Barua kutoka Afrika:Jinsi KFC nchini Kenya ilivyokaangwa kuhusu uhaba wa chipsi

Katika mfululizo wetu wa barua kutoka kwa wanahabari wa Kiafrika, mtangazaji wa Kenya Waihiga Mwaura anaandika kuhusu kile ambacho mzozo wa hivi majuzi kuhusu uhaba wa chipsi za KFC unasema kuhusu kilimo nchini mwake.

Ninapohitaji kujiongezea kalori za haraka ninapopata muda katika ratiba yangu ya shughuli nyingi unaweza kunipata mara kwa mara nikibugia mlo wa KFC.

Kula chipsi hizi kunaweza kuibua hisia ambazo hata wewe mwenyewe huzijui kwa sababu ya miaka mingi ya matangazo ya kampuni za kimataifa .

Lakini kamwe sijawahi kufikiria kitendo hicho kama kauli ya kisiasa au kiuchumi kuhusu biashara ya kilimo duniani na nafasi ya Kenya ndani yake.

Wiki hii hata hivyo, manunuzi ya bidhaa kutoka masoko ya kimataifa hadi humu nchini imekuwa mada kuu hapa kwani KFC ilisema haikuweza kutoa chipisi kwa vile haikuweza kuagiza viazi vyake kutoka Misri.

Badala yake, wateja walikuwa wakipewa vyakula mbadala kama vile ugali - Chakula ambachp watu wengi hawaendi KFC kukila.

Kampuni hiyo haitoi viazi ndani ya nchi, licha ya kwamba vinakuzwa kwa wingi na wakulima kulazimika kuviuza kwa bei ya chini.

Viazi ambavyo ni salama kula

Viazi, kwa hakika, ni zao la pili kwa kuliwa nchini Kenya baada ya mahindi, na hulimwa zaidi na wakulima wadogo.

Tatizo, inaonekana, lilikuwa kwamba wasambazaji wa ndani watarajiwa hawakupitia mchakato wa uhakikisho wa ubora wa KFC ambao unahakikisha "chakula chetu ni salama kwa matumizi ya wateja wetu", afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Afrika Mashariki Jacques Theunissen aliambia gazeti la Standard.

Hata hivyo alisema kwamba viungo vingine - hulinunuliwa kwenye soko la Kenya na kampuni hiyo imesema imejitolea kutetea bidhaa za humu nchini.

Ongeza hasira katika mitandao ya kijamii, wito wa kususia kampuni hiyo na hatimaye kuahidi kuwa itatafuta msambazaji anayefaa kutoka Kenya kuiletea viazi.

Hata hivyo, wapinzani walikuwa wepesi kutumia fursa hiyo.

Chicken Inn ilitoa tangazo na mwanamume anayetabasamu akibugia kifurushi cha chipsi - zote kutoka viazi vya humu nchini bila shaka.

Burger King pia ilisema ilikuwa na chipsi za kutosha.

Ingawa kampuni hizi zingine zinaweza kupata vyanzo mbadala vya viazi, haijabainika haswa kwa nini baada ya miaka 11 ya kuwa nchini, KFC haijapata msambazaji anayekidhi viwango vyake.

Francis Kimemia, gavana wa kaunti ya Nyandarua inayolima viazi, pia alitoa maoni yake akisema kuwa wakulima wake wanazalisha mboga bora. Alisema kuwa msimamo wa KFC "haujali wakulima".

Hasira sasa zimeanza kupoa lakini hili limefichua mianya katika mfumo wetu wa kilimo maana yake baadhi ya wakulima wetu wananyimwa soko zuri la hapa nyumbani.

Kutegemea bidhaa za kuagizwa kutoka nje

Sisi ni sehemu ya biashara ya kikanda inayozidi kuunganishwa ya chakula, ambayo ina faida zake - ikiwemo bei ya chini.

Lakini kama matokeo, ikiwa Kenya ingelazimishwa kufunga mipaka yake kwa uagizaji wa chakula kwa muda wa mwezi mmoja tu, bidhaa nyingi tunazozipenda hazitapatikana au zitakuwa ghali sana kununuliwa.

Uagizaji bidhaa mwaka jana kutoka Uganda, kwa mfano, ulifikia $250m (£165m).

Bidhaa kama mayai, asali, mahindi, maharagwe, mtama, mihogo, wimbi na viazi vitamu pamoja na bidhaa za maziwa husafirishwa mpakani na kisha kuuzwa kwa faida ndogo.

Wataalamu wanasema kuwa gharama za leba na nyinginezo za kilimo ni nafuu nchini Uganda, na hivyo kufanya bidhaa kuwa nafuu zaidi kuliko inayozalishwa hapa.

Lakini pia inaweza kuwa suala la mtazamo. Nchini Uganda nimegundua kuwa kilimo kinakubaliwa na watu wote, ilhali nchini Kenya watu wengi wanaonekana kutaka kazi za ofisi.

Nilipokuwa nikishughulikia uchaguzi wa mwaka jana nchini Uganda nilihoji watu wengi mashuhuri ambao wote waliishi nje ya mji mkuu, Kampala, kwenye maeneo makubwa ya ardhi ambako walilima chakula chao wenyewe.

Iwapo viongozi hao hao wangeishi Kenya, pengine wangeishi katika mashamba yenye lango na kilimo kidogo kwenye sehemu hizo

Ni hali hiyo hiyo ukiangalia biashara ya Kenya na Tanzania - jirani yetu upande wa kusini.

Mtazamo hasi kuhusu kilimo pamoja na sekta iliyojaa rushwa inamaanisha kwamba hakuna mtu anayeshangaa samaki wanapoagizwa kutoka China, sukari kutoka Brazili au tumbaku kutoka Uturuki.

Huenda Kenya isiweze kushindana kwa muda mfupi linapokuja suala la gharama za uzalishaji. Lakini kuna fursa kwa Kenya kuwa kituo cha kikanda cha usindikaji wa chakula, na hivyo kuongeza thamani ya bidhaa.

Kuweza kusambaza viazi vilivyochongwa kwa KFC ni mfano mmoja wa kile kinachoweza kutolewa ili kukuza soko la ndani.

Kwa bahati mbaya, shughuli nyingi zinazofanyika nchini Kenya kuhusu usindikaji zinafanywa na makampuni ya kigeni yanayofadhiliwa na mtaji. Faida huishia kuondoka nchini.

Huku uchaguzi ukikaribia mwezi wa Agosti, wagombeaji wamekuwa wakitoa ahadi za ajira, lakini hatujasikia mengi kuhusu jinsi ya kufufua sekta hii ya biashara ya kilimo.

Na wachache wa wabunge wetu watarajiwa wanaweza kuwa hawako tayari kukabiliana na makundi maslahi na utepetevu katika sekta ambayo hapo awali ililisha nchi .

Mabadiliko yanaweza kuwa polepole - na wakati huo huo, ninapozila chipsi za KFC sasa nitakengeushwa na mawazo kuhusu biashara ya kimataifa.

Barua zaidi kutoka Afrika