Mzozo wa Ukraine: Marekani yaonya oparesheni ya 'opotoshaji' ya Urusi

Chanzo cha picha, EPA
Urusi inapanga kufanya vitendo vya uchochezi ili kutafuta kisingizio cha kuivamia Ukraine, afisa mmoja wa Marekani amesema.
Msemaji wa Pentagon alisema watendaji wa Urusi walikuwa wakipanga operesheni ya "bendera ya uwongo", ili kuruhusu Moscow kuishutumu Ukraine kwa kuandaa shambulio. Urusi imepuuzilia mbali madai hayo.
Haya yanajiri baada ya wiki moja ya mazungumzo kati ya Marekani na Urusi kwa lengo la kutuliza mvutano
Siku ya Ijumaa Ukraine iliishutumu Urusi kwa kuhusika na udukuzi wa tovuti kadhaa rasmi.
Kabla ya udukuzi huo, ujumbe ulionekana kuwaonya Waukraine "kujitayarisha kwa mabaya". Hata hivyo hitilafu hizo zimerejeshwa ndani ya saa chache.
Marekani na Nato wamelaani shambulizi hilo na wametoa msaada kwa Ukraine. Urusi haijatoa tamko lolote kuhusu udukuzi huo.
Siku ya Ijumaa Msemaji wa Pentagon John Kirby aliwaambia waandishi wa habari kuhusu kile alichosema ni mipango ya Urusi.
"Imeweka tayari kundi la watendaji kufanya kile tunachoita operesheni ya bendera ya uwongo, operesheni iliyopangwa kuonekana kama shambulio dhidi yao au watu wanaozungumza Kirusi nchini Ukraine kama kisingizio cha kuingia," alisema.
Wahudumu hao walipewa mafunzo ya vita vya mijini na kutumia vilipuzi kutekeleza hujuma dhidi ya waasi wanaoiunga mkono Urusi, maafisa wa Marekani walisema.
Wazara ya Ulinzi wa Ukraine imesema vitendosawa na hivyo vinapangwa dhidi ya vikosi vya Urusi vilivypo kwenye eneo lililojitenga la Moldova.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amejibu kwa kusema ripoti hizo hazina msingi wowote na "haijathibitishwa na chochote".

Hatua kubwa ya Marekani
Sio kawaida kwa Marekani kujitokeza hadharani na maamuzi maalum ya kijasusi kama haya.
Lakini utawala wa Biden umeamua kwa uwazi kujaribu kusambaratisha madai yoyote ya uasi wa Urusi dhidi ya Ukraine kwa kufichua mkakati unaodaiwa kuwa hujuma na upotoshaji.
Msemaji wa Pentagon John Kirby alisema Marekani ilitaka ulimwengu ujue jinsi uvamizi unaweza kutokea, kwa sababu hali hii ilitoka kwenye riwaya iliyotumiwa na Warusi huko Crimea.
Matamshi ya afisa huyo wa Marekani yanafuatia kauli ya awali ya Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Jake Sullivan, ambaye aliwaambia waandishi wa habari kuhusu ujasusi kwamba Urusi inaweka msingi wa kujaribu kutengeneza kisingizio cha kuivamia Ukraine.
Alisema Urusi inatumia mbinu iliyotumia kuvamia Crimea mwaka 2014.
Urusi imekusanya silaha pamoja na maelfu ya wanajeshi kwenye mpaka na Ukraine, na hivyo kusababisha hofu ya uvamizi.
Maafisa wa Marekani na Urusi wamekuwa katika mazungumzo kwa muda wa wiki moja iliyopita katika jaribio la kupunguza mvutano kuhusu Ukraine, lakini makubaliano kidogo yanaonekana kufikiwa.
Urusi inakanusha kuwa inapanga kuivamia Ukraine bali inatafuta hakikisho dhidi ya shughuli za Nato katika eneo la mashariki, jambo ambalo nchi za Magharibi zinasema haziwezi kutoa.













