu linalotaka kujitenga ambalo linatafuta jimbo tofauti kwa Waarabu wa kabila katika mkoa wa Khuzestan unaozalisha mafuta kusini-magharibi mwa Iran.
Kundi hilo linatazamwa kama kundi la kigaidi na utawala wa Iran na tawi lake lenye silaha limefanya mashambulizi kadhaa ya kikatili, likiwemo shambulio la gwaride la kijeshi katika mji wa kusini-magharibi wa Ahvaz mwaka 2018 ambapo watu 24 waliuawa.
Mahakama hiyo pia iliwapata wanaume hao na hatia ya kuunga mkono kundi la wanamgambo la Jaish al-Adl, linaloendesha harakati zake nchini Iran na limeorodheshwa kama kundi la kigaidi nchini Marekani.
Kesi hiyo ni mfano wa hivi punde zaidi wa vita vya kijasusi vinavyokua kati ya maafisa wa ujasusi wanaoungwa mkono na Saudi Arabia na Iran nchini Denmark.
Mnamo mwaka wa 2018, mmoja wa wanaume hao watatu alikuwa mlengwa wa jaribio la mauaji ambalo linaaminika kufadhiliwa na Tehran, ambalo lilishuhudia raia wa Norway-Irani kufungwa kwa miaka saba kwa jukumu lake katika njama hiyo.
Iran ilitupilia mbali madai hayo, lakini Denmark ilimwita balozi wak.
Mkuu wa wakala wa kijasusi wa PET wa Denmark, Finn Borch Andersen, alionya baadaye kwamba haitakubali mataifa ya kigeni kuleta "migogoro yao ya pande zote" katika ardhi ya Denmark.
Mapambano ya ASMLA kwa ajili ya makabila ya Kiarabu
Kundi hilo linalojulikana pia kwa jina la Kiarabu, al-Nidhal, limekuwa likitafuta uhuru tangu mwaka 1999 kwa ajili ya makabila madogo ya Waarabu waliotengwa nchini Iran.
Taasisi tawala ya Iran imeitaja ASMLA kuwa ni shirika la kigaidi, ikilihusisha na mashambulizi mengi mabaya, hasa shambulio la kuvizia mwaka 2018 katika gwaride la Siku ya Jeshi katika mji wa kusini-magharibi wa Ahvaz.
ASMLA imekanusha kuhusika na shambulio hilo lililosababisha vifo vya zaidi ya watu kumi na mbili, miongoni mwao wakiwa wanawake na watoto.
Mmoja wa viongozi wakuu wa kundi hilo, Habib Chaab, kwa sasa anakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na ugaidi mjini Tehran. Mpinzani huyo mwenye makazi yake Uswidi alishawishiwa na maafisa wa kijasusi wa Iran katika ziara yake nchini Uturuki mwaka 2020 kabla ya kuhamishiwa Iran katika kile ambacho mamlaka ya Uturuki ilieleza kuwa ni utekaji nyara.
Wakati wa vikao vitatu vya Chaab hadi sasa, waendesha mashtaka wamemtaja adui mkuu wa Iran Israel na mpinzani wa kikanda Saudi Arabia kama wafuasi wa ASMLA, huku pia wakishutumu Denmark na Ubelgiji kwa kuwahifadhi wanachama wake.
Waarabu walio wachache nchini Iran wanaishi katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Khuzestan. Licha ya kukaa kwenye usambazaji wa nishati nyingi, mkoa umebakia kuwa duni, ukikabiliana na malalamiko mengi ya kiuchumi na kisiasa.
Na shida ya maji katika eneo hilo imezidisha hali ambayo tayari ni mbaya. Maandamano ya wiki moja ya kupinga matumizi mabaya ya maji majira ya joto yaliyopita yalichochea moto kutoka kwa vikosi vya usalama na kushuhudia takriban watu watatu wakiuawa.