Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Barua kutoka Afrika : Hamaki kuhusu mbinu za kuaibisha wanazotumia watoza madeni Kenya
Katika mfululizo wetu wa barua kutoka kwa waandishi wa habari wa Kiafrika, mtangazaji wa Kenya Waihiga Mwaura anaandika kwamba watoza deni au wanaokopesha watu wameendelea kushutumiwa kwa unyanyasaji na vitisho wakati wanajaribu kurejesha mikopo waliotoa kupitia programu za kukopesha za kidijitali.
Mchungaji alijitokeza katika chumba chetu cha habari katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi na malalamiko ya kushangaza.
Kwa zaidi ya kipindi cha wiki moja, alipokea simu nyingi za watoza madeni waliodai kwamba mmoja wa waumini wake alikuwa amemsajili kama mdhamini katika mkopo aliochukua.
Hapo awali yule mtu alifikiri ni utani lakini baada ya simu kadhaa za kukasirisha kutoka kwa watoza deni aliacha kuwa mdadisi hadi kushangazwa na mwishowe alikasirika juu ya jinsi deni hilo lilikuwa linamtia aibu.
Undani wa mazungumzo ya simu yalibadilika siku hadi siku.
Hapo awali wakopeshaji walikuwa na adabu na walimuomba tu azungumze na muumini wake aliyemdhamini kulipa mkopo ambao alikuwa amechukua zaidi ya mwezi mmoja uliopita.
Lakini muda mfupi baadaye, wale watoza deni waliopiga simu walizidi kuwa wakali na hata kumwita mchungaji bandia ambaye alikuwa amekataa kusema ukweli kwa waumini wake juu ya kulipa deni na kuahidi kwamba watafanya simu yake 'ilipuke' kwa simu zao zisizokoma.
Kuongeza chumvi kwenye kidonda, walimtukana mkewe wakati alipojaribu kuingilia kati.
Tishio la kumtoa figo
Kwa siku kadhaa mchungaji hangeweza kutumia simu yake kwasababu alikataa kufuata matakwa ya watoza deni.
Na baada ya simulizi hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na hashtag #Debtofshame, Wakenya wengi walianza kuzungumzia uzoefu wao walipokabiliwa na watoza deni.
(Sijaweka viunganishi vya taarifa hiyo au ujumbe wa Twitter kwasababu wanataja kampuni) @ onesmus336 alisema alionywa kuwa "nisipolipa, watakuja kuchukua figo yangu".
@Memokityok alisema aliwahi kukopa shilingi 2,000 za Kenya sawa na ($ 18; £ 13), na siku 10 baadaye
"Nilikuwa sinywi maji, sikuweza kulala wala kufikiria. Nilitukanwa matusi yote ambayo mtu angeweza kufikiria".
@muriuki_ngeera alisema alikuwa akifanya kazi kama wakala wa kurejesha deni na wafanyikazi walikuwa na malengo ya kila siku kufikia.
"Wamiliki hawakujali jinsi utakavyopata pesa zao. Wanachotaka wao ni kupata pesa zao tu. Ilibidi niache kazi hiyo kwa ajili ya kilinda heshima yangu", akaongeza.
Soko la pesa za kwenye simu ya mkononi lanawiri
Hakuna shaka kwamba Wakenya wanapenda kuchukua mikopo kupitia programu za kukopesha za kidigitali.
Ni njia yenye busara, unaweza kuifikia kwa wepesi na haihitaji dhamana.
Lakini ndani yake kuna shida kwa wakopeshaji wanaotumia tabia za ulipaji kupima uaminifu wao licha ya kwamba hawajawahi kukutana na wateja wao ana kwa ana.
Kwa kweli, hakuna ambalo lingewezekana ikiwa bara la Afrika halingekuwa kiongozi katika utumiaji wa pesa za kwenye simu duniani.
Waendeshaji mitandao ya simu za mkononi wametawala huduma za pesa barani Afrika kwa muongo mmoja uliopita.
Hivi karibuni hata hivyo, kumekuwa na mwangaka katika kampuni za teknolojia ya kifedha ambazo zimeweka msingi thabiti katika soko, zingine zikisaidiwa na vikundi vikubwa vya mitaji katika masoko ya Magharibi na Asia.
Wanatumia vizuri pengo lililopo katika sekta ya mikopo ambapo wapata mapato ya chini hawana fursa ya kupata mkopo kwalsababu wanakosa fursa za ajira, dhamana au wadhamini.
Lakini kuingia kwao katika soko la Afrika kumeibua wasiwasi mkubwa juu ya ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa hawadhibitiwi, na kwasababu ya mtindo wao wa kufanya biashara usiofaa.
Soko lao kubwa wameweza kunasa vijana wanaotafuta deni kwa kila namna na kampuni zinawaaibisha kwa kutumia mbinu zisizo za kawaida ikiwa wanashindwa kulipa.
Na wakati Wakenya wamekuwa wepesi wa kuchukua mikopo hii, wengine wameelezea viwango vyao vya riba kuwa vya juu mno.
Wakati riba ya mkopo wa wastani wa benki ni kati ya 12% na 14% kila mwaka, kwa mkopo wa kwenye programu ya simu riba yake inaweza kuwa kutoka kati ya 75% na 395% kwa mwaka.
Rehani kupitia mikopo ya njia ya simu za mkononi
Kwa kuongezea, wengine wameshutumiwa kwa tabia mbaya ya kukopesha na mkopeshaji mmoja wa Kichina anayedaiwa kuhitaji ulipaji wa mkopo ndani ya siku 30 wakati Google, mwenyeji wa programu hizi, inahitaji wakopaji kuruhusiwa siku 60 kulipa.
Lakini mwenyekiti wa Chama cha Wapeanaji Mikopo kwa njia ya kidigitali Kenya, Kevin Mutiso, ni mwepesi kuwatetea wanachama wake, akisema kumuaibisha mtu kwa deni alilochukua ni dalili mbaya ya wazo nzuri ambalo limesaidia wafanyibiashara wadogo wadogo kufikia mikopo kwa haraka sana.
Anasema bila mkopo wa njia ya kidijitali, Wakenya wengi wasingekuwa na uwezo wa kuendelea na shughuli zao kipindi cha kufungiwa kutotoka nje tangu kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 zaidi ya mwaka mmoja.
Watu wameweza kununua chakula, kulipa kodi ya nyumba, kulipa usafiri na huduma zingine na pia ada ya shule kupitia mikopo hii ya kwenye simu, anasema.
Ingawa wengine wanaamini kanuni ni ufunguo wa kuwazuia wapeanaji mikopo wabaya huku wengine wakiwa na wasiwasi kuwa kanuni hiyo itazuia ukuaji wa tasnia ambayo inaweza kushikilia ufunguo wa ajira na uwekezaji katika uchumi ulioathirika na Covid-19.
Na hata kwa kanuni kama vile Sheria ya Ulinzi wa Takwimu ya Kenya ya 2019 inaonekana haiwezekani kuzuia nguvu kubwa ya kukopesha kidijitali ambayo - kulingana na waangalizi wengine wa soko - hivi karibuni inaweza kufadhili kizazi kijacho cha rehani kupitia simu za rununu.