Rais Ben Ali: Sauti za siri zafichua muda wa mwisho wa dikteta wa Tunisia

BBC imepata kanda za sauti zisizo za kwadia zinazoaminika kuwa simu zilizopigwa na aliyekuwa rais wa Tunisia Zine al-Abidine Ben Ali wakati alipokuwa akisafiri kuelekea ughaibuni 2011.

Nyakati hiizi za mwisho zinaonesha jinsi utawala wake ulivyoanguka , na hivyobasi kumaliza hatma ya uongozi wake wa kidikteta uliodumu kwa miaka 23 na hivyobasi kuamsha harakati za kuleta demokrasia katika eneo hilo maarufu Arab Spring Uprising.

Sauti hizo zilizorekodiwa zimechanganuliwa na wataalamu wa sauti ambao walipata hakuna Ushahidi wa uingiliaji wa sauti hizo au utumizi mbaya.

Ben Ali alifariki akiwa ughaibuni 2019 , lakini BBC ilicheza sauti hizo kwa watu wanaowajua watu wanaohusika , na wanaamini kwamba sauti hizo ni za kweli - hatua inayothibitisha uhalisia wake.

Hatahivyo baadhi ya watu wanaohusika wamekana madai yake. Iwapo ni halisi , sauti hizo zinatoa picha halisi ya mabadiliko ya hali ya Ben Ali katika saa 48 za mwisho za utawala wake , huku akianza kuelewa athari za maandamano yaliokuwa yakikumba taifa lake lenye maafisa wa polisi wanaoogopwa mno.

Sauti hizo ambazo zimesishirikishwa katika taarifa hii zilianza kurekodiwa tarehe 13 mwezi Januari 2011. Sauti ya kwanza ni ya simu ya mtu anayeaminika kuwa mwandani wake Tarak Ben Ammar, mfanyabiashara Tajiri wa vyomboa vya Habari ambaye ni maarufu kwa kumshinikiza mwelekezi George Lucas kutengeneza filamu ya kwanza ya Star Wars nchini Tunisia..

Mapema siku hiyo Ben Ali alikuwa ametoa hutuba kwa taifa kupitia runinga , katika jaribio la kuzima moto wa maandamano hayo.

Maandamano hayo ya matatizo ya kiuchumi na miongo kadhaa ya utawala wa kiimla na ufisadi yaliazna wiki kadhaa mapema baada ya kijana mchuuzi wa barabarani, Mohamed Bouazizi, kujichoma moto wakati maafisa walipomzuia kuuza mazao katika mji wa Sidi Bouzid.

Kufikia tarehe 13 mwezi Januari takriban watu 100 walikuwa wamefariki katika maandamano ambayo yalikuwa hayazuiliki katika mji mkuu.

Lakini Ben Ali anasikika akiwa ametulizwa wakati Ben Ammar anaonekana kumtukuza kwa sifa.

"Ulikuwa mzuri sana, huyu ndiye Ben Ali ambaye tumekuwa tukimsubiri!" Anasema Ben Ammar kwenye rekodi hiyo.

Ben Ali anajidharau, akisema hotuba yake ilikosa ufasaha, lakini msiri wake anamtuliza.

"Si hivyo ... umerudisha historia. Wewe ni mtu wa watu. Unazungumza lugha yao," rafiki yake anasema

Ben Ali anacheka kwa kile kinachosikika kama kujituliza moyo. Lakini hotuba iliyotolewa kwa umma wa Tunisia ni wazi haitoshi. Siku iliyofuata, maandamano yanazidi na kutishia kuivamia Wizara ya Mambo ya Ndani. Mipango inafanywa kwa familia ya Ben Ali kupanda ndege kutoka nje ya nchi kwa usalama wao - kuelekea Saudi Arabia - na Ben Ali kisha anashawishiwa kuwasindikiza, anasema.

Maudhui na muda wa rekodi zinazofuata zinamweka Ben Ali kwenye ndege hii.

Anaweza kusikika akipiga simu kadhaa zinazozidi kwa watu watatu - wanaoaminika kuwa waziri wake wa ulinzi, mkuu wa jeshi, na mtu wa karibu - Kamel Eltaief.

Anaanza kwa kuuliza mtu tunayeelewa kuwa Waziri wa Ulinzi Ridha Grira kuhusu hali ilivyo Tunisia. Grira anamwambia kuwa rais wa muda sasa yameteuliwa . Ben Ali anamtaka Grira kurudia taarifa hii mara tatu, kabla ya kujibu kuwa atarejea nchini "baada ya saa chache".

Kisha anampigia simu mwanamume ambaye BBC inaamini kuwa msiri wake wa karibu Kamel Eltaief. Ben Ali anamwambia Eltaief kwamba waziri wa ulinzi amemhakikishia matukio yamedhibitiwa.

Eltaief hatahivyo anarekebisha dhana hiyo

"Hapana, hapana, hapana. Hali inabadilika kwa kasi na jeshi halitoshi," rafiki yake anamwambia.

Ben Ali anamkatisha na kumuuliza: "Je, unanishauri nirudi sasa hivi au la?" Anapaswa kurudia swali mara tatu zaidi kabla ya Eltaief kujibu vizuri.

"Mambo si mazuri," Eltaief anajibu hatimaye.

Ben Ali kisha anatoa wito kwa mtu ambaye tunaamini kuwa ni mkuu wa jeshi, Jenerali Rachid Ammar. Ammar haonekani kuitambua sauti inayompigia. "Mimi ndiye rais," Ben Ali hana budi kumwambia.

