Zifahamu operesheni kadhaa dhidi viongozi wakuu wa Islamic State na al-Qaeda

Operesheni za kijeshi zilizoongozwa na Marekani dhidi ya viongozi mbalimbali wa makundi ya wanamgambo zilionekana kushika kasi katika maeneo kadhaa ya ulimwengu na kusababishwa kuuawa kwa viongozi wa wanajihadi ambao wamekuwa wakiendesha shughuli zao kwenye maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Hawa ni baadhi ya viongozi waliouawa wakati wa operesheni dhidi ya vongozi wa Islamic State na al-Qaeda

Abu Ibrahim al-Hashimi al-Qurayshi

Kiongozi wa kundi la Islamic State (IS) aliuawa katika msako wa usiku wa kuamkia jana wa kikosi maalum cha Marekani kaskazini-magharibi mwa Syria, maafisa wakuu wa Marekani wamesema.

"Shukrani kwa ustadi na ushujaa wa vikosi vyetu vya jeshi, tumetoka kwenye uwanja wa vita Abu Ibrahim al-Hashimi al-Qurayshi," Rais Joe Biden alisema.

Maqurayshi walilipua bomu ambalo lilimuua yeye na watu wa familia yake mwenyewe, maafisa wa utawala waliviambia vyombo vya habari vya Marekani.

Walisema walipata miili ya watu 13 baada ya uvamizi huo.

Al-Qurayshi anaaminika kujiunga na ISIS mwaka 2003-2004, mtu anayeelezwa kuwa na utaalamu mkubwa wa kijeshi na kijasusi na alikuwa mhusika mkuu katika operesheni za ISIS.

Idara ya kijasusi ya Iraq inaamini kuwa ISIS imemficha al-Qardaash dhidi ya vita ili kumzuia asidhuriwe kwani ISIS inamhesabu mtu huyo kama mrithi wa al-Baghdadi.

Qardash alipata mafunzo ya mahakama katika Chuo cha al-Imam al-Adami huko Mosul.

Al-Qureyshi alikuwa na walinzi waliokuwa na silaha nzito huku akipigana kwa saa kadhaa na wanajeshi wa Marekani waliouawa katika operesheni hiyo.

Abu Bakr al-Baghdadi

Abu Bakr al-Baghdadi, kiongozi wa kundi la Kijihad la Islamic State (IS) na mtu ambaye alikuwa akisakwa sana duniani , alijiua kufuatia uvamizi wa Marekani uliotekelezwa na kikosi maalum cha wanajeshi kaskazini magharibi mwa Syria, kulingana na rais Trump.

Kiongozi huyo aliyejiita 'Kalifa Ibrahim' alikuwa amewekewa dola milioni 25 kwa mtu yeyote ambaye angefichua maficho yake na alikuwa akisakwa na Marekani na washirika wake tangu kuanzishwa kwa kundi la IS miaka mitano iliopita.

IS lilidhibiti kilomita 88,000 mraba wa eneo kutoa magharibi mwa Syria hadi mashiriki mwa Iraq, na likaweka utawala wake wa ukatili kwa zaidi ya watu milioni 8 , huku likijipatia mabilioni ya madola kutoka kwa mapato ya mafuta , wizi na utekaji nyara.

'Aliyeamini'

Jina lake Baghdadi - ni Ibrahim Awwad Ibrahim al-Badri - na alizaliwa 1971 katika mji wa kati wa Iraq kwa jina Samarra. Familia yake ni ya Waarabu wa madhehebu ya Sunni inayodaiwa kutoka katika kabila la mtume Muhammad la Quraysh - kitu kinachoaminika kuwa sifa ya kuwa Kalifa.

Akiwa kijana, alipewa jina la utani 'Muumin' na nduguze kwa kuwa alihudumia muda wake mwingi akiwa ndani ya msikiti akisoma Quran na kwamba mara kwa mara aliwashutumu walioshindwa kufuata sheria ya Kiislamu au sharia.

Kufuatia mashambulizi ya Marekani yaliompindua rais Saddam Hussein 2003, Baghdadi aliripotiwa kuanzisha kundi la wapiganaji wa Kiislamu kwa jina Jamaat Jaysh Al al- Sunnah wa-al-Jamaah ambalo lilishambulia vikosi vya Marekani na washirika wao.

Ndani ya kundi hilo, alikuwa kiongozi wa kamati ya sharia. Mapema 2004, Baghdadi alikamatwa na wanajeshi wa Marekani katika mji wa Faluja, magharibi mwa Baghdad, na kupelekwa katika kambi moja ya Bucca kusini.

Hamza bin Laden

Hamza Bin Laden, mwana wa mwanzilishi wa kundi la al-Qaeda Osama Bin Laden, aliuawa katika shambulio la angani , kulingana na vyombo vya habari vya Marekani vikinukuu maafisa wa ujasusi.

Mwezi Februari mwaka 2019, Serikali ya Marekani iliahidi kutoa dola milioni 1 kwa ajili ya yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kutambua ni wapi alipo.

Hamza Bin Laden, anayedhaniwa kuwa na umri wa miaka 30, alikuwa ametoa ujumbe mbalimbali wa sauti na video akitoa wito wa kufanya mashambulio dhidi ya Marekani na nchi nyingine.

Ripoti zilitolewa kwanza na mashirika ya habari ya NBC na New York Times.

