Fahamu ni nani kati ya kiongozi mkuu na rais aliye na mamlaka katika uongozi wa Iran

Iran ni nchi ambayo mfumo wake wa kisiasa ni mgumu kuelewa. Kwa upande mmoja, kuna mtandao wa taasisi zisizochaguliwa zinazodhibitiwa na Kiongozi Mkuu, na kwa upande mwingine, kuna bunge na rais aliyechaguliwa na wapiga kura wa Iran. Mifumo hii yote miwili inafanya kazi pamoja.

Lakini mfumo huu mgumu wa kisiasa unafanya kazi vipi na ni nani anayeshikilia funguo za mamlaka ndani yake?

Kiongozi Mkuu

Nafasi ya kiongozi mkuu inachukuliwa kuwa yenye nguvu zaidi katika siasa za Iran. Tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, ni watu wawili tu wamefikia wadhifa wa Kiongozi Mkuu. Wa kwanza kati ya hawa alikuwa Ayatollah Ruhollah Khomeini, mwanzilishi wa Jamhuri ya Iran, na wa pili alikuwa mrithi wake, Ayatollah Ali Khamenei wa sasa. Khomeini alipandishwa cheo hicho hadi cheo cha juu kabisa katika mfumo wa kisiasa wa Iran baada ya kupinduliw akwa utawala wa Shah Mohammad Reza Pahlavi.

Kiongozi mkuu ndiye kamanda mkuu wa majeshi ya Iran. Ana udhibiti wa vikosi vya usalama, anateua wakuu wa mahakama, nusu ya wajumbe wa Baraza la Walinzi wenye ushawishi, viongozi wa sala ya Ijumaa, wakuu wa televisheni za serikali na mitandao ya redio. Mashirika ya misaada ya mabilioni ya dola ya kiongozi mkuu yanadhibiti sehemu kubwa ya uchumi wa Iran.

Ayatollah Ali Khamenei alishika wadhifa wa kiongozi mkuu mnamo 1989 baada ya kifo cha aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa zamani Khomeini. Tangu kuwa kiongozi mkuu, Khamenei amethibiti vilivyo madaraka. Hajaruhusu sauti za kupinga mamlaka kuibuka.

Rais wa Iran

Uchaguzi wa urais wa Iran hufanyika kila baada ya miaka minne. Mtu ambaye atashinda uchaguzi anaweza kuwa Rais kwa muda usiozidi mihula miwili kwa wakati mmoja. Kwa mujibu wa Katiba ya Iran, Rais ndiye mtu wa pili mwenye nguvu zaidi nchini Iran. Yeye ndiye mkuu wa watendaji ambaye jukumu lake ni kuhakikisha katiba imefuatwa.

Kuanzia sera za ndani hadi za nje, Rais ana majukumu makubwa. Lakini uamuzi wa mwisho kuhusu masuala ya kitaifa ni wa Kiongozi Mkuu.

Wale wote wanaowania kiti cha urais wanapaswa kupata idhini kutoka kwa Baraza la Uongozi linaloshirikisha kundi la wanatheolojia 12 na wataalam wa sheria

Bunge

Bunge la Iran lenye wabunge 290, huchaguliwa kupitia uchaguzi mkuu kila baada ya miaka minne. Bunge lina uwezo wa kutunga sheria. Pamoja na hili, kuna uwezo wa kufuta bajeti ya mwaka.

Bunge linaweza kumwita Rais na mawaziri wa serikali na linaweza kuanzisha kesi ya kuwashtaki. Hata hivyo, sheria zote zilizopitishwa na Bunge lazima ziidhinishwe na Baraza la Walinzi.

Baraza la Uongozi

Baraza la Uongozi ndilo lenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Iran, ambalo kazi yake ni kuidhinisha au kuzuia sheria zote zinazopitishwa na bunge. Baraza hili linaweza kupiga marufuku wagombeaji kujaribu bahati yao katika uchaguzi wa bunge au uchaguzi kwa kamati ya wataalamu.

Kuna wanatheolojia sita katika baraza hili, ambao huteuliwa na Kiongozi Mkuu. Pamoja na hayo, wapo majaji sita wanaopendekezwa na mahakama na majina yao kupitishwa na Bunge. Wanachama huchaguliwa kwa awamu ya muda wa miaka sita, na wanachama wakibadilika kila baada ya miaka mitatu.