Ammar anamhakikishia kwamba "kila kitu kiko sawa". Tena, Ben Ali anauliza swali lile lile alilomuuliza Eltaief - je, arudi Tunisia sasa? Rachid anamwambia itakuwa bora kwake "kusubiri kidogo".

"Tunapoona kwamba unaweza kurudi, tutakujulisha, Bw Rais," Ammar anamwambia Ben Ali.

Anampigia simu waziri wake wa ulinzi kwa mara nyingine tena, akiuliza kama anafaa kurejea nyumbani, na wakati huu Grira yuko wazi zaidi, akimwambia Ben Ali kwamba "hawezi kumhakikishia usalama wake" ikiwa atafanya hivyo.

Mara tu baada ya saa sita usiku, ndege ya Rais Ben Ali inatua Jeddah, Saudi Arabia. Anaamuru rubani ajitayarishe kwa safari yake ya kurejea, na yeye na familia yake wanasindikizwa hadi kwenye Nyumba ya Wageni ya King Faisal Palace.

Lakini rubani anakaidi agizo hilo. Anamwacha Ben Ali na kuruka kurudi Tunisia.

Akiamka Saudi Arabia asubuhi iliyofuata, Ben Ali anampigia tena simu waziri wake wa ulinzi. Grira anakiri utawala haudhibiti kile kinachotokea mitaani. Anamwambia Ben Ali kwamba kuna mazungumzo hata ya mapinduzi. Ben Ali anapuuzilia mbali hili kama hatua ya "Waislamu wenye itikadi kali", kabla ya kuzungumza tena kuhusu kurejea nyumbani.

Grira sasa anaonekana kujaribu kujiweka sawa na bosi wake.

"Kuna hasira mitaani kwa njia ambayo siwezi kuelezea," Grira anasema. Anaonekana kutaka kuwa wazi na rais, na kuongeza: "Ili usiweze kusema kwamba nilikupotosha, na uamuzi ni wako."

Ben Ali anajaribu kutetea sifa yake. "Nimefanya nini mitaani? Niliwahi kuihudumia."

"Ninakupa hali, sio maelezo" Grira anajibu.

  • Tarehe 17 Desemba 2010 mchuuzi wa Tunisia alijichoma moto baada ya kuzuiliwa kuuza mazao.
  • Kitendo chake, na kifo kilichofuata, kilisababisha maandamano makubwa - zaidi ya watu 100 walikufa katika ghasia hizo.
  • Rais Ben Ali alitoa hotuba kwa taifa tarehe 13 Januari ambapo aliahidi kuchukua hatua kuhusu bei ya vyakula.
  • Jioni hiyo Ben Ali alipanda ndege na familia yake kuelekea Saudi Arabia

Ndani ya saa chache serikali mpya inaundwa nchini Tunisia - ambayo wengi wa mawaziri hao hao, akiwemo Grira, walidumisha misimamo yao. Ben Ali hakuwahi kurudi katika nchi yake, akibaki Jeddah, Saudi Arabia, hadi kifo chake mnamo 2019.

Waziri wa Ulinzi Ridha Grira na Mkuu wa Jeshi Rachid Ammar walikataa kutoa maoni yao kuhusu rekodi hizo walipowasiliana na BBC. Waziri wa Ben Ali, Kamel Eltaief na Tarak Ben Ammar, walikanusha kuwa simu zao zilipigwa, huku Ben Ammar akiongeza kuwa hakujaribu kumhakikishia rais kuhusu utawala wake.

BBC imetumia zaidi ya mwaka mmoja kufanyia utafiti kuhusu uhalisi wa rekodi hizo. Zimechambuliwa na wataalamu kadhaa wakuu wa uchunguzi wa sauti nchini Uingereza na Marekani ambao walitafuta dalili za kuchezewa au kuhaririwa, au uchakataji wa 'uongo wa kina' ambao unaiga sauti kwa njia isiyo halali. Hakuna pendekezo la aina yoyote ya upotoshaji lililoweza kupatikana.

BBC pia ilitaka kuthibitisha utambulisho wa wale walio kwenye simu kwa kuwachezea dondoo zinazofaa watu wanaojua angalau mmoja wa wazungumzaji wanaoonekana kusikika. Walioshauriwa ni pamoja na maafisa watatu wakuu wa usalama wa Ben Ali, viongozi wa chama chake cha kisiasa, na hata mwigaji wa sauti wa rais.

Wote waliofikiwa wangeweza kutambua wazungumzaji na hawakuibua wasiwasi kuhusu uhalisi. Ushahidi mwingine pia unathibitisha historia ya simu hizi, ikiwa ni pamoja na kauli za awali za Waziri wa Ulinzi Grira na Mkuu wa Jeshi Ammar kwamba walizungumza na rais alipokuwa kwenye ndege, na kumbukumbu za Ammar zinalingana kwa karibu na maudhui ya wito wake.

Rekodi hizo zinaonyesha jinsi mtawala wa kiimla ambaye alisimamia serikali ya ukandamizaji na ya kutisha kwa miaka 23 alikuwa amefikishwa hali ya kuchanganyikiwa na alikuwa chini ya huruma ya maagizo ya mawaziri wake katika dakika zake za mwisho madarakani. Mnamo 2011, wakati wa uhamisho wake huko Saudi Arabia, Ben Ali alipokea kifungo cha maisha bila kuwepo kwa vifo vya waandamanaji wakati wa mapinduzi.