Wapishi roboti wanaoweza kukupikia mlo wa krismasi

The Moley Robotic Kitchen

Chanzo cha picha, Moley Robotics

Iwapo una wasi wasi wa kuipikia familia yako siku ya krismasi basi hauko peke yako.

Lakini kwa Krismasi zinazokuja sasa kuna mambo mapya - mpate mpishi roboti kufanya kila kitu.

Kampuni kadhaa za teknolojia kwa sasa zinatengeneza roboti zinazoweza kupika na kupakua chakula, kwa huduma za kibiashara na zile za nyumbani.

Kati ya wale walio mstari wa mbele ni kampuni yenye makao yake mjini London ya Moley Robotics, ambayo inatarajiwa kutoa roboti yake ya Moley Robotic Kitchen mwaka ujao.

Ikiwa inapandikwa kwenye dari la nyumba, mikono miwili ya roboti hiyo inaning'inia ikiwa inaweza kupika zaidi ya mapishi 5000.

Unachagua tu kile ungependa ipike kwa kugusa skirini kisha roboti hiyo inafanya kila kitu.

Ili kusaidia kuunda roboti hiyo, Moley ilimuajiri mpishi mahiri Tim Anderson, ambaye mwaka 2011 aliibuka mshindi kwenye shindano la kupika la BBC, MasterChef.

Anasema angetengeneza chakula na roboti ingeweza kupangwa kurekodi kile alichokifanya

Chef Tim Anderson

Chanzo cha picha, Paul Winch-Furness

Maelezo ya picha, muasisi wa roboti anayepika, mpishi Tim Anderson

Mkurugenzi mkuu wa Moley, Mark Oleynik anasema mfumo wake hufanya kazi nyuma ya kioo ili mikono ya roboti isimgonge mwanadamu.

"Kama tahadhari zaidi, tuna mifumo ya radar inayoweza kutambua vifaa visivyohitajika kati ya roboti na eneo lolote na kusitisha huduma mara moja ili kuzuia hatari yoyote."

Bw Oleynik anaongeza kuwa mpishi huyo roboti anaweza kukusaidia kupika mlo wako wa Krismasi. Lakini kwa mpishi yeyote wa nyumbani aliye na nia ya kuiagiza, kwa saa kuna tatizo - gharama.

Bei ya chini kabisa kwa roboti ya Moley ni pauni 150,000. Roboti zingine wapishi ambazo ni ghali zinatengenezwa na kampuni ya Israeli ya Kitchen Robotics na ile ya Marekani ya Dexai Robotics.

Japo gharama ya roboti hizo inatarajiwa kushuka, nyingi ya teknolojia hizi mwanzo huwa nje ya uwezo wa watu wengi wanaotaka kuzitumia nyumbani, lakini wakati teknoljia zitaendelea kuboreka zaidi gharama yao itapungua.

Mgahawa ambao tayari unatumia roboti kwa mapishi yake yote ni wa Ufaransa wa kupika pizza wa mini-chain Pazzi.

Biashara hiyo inamilikiwa na wanafunzi wawili wa masuala ya roboti, waliogundua roboti yao ya kupika pizza na kisha wakafungua mgahawa wao wa kwanza mjini Paris mwaka 2019. Kwa sasa wako na mgahawa wa pili mjini Paris na mwingine mjini Brussels.

Pazzi's pizza-making robot at work

Chanzo cha picha, Pazzi

Mara inapopata agizo la kupika, roboti hiyo hukamilisha kila kitu inastahili kufanya ikiwemo kukanda unga, kuongeza viungo, kupika pizza, kuiweka kwa boksi , kuikatakata na kumkabidhi mteja ikiyafanya yote hayo kwa muda wa dakika tano.

Muasisi na mkurugenzi mkuu Philippe Goldman anasema roboti zimepangwa kudumisha hali juu ya kazi. Iwapo roboti itafinya unga na igundue kuwa unga ule una mashimo, itaukataa, iitupe na itengeze unga mwingine.

Bw Godman anasema Pazzi imepokea zaidi ya maswali 1,000 kuhusu roboti zake, mengi yakitoka Italia, Uingereza, Marekani na Ujerumani.

Mikaela Pisani mtaalamu wa mafunzo ya mashine anasema roboti hizo zitapunguza virusi kwenye chakula, na kudumisha usafi wa chakula.

Lakini pia ameonya kuwa zinaweza kuchangia kupotea ajira.

The touch screen of the Moley Robotic Kitchen

Chanzo cha picha, Moley Robotics

Wesley Smalley, mkuu wa zamani wa mgahawa wa hadhi ya juu wa Seasonality mjini Berkshire anasema roboti za jikoni haziwezi kuwa chaguo la migahawa cha hadhi za juu.

"Siamini roboti inaweza kuchukua mahala pa mwanadamu, hasa wakati inahusu mgahawa wa hadhi ya juu," Anasema.

"Ninakubali kuwa roboti zitasaidia kwenye ufanisi wa kufanya kazi zingine, Lakini usisahau kuwa mtu atahitajika kupanga progamu zao na kuongeza chakula."