Farc: Kamanda wa waasi wa Colombia 'El Paisa' auawa Venezuela

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi mpinzani wa zamani wa waasi wa Farc Colombia ameuawa katika shambulizi la kuvizia nchini Venezuela, vyombo vya habari vya ndani viliripoti Jumapili.
Hernán Darío Velásquez, jina la utani El Paisa, aliripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi katika jimbo la Apure nchini Venezuela.
Kifo chake hakijathibitishwa rasmi na jeshi la Colombia lilisema halina habari kuhusu mauaji hayo.
Vyombo vya habari vya ndani vimekisia kwamba mamluki wanaweza kumuua Velásquez, wakitafuta malipo kwa kukamatwa kwake.
Mamlaka ya Colombia ililiambia gazeti la El Tiempo kwamba hawatathibitisha kifo chake hadi maafisa wauone mwili wake. Msemaji wa Rais wa Colombia Iván Duque aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba ofisi yake ilikuwa ikitafuta habari zaidi.
Waasi wa Farc walikuwa kundi la Marxist ambalo liliendesha vita vikali dhidi ya serikali ya Colombia kwa zaidi ya miaka 50, kabla ya mwishowe kuitisha usitishaji mapigano mnamo 2016.
Kamanda wa moja ya vitengo vya kuogopwa zaidi vya Farc, Velásquez alijulikana kwa ukali wa mashambulizi yake.
Alikuwa nyuma ya mlipuko wa gari kwenye kilabu cha kijamii katika mji mkuu wa Colombia, Bogotá, ambao uliua watu 36 na kujeruhi karibu 200 zaidi mnamo 2003.
Sifa yake ilikuwa kwamba alipojiunga na mazungumzo ya mchakato wa amani mjini Havana mwaka wa 2016, wengi waliona hiyo kama ishara kwamba waasi hao walikuwa wamejitolea kweli kuweka chini silaha zao.
Lakini mwaka wa 2018 aliachana na mapatano hayo na akajitokeza tena mwaka mmoja baadaye pamoja na viongozi wa zamani wa Farc Iván Márquez na Jesús Santrich kutangaza kuundwa kwa kundi jipya la waasi linaloitwa Segunda Marquetalia, na akatangaza kwamba alikuwa akichukua silaha kwa mara nyingine tena.
Ikiwa kifo chake kitathibitishwa itakuwa ni hasara ya pili kwa kundi hilo mwaka huu.
Santrich, ambaye wakati mmoja alikuwa mhusika mkuu katika mchakato wa amani, aliuawa katika ufyatulianaji wa risasi nchini Venezuela mwezi Mei na kile kikundi cha wapinzani kilidai kuwa ni makomando wa jeshi la Colombia.
Takriban wapiganaji 13,000 wa kundi la Farc wameweka chini silaha zao tangu kusitishwa kwa mapigano mwaka wa 2016 na kundi hilo tangu wakati huo limebadilika na kuwa chama kidogo cha kisiasa, kinachoshikilia viti 10 katika bunge la Colombia.
Hata hivyo, ghasia zinaendelea katika baadhi ya maeneo ya Colombia ambapo takriban wapinzani 5,000 wanaendelea kupigana dhidi ya vikosi vya serikali.
Serikali ya Colombia imewashutumu mara kwa mara viongozi wa Venezuela kwa kuwahifadhi wapinzani wa Farc na imedai kuwa shambulio la helikopta iliyokuwa imembeba Rais Duque mwezi Juni ilipangwa kutoka katika jimbo hilo jirani.














