Pablo Escobar:Mhalifu sugu aliyevuka mipaka katika vita vyake na serikali

Chanzo cha picha, Getty Images
Mhalifu sugu wa Colombia na mlanguzi wa dawa za kulevya Pablo Escobar alijijengea sifa kwa ujanja wake kukwepa mkono wa sheria na kufanya kila alilotaka ili kuendelea na biashara yake haramu .
Lakini alichotambuliwa kama mbinu yake kubwa ni ukatili wa hali ya juu ambao hata uliitisha serikali .
Escobar kama mkuu wa kundi la Medellín, kwa hakika alikuwa mfanyabiashara hodari wa dawa za kulevya ulimwenguni katika miaka ya 1980 na mapema miaka ya 90.
Sekta ya kokeni ilipostawi nchini Colombia — kwa sababu ya kuwa karibu na Peru, Ecuador, na Bolivia, ambako koka inapandwa na baadaye kugeuzwa kuwa kokeni — Escobar alijiingiza katika magendo ya dawa za kulevya. Katikati ya miaka ya 1970 alisaidia kuunda shirika la uhalifu ambalo baadaye lilijulikana kama shirika la Medellín. Washirika wake mashuhuri ni pamoja na ndugu wa Ochoa: Juan David, Jorge Luis, na Fabio. Escobar aliwahi kuwa mkuu wa shirika, ambalo lilizingatia sana uzalishaji, usafirishaji, na uuzaji wa kokeni.
Baadhi ya uhalifu wa kutisha aliotekeleza Escobar
- Aliweka bomu kwenye ndege.
- Aliweka bomu kwenye duka kubwa lililofurika wateja .
- Aliweka bomu katika makao makuu ya kitaifa ya shirika la ujasusi.
- Alikuwa ametangaza zawadi ya kiasi cha pesa kwa yeyote aliyemuua polisi Medellín.
- Aliwahi kumuua waziri amaye alizungumza kuhusu kuwapeleka kwa lazima walanguzi wa dawa za kulevya Marekani ili kushtakiuwa
- Alimuua mkurugenzi wa gazeti moja lililokosoa uhalifu wake na kisha kulipua bomu katika ofisi za gazeti hilo
- Escobar alimuua mgombeaji wa urais aliyeahidi kupambana na viongozi wa magenge ya uhalifu na wauzaji wa dawa za kulevya
Katikati ya miaka ya 1980 shirika la Medellin lilitawala biashara ya kokeni, na Escobar alikuwa na nguvu na utajiri wa ajabu.
Kulingana na ripoti zingine, alikuwa na mali ya thamani ya takriban dola bilioni 25, ambayo ilimsaidia kuwa maisha ya kifahari ambayo ni pamoja na shamba la ekari 7,000 (hekta 2,800) kwa jina Hacienda Nápoles (iliyopewa jina la Naples, Italia) huko Colombia. Inasemekana iligharimu $ 63 milioni na ilikuwa na uwanja wa mpira wa miguu, sehemu ya kuweka sanamu za dinosaur, , uwanja wa kupigania ng'ombe, uwanja wa ndege, na uwanja wa tenisi.
Mali hiyo pia ilikuwa na mbuga ya wanyama wa pori ambayo ilikuwa na twiga, viboko, na ngamia, kati ya wanyama wengine. Kwa kuongezea, Escobar alifadhili miradi mingi kusaidia masikini, akilinganishwa na Robin Hood. Mtazamo huo ulimsaidia kushinda uchaguzi wa kiti katika Bunge la nchi hiyo mnamo 1982.
Gereza kama kasri
Katikati ya umwagikaji wa damu uliokua, msako mkubwa ulifanywa ili kumkamata Escobar, wakati serikali pia ikianza mazungumzo ya kujisalimisha kwake.
