Barua kutoka Afrika: Kwanini Malkia wa Uingereza ana kiti cha Ufalme Nigeria?

Katika safu yetu ya barua kutoka kwa waandishi wa Kiafrika, mwandishi wa habari wa Nigeria na mwandishi wa riwaya Adaobi Tricia Nwaubani wanaandika kuhusu kiti cha enzi kilichotengwa kwa Malkia wa Uingereza katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Imani kati ya watu wa Efik kusini mwa Nigeria ni kwamba mmoja wa wafalme wao wa Karne ya 19 alikuwa ameoana na Malkia Victoria wa Uingereza.

"Nilisikia kwanza kuhusu hilo mnamo 2001, wakati nilikuwa nikipitia makumbusho na kuona barua hii ya kupendeza kati ya Malkia Victoria na Mfalme Eyamba," alisema Donald Duke mwenye miaka 60, ambaye alifanya ukarabati mkubwa kwenye jumba la kumbukumbu la kitaifa na pia alianzisha makumbusho ya biashara ya watumwa katika mji mkuu wa jimbo la Cross River mjini Calabar, wakati alipokuwa gavana huko tangu 1999 hadi 2007.

"Nilidhani ni muhimu tuandike historia yetu, kwa hivyo tulifanya utafiti mwingi," alisema.

Mfalme Eyamba wa tano alikuwa mmoja wa wafalme wawili walio katika mji wa pwani wa Calabar, wakati huo uliundwa na nchi mbili huru.

Mfalme Eyamba V wa Mji wa Duke na Mfalme Eyo Honesty II wa Mji wa Creek walisimamia shughuli za kabila la Efik katikati ya karne ya 19, na kudhibiti biashara na wafanyabiashara wa Ulaya.

Kwa sababu ya eneo lao kando ya pwani, Efik iliendeleza uhusiano wa muda mrefu na Wazungu, ambao uliathiri sana utamaduni wao.

Mara nyingi walichukua majina ya Kiingereza, kama vile Duke na Henshaw, na mavazi ya kitamaduni ya wanaume na wanawake ni sawa na mitindo ya Kiingereza ya enzi ya Victoria.

Jamii ya Efik pia ilitawala biashara ya watumwa. Walifanya kazi kama watu wa kati kati ya wafanyabiashara wa Kiafrika kutoka maeneo ya bara na wafanyabiashara weupe kwenye meli haswa kutoka miji ya Kiingereza kama Liverpool na Bristol.

Walijadili bei za watumwa, kisha wakakusanya mrabaha kutoka kwa wauzaji na wanunuzi. Walifanya kazi bandarini, wakipakia na kushusha, na kuwapatia wageni chakula na vitu vingine.

"Wafalme walitajirika sana. Familia zilikuwa maarufu. Walidhibiti eneo kubwa zaidi la watumwa kutoka Afrika," Bwana Duke alisema.

Mashuhuda wa wakati wa biashara ya utumwa

Zaidi ya Waafrika milioni 1.5 walisafirishwa kwenda kwenye kile kilichoitwa Ulimwengu Mpya - Marekani - kupitia bandari ya Calabar na kuifanya kuwa moja ya sehemu kubwa zaidi ya kutoka wakati wa biashara ya mabara

Kitabu kilicho na jarida la Karne ya 18 cha mfanyabiashara wa watumwa wa Efik - kilichoandikwa kwa Kiingereza cha lugha ya Pidgin na kugunduliwa katika nyaraka za kimishonari za Uskoti - kilichapishwa mnamo mwaka 1956.

Kilipewa jina la 'Diary of Antera Duke, ndio akaunti ya ushuhuda uliobaki wa biashara ya watumwa na mfanyabiashara wa Kiafrika.

Miongo kadhaa baada ya biashara ya watumwa kukomeshwa nchini Uingereza mnamo 1807, mizigo ya kibinadamu ilikuwa bado ikisafirishwa kwenda nchi nyingine kupitia Calabar.

"Ilikuwa muhimu kwamba Malkia Victoria alikuwa na wafalme wa Calabar upande wake," Bwana Duke alisema.

"Aliandika barua akiuliza kwamba waache kufanya biashara ya watu na kuanza kufanya biashara ya viungo, mafuta ya mawese, vioo, na vitu vingine."

Hapa ndipo hadithi inaanza.

Katika barua yake kwa Mfalme Eyamba, Malkia Victoria alitoa vishawishi ambavyo vilijumuisha ulinzi kwake na kwa watu wake.

