Fahamu namna wafungwa walivyotumia njia za kushangaza kutoroka gerezani

Gereza likiwa na ulinzi mkali

Chanzo cha picha, EPA

Muda wa kusoma: Dakika 4

Wafungwa watatu wanaohusishwa na ugaidi walitoroka gereza la kamiti nchini Kenya mapema juma hili.

Watatu hao Musharaf Abdalla maarufu Alex Shikanda , Joseph Ouma na Mohammed Ali Abikar na Alhamisi walikamatwa katika eneo la Kitui.

Walitoroka kutoka jela inayolindwa zaidi baada kutoboa ukuta wa jela hiyo.

Baadaye walitumia nguo aina ya blanketi na waya kutengeneza kamba ambazo walitumia kupanda kuta mbili ndefu za jela hiyo.

Lakini Musharaf, Joseph na Ali Abikar si watu wa kwanza kutoroka gerezani. Hapa kuna hadithi zingine za kushangaza za kutoroka gerezani ulimwenguni.

Kitendo cha kutoroka jela cha Mfaransa mmoja kwa jini la Redoine Faid mwaka 2018 ni kama hadithi . Redoine Faid - ambaye alitoroka kwa helikopta baada ya kujihami kwa silaha - aliripotiwa kuwa shabiki wa filamu za uhalifu za Hollywood.

Faid aliwahi kusema mtindo wake wa maisha umeigizwa na majambazi wanaochezwa na Robert de Niro na Al Pacino. Alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 25 kutokana na kushiriki kwake katika wizi ambao hakufanikiwa ambapo afisa wa polisi aliuawa mwaka 2010.

Alipata sifa mbaya nchini Ufaransa baada ya kutoroka jela kwa wiki sita mnamo 2013.

Polisi wenye silaha

Chanzo cha picha, EPA

Nchini Ugiriki mfungwa mmoja alitumia helikopta kutoroka kutoka kwa gereza lenye ulinzi mkali si mara moja, lakini mara mbili - mwaka 2006 na 2009.

Ndege zisizo na rubani pia zinakuwa hatari kwa usalama kwa magereza kote ulimwenguni - ripoti zinasema huenda zilitumika kabla ya kutoroka kwa Faid.

Mnamo mwaka wa 2017, mteka nyara aliyepatikana na hatia Jimmy Causey aliweza kutoroka kutoka kwa gereza la South Carolina kwa kutumia vikata waya na simu za mkononi.

Siagi inayonata

Wafungwa kumi na wawili walitoroka katika jela ya kaunti ya Alabama mnamo 2017 baada ya kutumia siagi ya karanga kumlaghai mlinzi ili afungue mlango unaoelekea nje.

Wanaume hao walimchanganya mfanyakazi mpya kwa kupaka siagi juu ya namba kwenye mlango wa kutokea.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Afisa wa eneo hilo alikiri mpango huo ulikuwa wa "mawazo ya werevu", lakini wanaume wote waliishia rumande baadaye.

Joaquin 'El Chapo' Guzman

Mmoja wa watoro wa gerezani wanaojulikana sana katika historia. Ni Joaquin "El Chapo" Guzman. Mlanguzi huyu wa dawa za kulevya alizipa hekaheka jela mbili za Mexico zenye ulinzi mkali.

Mnamo mwaka wa 2001 aliripotiwa kutoroshwa kutoka chini ya ulinzi ndani ya kikapu cha nguo chafu - Alikwepa kukamatwa tena kwa miaka 13 mingine.

Baada ya kurejeshwa gerezani, alitoroka tena kupitia shimo la bafuni mnamo mwaka 2015. Mfumo wa handaki wenye umbali wa maili moja ulikuwa umejengwa chini, ukiwa na taa, uingizaji hewa na reli kwa ajili ya pikipiki.

Joaquin Guzman Loera, aliyejulikana kwa jina 'El Chapo' akipelekwa gereza lenye ulinzi mkali El Altiplano, Mexico City Januari 2016

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa aibu zaidi ya mamlaka ya Mexico, kitendo cha El Chapo cha kutoweka kilinaswa kwenye CCTV.

