Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inasema haitaivamia Ukraine wakati wa mazungumzo na Marekani?

Mwanajeshi wa Ukraine akiwa mpakani na Urusi. Moscow imewapeleka maelfu ya wanajeshi wake katika eneo hilo la mpakani.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mwanajeshi wa Ukraine akiwa mpakani na Urusi. Moscow imewapeleka maelfu ya wanajeshi wake katika eneo hilo la mpakani.

Urusi imeiambia Marekani kwamba haina nia ya kuivamia Ukraine, baada ya maafisa wa nchi zote mbili kukutana kwa mazungumzo ya juu mjini Geneva.

Baada ya mkutano uliodumu kwa saa saba siku ya Jumatatu, pande zote mbili zilikubaliana kuendeleza na juhudi za kupunguza mivutano.

Lakini hakukuwa na dalili ya mafanikio makubwa kufuatia mazungumzo hayo.

Takriban wanajeshi 100,000 wa Urusi wanaaminika kuwa karibu na mpaka na Ukraine, jambo linalozusha hofu ya kuvamiwa na maonyo kutoka nchi Magharibi.

Marekani imesema kutakuwa na vikwazo iwapo Urusi itaivamia Ukraine.

Wakati huo huo, Urusi imeionya Marekani kutodharau hatari zinazoweza kutokana na mivutano kati yake na nchi za Magharibi.

"Tuliwaeleza wenzetu kwamba hatuna mpango wa kuivamia Ukraine," Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Ryabkov aliwaambia waandishi wa habari kufuatia mkutano huo.

Alisema Urusi iliwaambia wenzao wa Wamarekani "kwamba hatua zote za mafunzo ya wanajeshi zinafanywa ndani ya Urusi na kwamba hakuna sababu ya kuogopa kuibuka mzozo katika suala hili".

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Wendy Sherman alielezea mazungumzo hayo kama "mijadala ya wazi wa kuhimiza uelewa mzuri wa masuala ya usalama ya kila upande"

Bado hakuna makubaliano muhimu

Hii ilikuwa ni fursaya kwanza kwa wanadiplomasia wa Urusi na Marekani kujadiliana ana kwa ana kuhusu Ukraine, na madai ya Urusi kwa Nato kujiondoa kutoka Ulaya mashariki.

Na ingawa makubaliano kidogo yanaonekana kufikiwa, pande zote mbili zilielezea wasiwasi wao huku kukiwa na uwezekano wa mazungumzo kuendelea siku zijazo.

Pendo kati ya pande zote mbili bado ni kubwa. Marekani iliitaka Urusi kuwaondoa wanajeshi wake kwenye mpaka wa Ukraine lakini haikupata hakikisho kwamba hilo litafanyika.

Urusi ilidai kuwa Nato kutoa hakikisho kuwa haitawahi kutoa uanachama kwa Ukraine. Marekani ilikataa hili moja kwa moja.

Bi Sherman alisema Marekani imekataa mapendekezo ya Urusi ambayo hayakuwa muhimu kwa serikali ya Marekani, ikiwa ni pamoja na matakwa ya Urusi kwamba Nato isiijumuishe kamwe Ukraine katika muungano huo.

"Hatutaruhusu mtu yeyote kushutumu sera ya Nato ya mlango wazi, ambayo imekuwa muhimu katika muungano wa Nato," alisema.

Kulingana na Bi Sherman, ujumbe wa Marekani uliwaambia Warusi kwamba uvamizi wowote ungekabiliwa na "gharama kubwa na matokeo zaidi ya yale waliyokabiliana nayo mwaka wa 2014" wakati Urusi ilipotwaa rasi ya Crimea kutoka Ukraine.

Hatua hizi zinaweza kujumuisha vikwazo dhidi ya taasisi muhimu za kifedha, udhibiti wa mauzo ya nje, "kuimarishwa kwa nguvu za Nato kwenye maeneo ya washirika" na kuongeza msaada wa usalama kwa Ukraine, aliongeza.

Bw Ryabkov alisema mazungumzo hayo yalikuwa "kama ya kibiashara " lakini aliionya Marekani "kutopuuza hatari" za mvutano huo.

Mazungumzo hayo ya Geneva ni ya kwanza kati ya mikutano kadhaa kati ya maafisa wa Marekani na wa Urusi wiki hii, ambayo pia itajumuisha mkutano katika makao makuu ya Nato huko Brussels na katika baraza la kudumu la Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, linalojumuisha Urusi.

Russian troop build-up: View from Ukraine front line
Maelezo ya picha, Urusi inaongeza wanajeshi wake kwenye eneo la mpaka wake na Ukraine

Mkutano wa Jumatatu, hata hivyo, ulifanyika bila washirika wa Marekani kutoka Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ukraine, na kusababisha kuhakikishiwa kutoka kwa Bi Sherman na maafisa wengine wa Marekani kwamba Ukraine, Ulaya na Nato zitajumuishwa katika maamuzi yoyote.

Mapema Jumatatu, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell Fontelles alisema anaamini uvamizi wa Urusi bado unawezekana. "Kuna wanajeshi 100,000 wa Urusi upande wa pili wa mpaka," alisema. "Nadhani hawajaenda huko kunywa kahawa!"

Taarifa zaidi kuhusu mzozo wa Ukraine:

Bw Borrell aliongeza kuwa ameambiwa hakuna kitakachokubaliwa bila ya "ushiriki mkubwa wa EU".

Kupanuka kwa maeneo yanayodhibitiwa na majeshi ya NATO tangu mwaka 1997:

A graphic showing Nato's expansion since 1997
Maelezo ya picha, Ramani inayoonyesha kupanuka kwa maeneo yanayodhibitiwa na majeshi ya NATO tangu mwaka 1997:

Urusi imekanusha mara kwa mara kuwa haina mpango wowote wa kuivamia kijeshi Ukraine. Mwezi uliopita, serikali ya Urusi ilichapisha orodha ya matakwa ikiwa ni pamoja na ahadi kwamba Ukraine haitawahi kujiunga na Nato.