Kisha akasaini kama "Malkia Victoria, Malkia wa Uingereza", ambaye mkalimani wa eneo hilo alipeleka kimakosa kama "Malkia Victoria, Malkia wa Watu Wazungu".

Mfalme Eyamba aliamua kwamba ikiwa angekubali ulinzi kutoka kwa mwanamke, basi lazima waoane. Alimwambia hivyo katika jibu lake lililoandikwa, na akasaini kama, "Mfalme Eyamba, Mfalme wa Watu Wote Weusi".

"Alikuwa mkali nadikteta," alisema Charles Effiong Offiong-Obo, mkuu wa Efik ambaye pia ni mwandishi wa sasa wa ukoo wa Duke Town.

"Aliandika kwa Malkia na akasema anataka kumuoa ili wote wawili watawale dunia."

Mtu anaweza kufikiria tu majibu ya Malkia Victoria wakati wa kusoma barua ya Mfalme Eyamba. Lakini hakukataa kabisa ofa yake.

"Alikubali barua ya mfalme na akasema alitarajia kuwa na uhusiano mzuri wa kibiashara naye," Bwana Offiong-Obo alisema.

Barua yake iliambatana na zawadi kadhaa - pamoja na hati ya kifalme, upanga, na Biblia - ishara nzuri ambayo Mfalme Eyamba alitafsiri kama kukubalika kwa ofa yake ya ndoa.

Kwa hivyo, watu walianza kuamini kwamba mfalme wao alikuwa ameoa malkia.

Nakala za mawasiliano kati ya Malkia Victoria na Kings Eyamba na Honesty zinaoneshwa kwenye jumba la kumbukumbu la Kitaifa huko Calabar, jengo ambalo hapo awali lilikuwa kiti cha utawala wa kikoloni wa Uingereza kusini mwa Nigeria.

Baadhi ya barua za asili zimeuzwa kwa mtu binafsi ambaye hakutajwa jina, niliambiwa na mfanyakazi wa Kampuni ya Covers Rare Books Inc, ambayo ilishughulikia uuzaji huo.

Wakati fulani katika Karne ya 20, watu wa Efik walikubaliana kwamba ni mfalme mmoja tu, anayejulikana kama obong, ndiye angewawakilisha, na hivyo kuunganisha viti vya enzi vilivyokuwa vimekaliwa na Wafalme Eyamba na Honesty.

Mwanamfalme anakuwa 'mkwe'

Prince Michael wa Kent alikuwa katika ziara fupi ya faragha huko Calabar mnamo 2017, wakati Obong anayetawala, Edidem Ekpo Okon Abasi Otu V, aligundua kuwa mkwe wa watu kutoka Uingereza alikuwa mjini.

Alimchukua mkuu - mwanachama wa familia ya kifalme ya Uingereza na binamu wa kwanza wa Malkia Elizabeth II - na akamfanya chifu na jina Ada Idagha Ke Efik Eburutu, maana yake "Mtu wa heshima na hadhi ya juu katika Ufalme wa Efik Eburutu".

Barbara Etim James, obong-awan, au malkia, kati ya Efik anakumbuka kwamba alipewa siku mbili tu kupanga sherehe kubwa ya kutunuku jina hilo, ambalo lilifanyika kwenye kasri la obong.

"Wakati wa ziara ya Prince Michael, kwa kila fursa, walimkumbusha kwamba alikuwa mkwe wao. Hata kwenye sherehe, walisimulia hadithi hiyo tena," alisema.

"Prince Michael alifurahi kusikia uhusiano wa kihistoria kati ya Efik na Ufalme wa Uingereza na aliheshimiwa kuongezea uhusiano huo na ukuu wake wa Efik," akaongeza.

Kulingana na utamaduni ulioanza kufuata "ndoa" ya Mfalme Eyamba na Malkia Victoria, kutawazwa kwa Obong wa Calabar bado kunafanyika katika awamu mbili.

Baada ya ibada za jadi kukamilika katika jamii, sherehe ya kutawazwa inaendelea katika Kanisa la Presbyterian (zamani Kanisa la Uskochi), ambapo obong huvaa taji na kofia.

Viti vya enzi viwili vimewekwa kando na anakaa juu ya kimoja, wakati cha pili kimeachwa kitupu kwa Malkia wa Uingereza ambaye hayupo (au Biblia imewekwa juu yake). Mkewe anayejulikana anakaa nyuma yake.

"Hapa tuna muungano kati ya Malkia wa Wazungu na Mfalme wa Watu Weusi," Bwana Duke alisema.