Baada ya miezi kadhaa ya kukimbia - na mahojiano na mwigizaji wa Hollywood Sean Penn - Guzman hatimaye alikamatwa tena katika jimbo la Sinaloa.

Kulikuwa na uvumi kwamba alitoroka tena mnamo mwaka 2016 - taarifa ambazo zilikanushwa. Alikuwa chini ya ulinzi wa Marekani akisubiri kufikishwa mahakamani wakati huo kujibu mashtaka ya dawa za kulevya baada ya kurejeshwa nchini humo.

Alivaa viatu vya visigino virefu na nguo za mkewe

Mnamo 2012, mlanguzi wa dawa za kulevya Ronaldo Silva, 39, aliripotiwa kutoroka katika gereza moja nchini Brazil kwa kubadilishana nguo na mkewe wakati alipomtembelea.

Silva alivaa nguo za mkewe kabla ya kutoroka

Chanzo cha picha, Brazil Civil Police

Baada ya kuripotiwa kunyoa na kupaka lipstick, alinaswa tena baada ya kuonekana akihangaika kutembea na viatu vya visigino virefu kwenye kituo cha basi kilicho karibu.

Picha ziliibuka akiwa amevalia vazi hilo, likiwemo wigi, baada ya kurudishwa gerezani.

'Houdini raia wa Korea Kusini'

Choi Gap-bok alipata umaarufu nchini Korea Kusini baada ya kutoroka kizuizini katika mkoa wa Daegu mnamo 2012.

Mtaalamu mazoezi ya yoga, alitoka akiwa amejipaka mafuta ili aweze kupita kwenye dirisha la sentimeta 15 kwa 45 lililokusudiwa linatumika kupitishia chakula.

Wachunguzi walisema mwanaume huyo mwenye uzani wa kilo 52)na futi 5 kwa inchi 1.7 alitoroka kwa chini ya dakika moja kwa "akipenya kwa urahisi mithili ya pweza".

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 50 alikamatwa tena baada ya siku sita . Kisha alifungiwa kwenye seli na sehemu ndogo ya kupitisha chakula, isiyoweza.

Kutoroka gereza la Alcatraz

Pengine tukio la kutoroka jela linalojulikana zaidi kati ya yote lilitokea karibu na San Francisco mnamo 1962.

Visiwa ya Alcatraz na Angel

Chanzo cha picha, Getty Images

Lilitambulika kama gereza lenye ulinzi mkali zaidi katika nchi ya wakati huo, Alcatraz lilikuwa kwenye mwamba katikati ya Ghuba ya San Francisco, na iliimarishwa kwa sheria kali na mbinu za ulinzi.

Ilidaiwa kuwa salama sana kiasi cha kwamba wafungwa waliojaribu kutoroka mahali pengine walipelekwa huko kama adhabu. Licha ya hayo, kulikuwa na majaribio zaidi ya dazeni ya wafungwa katika kipindi cha miongo mitatu.

Waliacha vinyago vitandani kabla ya kutoroka

Chanzo cha picha, Getty Images

Mnamo Juni 1962 ukaguzi wa kawaida wa gereza asubuhi ulionesha kwamba ndugu John na Clarence Anglin na mfungwa mwingine, Frank Morris, hawakuwa kwenye vitanda vyao.

Walikuwa wametengeneza vitu mithili ya watu na kuviacha kitandani kisha wakatoroka kupitia matundu ya hewa na kupita kwenye ushoroba usio na ulinzi, kabla ya kuondoka kwenye kisiwa hicho.

Ni nini hasa kilifanyika baadaye bado ni siri, na imekuwa mada ya uvumi wa kina tangu wakati huo.

FBI hatimaye ilihitimisha kuwa huenda watu hao walikufa maji walipokuwa wakivuka, lakini ukurasa wa tovuti ya ofisi hiyo kuhusu kesi hiyo bado ulikuwa unaomba taarifa za umma kuhusu watu hao watatu.