Hamza Bin Laden aliwatolea wito wapiganaji wa jihadi kulipiza kisasi mauaji ya baba yake aliyeuliwa na kikosi maalum cha Marekani nchini Pakistan mnamo mwezi Mei 2011.

Kadhalika alikuwa amewatolea wito watu wa rasi ya Arabia kulipiza kisasi. Saudi Arabia ilimyang'anya uraia mwezi Machi.

Aliaminika kuwa katika kifungo cha nyumbani nchini Iran lakini ripoti nyingine zilisema kuwa huenda alikuwa akiishi katika mataifa ya Afghanistan, Pakistan na Syria.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema kuwa nyaraka zilizokamatwa katika uvamizi wa mwaka 2011 katika nyumba ya baba yake ya Abbottabad, Pakistan, zinaonyesha kuwa Hamza Bin Laden alikuwa anaandaliwa kuchukua utawala wa al-Qaeda.

Vikosi vya Marekani pia viliripotiwa kubaini video hii ya harusi yake akimuoa binti wa afisa mwingine wa ngazi ya juu wa al-Qaeda ambayo ilidhaniwa kufanyika nchini Iran:

Baba mkwe wake alikuwa ni Abdullah Ahmed Abdullah au Abu Muhammad al-Masri, ambaye anatafutwa kwa madai ya kuhusika katika mashambulio ya ugaidi ya mwaka 1998 dhidi ya balozi za Tanzania na Kenya.

Al-Qaeda lilikuwa ni kundi lililotekeleza mashambulio mabaya ya ugaidi ya Septemba 11, 2001 dhidi ya Marekani, lakini hadhi yake kwa sasa imeshuka katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita baada ya kuibuka kwa umaarufu wa kundi la Islamic State.

Osama bin Laden

Mwanzilishi na kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Qaeda, Osama Bin Laden, aliuawa na majeshi ya Marekani nchini Pakistan, rais wa wakati huo Barrack Obama alisema

Kiongozi huyo wa al Qaeda aliuawa baada ya makabiliano na wanajeshi wa Marekani nje ya mji wa Islamabad kwa mujibu wa taarifa za kijasusi.

Bw Obama alisema baada ya ufyatulianaji wa risasi, majeshi ya Marekani yaliuchukua mwili wake.

Bin Laden alishutumiwa kwa kuhusika katika baadhi ya vitendo vya ugaidi ikiwemo mashambulizi mjini New York na Washington, mnamo Septemba 11, 2001.

Kifo chake kilikuwa pigo kubwa kwa kundi la al Qaeda lakini kulikuwa na hofu ya kutokea mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Taarifa za mahali alikojificha zilianza kupatikana Agosti mwaka 2010

Kufuatia uchunguzi wa ujasusi waligundua amejificha mjini Pakistan.

Bw. Obama alitoa amri kwa shughuli ya ''kumsaka bin Laden'' kufanyika. Bw Obama alisema operesheni hiyo iliendeshwa na kundi ndogo la wanajeshi wa Marekani katika eneo la Abbottabad, kaskazini mwa Islamabad.

Baada ya ufyatulianaji wa risasi, bin Laden aliuwawa na mwili wale kuchukuliwa na majeshi ya Marekani.

Alifahamika nchini Afghanistan katika miaka ya mwisho ya 1980, kama mwarabu aliyejitolea kujiunga na kikosi cha Afghanstan kilichoungwa mkono na mujahideen kilichopigana kuvifukuza vikosi vilivyoteka eneo la Usovieti

Osama Bin Laden alianzisha shirika la kusaidia wahudumu wa kujitolea ambalo lilikuja kutambuliwa kama al-Qaeda, au "ngome"

Aliondoka Afghanistan mnamo mwaka 1989, na kurejea tena mwaka 1996 kuongoza makambi ya mafunzo ya kijeshi ya maelfu ya waislamu kutoka mataifa ya kigeni.

Al-Qaeda ilitangaza "vita vitakatifu " dhidi ya Wamarekani,wayahudi na washirika wao.

Abu Musab al-Zarqawi

Mnamo Juni 7, 2006, vikosi vya Marekani vilimuua Abu Musab al-Zarqawi, kiongozi wa al-Qaeda nchini Iraqi, katika shambulio la anga kwenye makazi kaskazini mwa Baghdad. Tovuti zenye uhusiano na Al-Qaeda zilithibitisha haraka kifo hicho.

Watu sita waliuawa katika shambulio hilo, akiwemo mwanamke na mtoto, maafisa wa kijeshi walisema.

Shambulio hilo lilifanyika miaka mitatu baada ya Vita vya Iraq, ambavyo utawala wa George W. Bush ulikuwa umeanza kutokana na madai ya uwongo kwamba Iraq ilikuwa na silaha za maangamizi makubwa na kwamba kiongozi wa Iraq Saddam Hussein alikuwa akiishi na al-Qaeda.

Zarqawi, maafisa wa utawala wa Bush walishutumiwa kimakosa, kuwa aliwahi kuwa kiungo kati ya al-Qaeda na serikali ya Hussein.

"Kifo cha Zarqawi ni pigo kubwa kwa al-Qaeda," Bush alisema katika hotuba yake katika Ikulu ya White House siku iliyofuata. "Ni ushindi katika vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi, na ni fursa kwa serikali mpya ya Iraq kubadili wimbi la mapambano haya."

Islamic State ilikua kutoka kwa washirika wa al-Qaeda wa Iraqi miaka kadhaa baadaye na kujitambulisha kama mbadala wa ushirika mbaya zaidi.