Mnamo Juni 1991, siku ile ile ambayo Bunge la Colombia lilipiga kura kukataza kuwapeleka raia wa Colombia nchini Marekani kushtakiwa kwa uhalifu katika katiba mpya ya nchi, Escobar alijisalimisha na baadaye akafungwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kufungwa kwake, hata hivyo, hakukuathiri sana shughuli zake za jinai na mtindo wake wa maisha. Aliruhusiwa kujenga gereza la kifahari, ambalo lilijulikana kama La Catedral. Sio tu kwamba gereza hilo lilikuwa na kilabu cha usiku, sauna, maporomoko ya maji, na uwanja wa mpira, pia ilikuwa na simu, kompyuta, na mashine za faksi. Walakini, baada ya Escobar kuwatesa na kuwaua washirika wawili wa kundi lake la uhalifu huko La Catedral, maafisa waliamua kumhamishia kwenye gereza lisilo la kifahari. Kabla ya kuhamishwa, Escobar alitoroka kizuizini mnamo Julai 1992.
Serikali ya Colombia — iliripotiwa ikisaidiwa na maafisa wa Marekani na Walanguzi wapinzani wa dawa za kulevya-ilianzisha msako. Mnamo Desemba 2, 1993, Escobar alisherehekea siku yake ya kuzaliwa alipotimu umri wa miaka 44 akidaiwa kufurahiya keki, mvinyo na bangi.
Siku iliyofuata maficho yake huko Medellín yaligunduliwa. Wakati vikosi vya Colombia vilipovamia jengo hilo, Escobar na mlinzi walifanikiwa kufika kwenye paa. Alikimbizwa na kupigwa risasi .Wengine, hata hivyo, walidhani kwamba alijiua mwenyewe. Baada ya kufa, kundi la Medellín pia liliporomoka
Gereza La Catedral lilivyogeuzwa kuwa ukumbi wake wa starehe
Katika ufichuzi kupitia kitabu chake cha ″My War In Medellin,″ kanali Augusto Bahamon ambaye aliwahi kuhudumu kama mkuu wa jeshi aliyesimamia gereza la Escobar alisema Pablo ndiye aliyetengeza muundo wa gereza hilo na kugharamia ujenzi wake .
Akiwa jela ,Escobar aliweza kutazama vizuri sehemu na mandhari ya kuvutia katika bonde la Medellin .Seli yake ilikuwa na vyumba viwili na eneo maalum la kuweka nguo zake .Nje katika mji wake alikozaliwa wa Envigado Escobar aliweza kupunga upepo mwanana wa milima iliyokuwa karibu .
Kanali Bahamon amesema kwamba wakati huo 'sio Escobar ambaye alikuwa akijisalimisha kwa idara ya haki bali ni idara ya haki ndiyo iliyokuwa imejisalimisha kwa Escobar'
Baadaye Bahamon alistaafu baada ya kushtumia kwa kumruhusu nyota wa soka wa Colombia Rene Higuita kwenda gereza kumuona Escobar bila kupewa idhini iliyohitajika .
Bahamon alisema Escobar ndiye aliyekuwa akiielekeza serikali jinsi ya kujenga gereza hilo na hata kuamua walinzi waliofaa kumlinda .

Chanzo cha picha, Getty Images
Escobar na washirika wake 17 mwezi juni mwaka huo walikubali kujisalimisha kwa mamlaka ili kupunguziwa adhabu ya kifungo jela na kuepuka kukmatwa kupelekwa nje ya nchi kujibu mashtaka kadhaa ya uhalifu yakiwemo ulanguzi wa dawa za kulevya ,mauaji na utakatishaji fedha .
Bahamon aliongeza kwamba meya wa mji wa Envigado ndiye aliyetekeleza maagizo ya escobar kuhusu namna ya kujenga gereza hilo na hata ndiye aliyependekeza kuboreshwa kwa mfumo wa kutoa maji taka ambao baadaye Escobar aliutumia kukwepa .
Kabla ya operesheni kubwa ya serikali dhidi ya kundi la Medellin mnamo 1989, Escobar alikuwa amegeuza mji wa Envigado kuwa himaya yake ya kibinafsi, hata kuanzisha jeshi lake la polisi.
Baadhi ya polisi na viongozi wa kisiasa wamedai kwamba Escobar aliendelea kuendesha biashara yake ya dawa za kulevya na kuagiza mauaji ya watu kutoka gerezani.
Utawala wa Rais Cesar Gaviria ulitetea msamaha kwa Escobar ukisema mpango huo ulipunguza ugaidi na kudhoofisha shirika la Medellin na mengine ya ulanguzi wa dawa za kulevya














