Mzozo wa Ukraine: 'Msaada wa 'zana hatari' kutoka Marekani wawasili Kyiv

Chanzo cha picha, US Embassy Kyiv
Tani 90 shehena za "silaha hatari" za Marekani zimewasili nchini Ukraine, huku mvutano juu ya kuongezeka kwa wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka wa nchi hiyo.
Ilikuwa shehena ya kwanza ya hivi karibuni kuidhinishwa kama msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine, na ilijumuisha risasi kwa "walinzi walio mstari wa mbele".
Uwasilishaji huo ulifuatia ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken mjini Kyiv wiki hii, ambapo alionya kuhusu hatua kali ikiwa Urusi itaivamia.
Moscow imekanusha mpango wowote wa kushambulia au kuivamia Ukraine.
Rais wa Marekani Joe Biden aliidhinisha huo msaada wa kiusalama wa thamani ya dola milioni 200 (£147.5m) mwezi Disemba.
Ubalozi wa Marekani mjini Kyiv ulisema msaada huo ishara ya "kujitolea kwake kwa Ukraine kujilinda".
"Marekani itaendelea kutoa usaidizi kama huo kusaidia Wanajeshi wa Ukraine katika juhudi zao zinazoendelea za kutetea mamlaka ya Ukraine na uadilifu wa eneo lao dhidi ya uvamizi wa Urusi," iliandika kwenye Facebook.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksiy Reznikov aliishukuru Marekani kwa msaada huo.

Mvutano juu Ukraine

Urusi imewahi kuvamia eneo la Ukraine - rasi ya Crimea mnamo 2014. Tangu wakati huo, takriban watu 14,000 wameuawa na takriban milioni mbili walikimbia makazi yao kwa sababu ya mapigano kati ya jeshi la Ukraine na waasi wanaoungwa mkono na Urusi. Makubaliano dhaifu ya amani yalifikiwa mnamo 2015.
Sasa, mkuu wa muungano wa kijeshi wa Nato ameonya kuna hatari ya kusuka upya kwa mzozo barani Ulaya baada ya takriban wanajeshi 100,000 wa Urusi kukusanyika katika mpakani.
Moscow imekanusha kuwa inapanga uvamizi, lakini Rais Vladmir Putin ametoa matakwa kwa mataifa ya Magharibi ambayo anasema yanahusu usalama wa Urusi, ikiwemo Ukraine kuzuiwa kujiunga na Nato.
Pia anataka Nato kukomesha na mazoezi ya kijeshi na kuachana na mpango wa kupeleka silaha mashariki mwa Ulaya, akisema hatua hiyo ni tishio la moja kwa moja kwa usalama wa Urusi.