Baraza hilo lina wafuasi wengi wa kimsingi, akiwemo mwenyekiti Ayatollah Ahmed Jannati.

Kamati ya wataalamu

Ni shirika lenye nguvu lenye wanachama 88, ambalo linajumuisha wanazuoni wa Kiislamu na Maulamaa. Kazi ya taasisi hii inatokana na uteuzi wa Kiongozi Mkuu wa kufuatilia utendaji wake. Ikiwa taasisi inaona kuwa Kiongozi Mkuu hana uwezo wa kufanya kazi yake, basi taasisi hii pia ina uwezo wa kumuondoa Kiongozi Mkuu.

Hata hivyo, haijawahi kutokea kwamba maamuzi ya Kiongozi Mkuu yamepingwa. Lakini taasisi hii imekuwa muhimu sana kutokana na wasiwasi wa mara kwa mara kuhusu afya ya Ayatollah Ali Khamenei mwenye umri wa miaka 82.

Ikiwa kiongozi mkuu atakufa, shirika hili hufanya uchaguzi wa siri, ambapo mtu aliye na wingi wa wazi anatangazwa mrithi. Uchaguzi wa wanachama wa shirika hufanyika kila baada ya miaka minane.

Baraza la Ufanisi

Baraza hili linatoa ushauri kwa Kiongozi Mkuu. Katika kesi ya mzozo kati ya Baraza la Uongozi na Bunge katika maswala ya kisheria, chombo hiki kina haki ya kuamua. Kiongozi Mkuu anawateua wajumbe wote 45 wa baraza hili ambao ni watu mashuhuri wa kidini, kijamii na kisiasa.

Rais wa sasa wa shirika hilo ni Ayatollah Sadeq Amoli Larijani, mtu mwenye siasa kali na mkuu wa zamani wa mahakama.

Mkuu wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Iran anateuliwa na Kiongozi Mkuu. Jaji Mkuu anawajibika kwa Kiongozi Mkuu pekee.

Ni mkuu wa mahakama ya nchi. Mahakama chini yake hufafanua uzingatiaji wa sheria za Kiislamu na sera za kisheria.

Mahakama, pamoja na Idara ya Usalama na Ujasusi, zimechukua hatua dhidi ya wale wanaopinga. Wanaharakati wa haki za binadamu mara nyingi hushutumu mahakama kwa kuendesha isivyo kisheria dhidi ya watu waliokamatwa kwa misingi ya masuala ya usalama wa taifa.

Mpiga Kura

Kati ya watu milioni 83 wa Iran, wapiga kura wapatao milioni 58, yaani watu waliotimiza umri wa miaka 18 wanaweza kupiga kura.

Vijana ndio wengi katika wapiga kura. Zaidi ya nusu ya idadi ya watu ni chini ya miaka 30. Tangu Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, idadi ya wapiga kura imekuwa zaidi ya 50%.

Hata hivyo, katika uchaguzi wa bunge wa 2021, kutokana na hali mbaya ya uchumi na kutoridhika, watu wengi walionekana kususia upigaji kura.

Vikosi vya Jeshi

Vikosi vya kijeshi vya Iran vinajumuisha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Jeshi Mkuu.

IRGC iliundwa baada ya mapinduzi kwa lengo la kulinda mfumo wa Kiislamu na kuweka nguvu sambamba na jeshi la pamoja. Hata hivyo, sasa imekuwa nguvu kubwa ya silaha, kisiasa na kiuchumi na uhusiano wa karibu na Kiongozi Mkuu.

Walinzi wa Mapinduzi wana jeshi lake la ardhini, jeshi la wanamaji na jeshi la anga. Jukumu la kusimamia silaha muhimu za Iran pia liko kwa taasisi hii.

Shirika hilo pia linadhibiti Kikosi ambacho kimekuwa na jukumu la kuzima upinzani wa ndani.

Maafisa wote wakuu wa IRGC na makamanda wa kijeshi wanateuliwa na Kiongozi Mkuu ambaye pia ndiye Amiri Jeshi Mkuu. Makamanda na maafisa hawa wanawajibika kwa Kiongozi Mkuu pekee.

Baraza la mawaziri

Wajumbe wa Baraza la Mawaziri huchaguliwa na Rais. Majina yao yanaidhinishwa na bunge, ambalo linaweza pia kuwaadhibu mawaziri. Baraza hili la mawaziri linaongozwa na Rais au Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye anahusika na mambo yanayohusiana na baraza la mawaziri.