Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo Ethiopia: Raia wa kigeni waendelea kushauriwa waondoke
Ujerumani na Ufaransa zimekuwa nchi za hivi punde zaidi kuwashauri raia wao kuondoka Ethiopia huku kukiwa na ongezeko la vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Marekani na Uingereza pia hivi majuzi walitoa ushauri kama huo, na Umoja wa Mataifa umeanza kile unakitaja kuwa kuhamisha kwa muda baadhi ya wafanya kazi wake.
Haya yanajiri wakati wapiganaji wa Tigray wanasema wanazidi kusonga mbele kuelekea mji mkuu Addis Ababa.
Waziri mkuu Abiy Ahmed anasema ataeleka mstari wa mbelea kuwakabili waasi.
Mzozo huo ambao umedumu mwaka mmoja umechangia kutokea mgogoro wa kibinadamu, huku maelfu wakikabiliwa na hali ya njaa kaskazini mwa Ethiopia.
Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni kulazimishwa kukimbia makwao
Mjumbe maalum wa Marekani Jeffrey Feltman, anasema hatua zinapigwa kupata suluhu la kidiplomasia lakini hilo linahatarishwa na kuendelea kwa mapigano.
Alisema pande zote zinaonekana kuamini kuwa zinakaribia kupata ushindi wa kijeshi.
Bw Feltman alionya kuwa iwapo waasi wataelekea Addis Ababa itakuwa ni hali ambayo haitakubalika na janga.
Ni vigumu kuthibitisha ripoti kutoka mstari wa mbele wa vita lakini kundi la TPLF linasema wapiganaji wake wanadhibiti mji ulio umbali wa kilomita 200 kutoka mji mkuu Addis Ababa. Serikali ya Ethiopia imekuwa ikikanusha kuendelea kusonga mbele kwa waasi.
'Wacha tukutane mstari wa mbele'
Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni nchini Ujerumani ilisema raia wake wanapaswa kuhama nchi hiyo bila kuchelewa.
Wakati huo huo nakala moja ya ndani ya Umoja wa Mataifa ilisema familia za wafanyakazi wa kimataiafa zinapaswa kuondolewa ifikapo Novemba 25.
Awali Marekani na Uingereza walitangaza kuwa walikuwa wanawaondoa wafanyakazi wa kidiplomasia wasio hitajika na kuwaambia raia wao wengine kuondoka.
Kwenye ujumbe katika mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu, Abiy Ahmed aliyeshinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2019, alisema anaelekea mstari wa mbele kuongoza wanajeshi.
"Wale ambao wanataka wawe kati ya watoto wa Ethiopia, watakaokumbukwa na historia amkeni leo kutetea nchi yenu. Tukutane mstari wa mbele," alisema.
Alishinda tuzo ya Nobel baada ya kumaliza msukosuko wa karibu miongo miwili na Eritrea ulioendelea baada ya vita kati ya nchi hizo mbili.
TPLF wamepuuza ujumbe wake Abiy ambapo msemaji wake Getachew Reda, alisema "vikosi vyetu havitalegeza kamba katika kufikisha kikomo serikali yake Abiy".
Muungano wa Afrika unaongoza jitihada kupata suluhu kwa vita kwa njia ya mazungumzo lakini hakuna upande umejitolea kwa mazungumzo.
Vita hivyo vilianza kufuatia tofauti kati ya waziri mkuu Abiy na TPLF ambao kwa karibu miaka 27 walitawala nchi nzima na sio tu Tigray.
Bw Abiy aliingia madarakani mwaka 2018 ambapo alifanya mabadiliko ya haraka na kupata amani na hasimu wa muda mrefu Eritrea, lakini TPLF walitengwa.
Mzozo kati TOLF na Abiy kisha ukalipuka na kuwa vita miezi 12 iliyopita wakati vikosi vya Tigray vililaumiwa kwa kushambulia kambi za wanajeshi na kuiba silaha ambapo serikali ya shirikisho ilijibu.