Barua kutoka Afrika : Tamaa ya utajiri wa haraka yawapelekea wengi kutapeliwa Kenya

Muda wa kusoma: Dakika 3

Katika mfululizo wetu wa makala kutoka kwa wanahabari wa Afrika, Waihiga Mwaura kutoka Kenya ameandika kuhusu utapeli wa pesa za mtandaoni ikiwemo mmoja ambaye alifanya biashara kwa kutumia jina lake kulaghai wawekezaji.

Nilipigiwa simu na daktari ambaye sikumjua, akiniuliza ikiwa nimemuhoji bilionea wa Kenya kuhusu bidhaa mpya ya pesa za mtandaoni aina ya Bitcoin katika tovuti moja.

Ghafla nikaingiwa na wasiwasi kwasababu nilijua kuwa nimeingia kwenye mtego wa ulaghai wa mtandaoni ambao umekuwa ukiendelea kwa miaka miwili uliodai kwamba pamoja na bilionea wa mtandaoni, nimezindua jukwaa la biashara ya pesa za mtandaoni.

Lakini licha ya juhudi zangu kuonya Wakenya kuhusu ulaghai huo unaoendelea kupitia majukwaa ya mitandao wa kijamii, ilionekana kuwa walaghai hao walikuwa wanabadilisha anwani yao ya mtandaoni na mikakati yao kulenga Wakenya wasioelewa nini kinaendelea, wanaomka kila asubuhi wakiwa na matumaini kwamba siku itakuwa na mafanikio.

Katika kile ambacho kilionekana kuwa mchanganyiko wa hatari kubwa iliyopo - na tamaa ya kupata mazuri - wengi walitumbikia katika mtengo huu wa walaghai ambao awali ulionekana kuwa majibu ya maombi ya wengi.

Raia wa Marekani alikamatwa.

Utapeli wa hivi karibuni kubainika nchini Kenya ulihusisha programu ya kwenye simu kwa jina la 'Amazon Web Worker Africa', ambayo ilidai kuhusika na kampuni ya Amazon na ilikuwa inafikiwa kupitia simu ya mkononi au tovuti.

Ukweli ni kwamba haukuwa na uhusiano wowote na kampuni kubwa ya manunuzi ya Amazon.

Wiki chache zilizopita, wawekezaji wa programu ya 'Amazon Web Worker' waliamka na kugundua kuwa programu hiyo haipatikani tena yaani imefutwa kabisa katika mfumo wa 'Google Play Store' bila mawasiliano rasmi na walichokuwa wamewekeza ikiwa ni maelfu ya madola pesa zao zikipotea kwasababu hawakuweza kuifikia tana program hiyo.

Pendekezo la programu hiyo lilikuwa rahisi kabisa, unalipwa kwa kuingiza wengine katika mtandao huo na pia unalipwa kwa kuweka akiba katika programu hiyo.

Wakati huo huo, waliahidiwa asilimia fulani ya mapato unayopata wakati ulichowekeza kinaendelea kuwa salama.

Muda mfupi baada ya programu hiyo kutoweka, mamia ya Wakenya walianza kumininika kwenye mitandao ya kijamii kuonesha wasiwasi wao, wengine wakilaumu marafiki wa karibu na familia waliowatambulisha katika programu hiyo kama "fursa ya uwekezaji".

Taarifa njema ni kwamba mamlaka ya Kenya ilitangaza kumkamata raia wa Marekani, 50, ambaye anadaiwa kuhusika na sakata ya programu ya "Amazon Web Worker".

Polisi ilisema mtu huyo anashukiwa kuwa sehemu ya njama hiyo ya utapeli na atashitakiwa kwa makosa ya utakatishaji wa fedha na ulaghai wa mtandaoni.

Kukamatwa kwake - ambako kulifanyika akiwa uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Nairobi akijaribu kutoroka, kumekuwa matumaini kwa baadhi ya wawekezaji kwamba wataweza kupata pesa zao walizotapeliwa.

Ulaghai katika uwekezaji kumekuwa jambo la kawaida nchini Kenya na huenda hili linahusika na kiwango cha chini cha ukosefu wa ajira.

Takwimu za kabla ya janga kutoka nchini Kenya zinaonesha kuwa asilimia 40 ya vijana nchini Kenya hawana ajira kuanzia Februari 2020 na wakati janga la virusi vya corona likiwa linatikisa katika wimbi la tatu, hali ya ukosefu wa ajira sasa hivi imekuwa hata mbaya zaidi, ingawa takwimu za hivi karibuni bado hazijatolewa.

Utapeli huo hujitokeza kwa njia mbalimbali - kuanzia makubaliano yanayoonekana kuwa mazuri sana ya ardhi - uwekezaji katika mashamba, ununuzi wa nyumba, biashara ya ubadilishanaji wa fedha za kigeni mtandaoni na hata mipango ya ajabu ajabu inayoonesha mapato ya juu au ya haraka.

Biashara ya fedha za mtandoani pia nayo imekumbwa na utata mwingi tu huku ile ya Bitcoin ikisambaratika nchini Kenya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mipango hii ya utapeli huwa ikoje?

•Wawekezaji wa awali huwa wanazawadiwa kiwango cha juu cha mapato kutokana na walichowekeza lakini wanahitaji wawekezaji zaidi kujiunga ili kuendeleza kiwango cha juu cha mapato

•Wawekezaji zaidi hutapeliwa baada ya kujiunga kwasababu uwekezaji wao hutumiwa kulipa wawekezaji wa awali, wao hupokea pesa kidogo. Na inakuwa hawana namna zaidi ya kutafuta wengine zaidi kujiunga ili kuongeza mapato yao

•Baadhi ya mipango hiyo ya utapeli hufilisika idadi ya wawekezaji wapya ikipungua

Katika moja kati ya utapeli wa biashara ya fedha za mtandaoni, Wakenya wengi wanasemekana kwamba walipoteza zaidi ya dola milioni 25, na bado hawajawahi kupata pesa zao hadi hii leo.

Wahiga Mwaura alizungumza na mwekezaji mmoja ambaye alipoteza karibu dola 30,000 katika mpango kama huo Afrika lakini cha kushangaza ni kwamba alisema bado anaweza kujaribu tena iwapo fursa itajitokeza kama makubaliano ni mazuri.

Ikiwa watu watakuwa na akili za namna hiyo, bila shaka kuna uwezekano mkubwa wakaendelea kupoteza pesa zao.