Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Utawala wa Zine al-Abidine Ben Ali Tunisia, anakumbukwa vipi?
Kiongozi wa zamani Tunisia Zine el-Abidine Ben Ali amefariki uhamishoni akiwa na miaka 83.
Ben Ali alioongoza nchi hiyo kwa miaka 23 na alipongezwa kwa kuidhinisha utulivu na ufanisi wa kiasi fulani wa kiuchumi.
Lakini alishutumiwa pakubwa kwa kukandamiza uhuru wa kisiasa na kwa ufisadi ulioenea pakubwa.
Mnamo 2011, alitimuliwa madarakani kufuatia maandamano ya umma. Hili lilisababisha wimbi la maandamano katika ulimwengu wa kiarabu.
Takriban nusu ya viongozi wa mataifa hayo ya kiarabu walitimuliwa au kumeshuhudiwa mizozo kufuatia kutimuliwa kwa rais huyo wa Tunisia katika kilichokuja kujulikana kama vuguvuvgu la machipuko katika ulimwengu wa kiarabu au Arab Spring.
Ben Ali alikimbilia Saudia alipoondoka madarakani na ameishi huko mpaka kufariki jana Alhamisi.
Anatarajiwa kuzikwa leo Ijumaa Saudi Arabia, mawakili wake wameliambia shirika la habari la Reuters.
Udhibiti mkali ndio uliomponza
Zine al-Abidine Ben Ali alifanikiwa kusalia madarakani kwa miaka 23.
Mwishowe, alichelea kuchukua hatua kulizima wimbi la vuguvugu ambalo halikutarajiwa na lililopata umaarufu mkubwa.
Ben Ali alilazimika kutimuka nchini wakati wa wimbi hilo mnamo 2011.
Aliingia uongozini mnamo 1987, kwa kumtimua kiongozi aliyekuwepo Habib Bourguiba na kuishia kuwa rais wa pili nchini.
Alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza, Ben Ali aliahidi mageuzi, demokrasia , haki kwa wanawake na elimu.
Lakini umwagikaji damu katika nchi jirani Algeria katika miaka ya 1990 ulimfanya kuhofia wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya kiislamu, na wakati aliyazuia yaliokuwa yakishuhudiwa Algeria kuingia nchini mwake, alishindwa kuiwasilisha jamii ilio na uwazi zaidi.
Alifanikiwa kuidhinisha ukuwaji wa uchumi Tunisia lakini hakuna aliyeshawishika kwa ushindi wake mara tatu na kwa 99.9% katika uchaguzi mkuu.
Baada ya ukandamizaji wa miaka kadhaa mageuzi yalijiri kufuatia kifo cha Mohamed Bouazizi - kijana mmoja ambaye alihisi kuteseka na kuchoshwa na hali ya maisha chini ya utawala wa viongozi kama Ben Ali.
Bouazizi alikuwa muuza matunda na mboga pasi kuwa na kibali kwasababu alishndwa kupata ajira.
Mnamo Desemba 2010, Bouazizi alijiteketeza moto, hatua iliyozusha maandamano ambayo mwisho wake yalichangia kuanguka utawala wa Ben Ali, aliyewashangaza wengi wakati alipopanda ndege na kuelekea Saudia.
Mnamo Juni 2011, mahakama nchini Tunisia ilimhukumu kiongozi huyo wa zamani - akiwa hayuko nchini - miaka 35 gerezani kwa ubadhirifu wa fedha.
Udhibiti wake mkali wa jamii, uligubikwa kwa mtandao wa majasusi, watoa taarifa na maafisa wa siri wa polisi waliomsaidia kiongozi huyo kusalia madarakani, lakini mwishowe hasira dhidi ya utawala huo mkali ndio uliomponza.
Kifo chake Ben Ali kinajiri siku kadhaa baada ya Tunisia kuandaa uchaguzi wa pili wa huru wa urais tangu alipotimuliwa.
Umetokana na kifo cha rais aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza kidemokrasia nchini humo, Beji Caid Essebsi, aliyeingia madarakani mnamo 2014.