Hypersonic : Kwanini Marekani ina wasiwasi mkubwa kuhusu silaha hii ya China?

Muda wa kusoma: Dakika 3

Waziri wa ulinzi nchini Marekani Lloyd Austin alisema siku ya Alhamisi kwamba hatua ya China kutengeneza silaha ya hypersonic inasababisha wasiwasi katika eneo hilo.

Amesema kwamba Marekani itakuwa tayari kukabiliana na tishio lolote kutoka kwa China.

Austin alikuwa amewasili mjini Seoul kushiriki katika majadiliano ya kila mwaka kuhusu usalama na Korea Kusini. Wakati huo, mataifa yote mawili yalizungumzia hofu inayozuka kutokana na mataifa jirani ya Korea Kusini , China na Korea kaskazini.

Zote China na Korea Kaskazini zinajaribu kutengeneza silaha zenye uwezo mkubwa zaidi.

Korea Kaskazini imekuwa ikifanyia majaribio silaha zake. Wakati huohuo, Jeshi la China limezindua roketi kama hizo mara mbili katika siku za nyuma , ambazo baada ya kuzunguka dunia yote ziliweza kulenga ilipolenga kushambulia.

Inaaminika kwamba Marekani ina wasiwasi kuhusu jaribio hilo.

Mwezi Julai, China ilifanya jaribio ambalo wataalamu walisema lilikuwa jaribio la silaha ya hypersonic. Ijapokuwa China ilisema kwamba lilikuwa jaribio lililohusisha matumizi ya roketi ya zamani.

Akizungumzia kuhusu jaribio la silaha ya China mwezi Julai , Lloyd Austin alisema, tuna wasiwasi kuhusu uwezo wa kijeshi ambao China inaunda kwasababu unazua hofu na majirani zake

Alitaja juhudi za China kutengeneza silaha mpya ili kuimarisha uwezo wake wa kijeshi.

''Tutaendelea kuongeza uwezo wetu ili kujilinda na washirika wetu na tutajitayarisha kukabiliana na tishio lolote la China'', alisema.

Marekani pia inatengeneza silaha za hypersonic

Mwezi uliopita , Mkuu wa jeshi nchini Marekani Jenerali Mark Milley alisema kwamba Marekani pia inatengeneza silaha za hypersonic.

Wataalamu wanaamini kwamba Marekani ina wasiwasi kwamba haipaswi kusalia nyuma ya China na Urusi katika utengenezaji wa silaha.

Mwezi Septemba mwaka huu, Marekani ilidai kwamba ilifanikiwa kufanyia majaribio silaha yake aina ya Hypersonic.

Silaha aina ya hypersonic inaweza kusafiri kwa kasi ilio mara tano zaidi ya kasi ya sauti na inaweza kutumia kasi hiyo kufanya mashambulizi kwa kukwepa mifumo ya kujilinda dhidi ya silaha za angani.

Hatahivyo , wataalamu wengine wanasema kwamba makombora ya hypersonic huenda yakachangia katika kuondoa hofu ama kusitisha mashindano ya utengenezaji wa silaha.

'Njia za kidiplomasia dhidi ya Korea Kaskazini'

Kuhusu Korea kaskazini, Lloyd Austin alisema kwamba alikuwa na majadiliano ya kina na waziri wa ulinzi nchini Korea Kusini Soo Wook kuhusu suala hilo na pia vilevile walizungumzia kuhusu ushirikiano wa kibiashara.

Alisema kwamba juhudi za Korea Kaskazini zilikuwa zinachangia hofu katika usalama wa eneo hilo. Alisisitiza kwamba zote Marekani na Korea Kusini ziko tayari kuchukua njia ya mazungumzo katika suala la Korea kaskazini.

Wakati huohuo, waziri wa ulinizi nchini Korea Kusini Soo Wook alisema kwamba ili kuweza kuwepo kwa amani ya kudumu katika rasi ya Korea, ni muhimu kwamba washirika wake waelewe kujitolea kwa Korea Kusini - korea kaskazni na Korea Kaskazini - Marekani.

Licha ya hali mbaya ya kiuchumi na hali mbaya iliosababishwa na mlipuko wa corona, Korea Kaskazini imekataa ombi la Marekani kuanza mazungumzo.

Korea kaskazini inasema kwamba Marekani kwanza inapaswa kubadilisha tabia yake kwa Korea Kaskazini na kuondoa vikwazo ilivyoiwekea.

Kwa upande mwengine , Utawala wa Joe Biden unasema kwamba vikwazo hivyo vya kimataifa havitaondolewa hadi taifa hilo litakapokusitisha utengeneza wa silaha za kinyuklia.

Mapema wiki hii, Pentagon ilitoa ripoti kwamba Marekani inapaswa kuimarisha ushirikianao na washirika wake ili kukabili tabia za kichokozi za jeshi la China na tishio kutoka kwa Korea kaskazini.