Rais Samia Suluhu tayari amezindua shilingi Trilioni 1.3 fedha za ufadhili kukabiliana na janga la Corona Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Uzinduzi wa Mpango wa Serikali ya Tanzania wa kuinua Uchumi kwa kutumia mkopo wa fedha wa shilingi Trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Korona umeibua mjadala miongoni mwa raia nchini humo huku makundi mbalimbali yajikita kwenye matumizi ya fedha hizo.
Wakati wa uzinduzi huo Rais alitoa onyo kwa watendaji na kuelekeza kuondoa urasimu, usimamizi wa fedha za umma ambalo nalo limetajwa kuwa kupita njia za watangulizi wake kwa nyakati tofauti wamepata kutoa juu ya usimamizi wa mali za umma, kudhibiti mianya ya rushwa na ufanisi wa miradi lakini kila mwaka ripoti za ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu zimekuwa zimekuwa zikiibua ubadhirifu, upotevu wa fedha na matumizi yasiyoelezeka ndani ya taasisi za serikali.
Duru za siasa na uchumi zimebainisha kuwa mpango wa kukopa fedha kutoka IMF ni hatua nzuri na mbinu inayofaa ya kuhami uchumi ambao uliathiriwa na ugonjwa wa korona licha ya utawala uliopita kutotoa takwimu halisi ya maambukizi na vifo. Pia baadhi ya wataalamu wamekosoa uamuzi wa Rais Samia Suluhu kutumia mzabuni mmoja kwa kile alichokiita kuwa zabuni za ushindani zinachukua muda mrefu na kushindwa kukidhi mahitaji muhimu nya muda wa utekelezaji wa miradi ndani ya miezi tisa kuanzia sasa, ambapo imetajwa kuwa huenda ikawa ni kiini cha rushwa, uzembe, upendeleo, pamoja na uwezo mdogo wa mzabuni.
Nini madhara ya utaratibu wa mzabuni mmoja?
Akizungumza katika makao makuu ya nchi hiyo, Dodoma wakati wa kuzindua Kampeni ya Maendeleo dhidi ya UVIKO-19, Rais Samia aliagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kutoa vibali vya utekelezaji wa miradi kwa kupata mzabuni mwenye uwezo wa kutekeleza mradi badala ya kuitisha zabuni kwa mfumo wa ushindani wa wazabuni wengi, ambayo kwa mujibu wa sheria za nchi, huchukua takriban miezi mitatu au zaidi hadi kutangazwa mshindi.
"Kwa wasimamizi, hii miradi iishe kwa miezi tisa. Sitaki tusiitekeleze kwa vizingizio. Wazabuni wapatikane kwa single sourcing, mkitaka kufanya kwa utaratibu mwingine wa kutangaza zabuni kwa miezi mitatu mtatuchelewesha. Twende na single sourcing. Halmashauri, idhini itolewe na PPRA pia urasimu uondolewe katika misamaha ya kodi kwa vifaa kutoka nje ya nchi vinavyokuja kutumika katika miradi hiyo na CAG nawe fuatilia kwa karibu fedha za miradi hii," alisema Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa muktadha huo, hoja ya msingi inayojengwa hapa ni kwamba ingefaa kwa taasisi ya ununuzi wa umma ziambiwe kuharakisha mchakato badala ya kulazimisha kutumia mzabuni mmoja ambaye inaonesha dhahiri kuwa na ukakasi na kujenga mazingira yanayotia shaka. Vilevile uamuzi huo unachochea wasiwasi wa kuibuka dhana ya upendeleo na kupeana zabuni kwa kufahamiana zaidi kuliko uwezo wa kutekeleza miradi husika. Ingawaje kazi zinaweza kufanyika haraka kadiri ya matakwa ya mamlaka za Tanzania lakini hofu hii si ya kupuuzwa asilani.
Dkt. Richard Mbunda, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa utaratibu wa kuondoa ushindani wa zabuni ni pale ambapo kuna Taasisi maalum ya umma imepewa jukumu la kutekeleza miradi husika. Na faida yake ni kupunguza mzigo wa gharama katika miradi inayotakiwa kutekelezwa na kwa muda maalumu kama ulivyotajwa na Rais.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Lakini kutoa zabuni bila ushindani kutaleta upendeleo kwa baadhi ya wazabuni kwa gharama za watu wengine. Rushwa inaweza kutamalaki maana ili mtu au wakandarasi wapate zabuni watahitaji tu kuongea lugha nzuri na wahusika wa kupitisha ambao ni PPRA. Tatu, ni uwezekano wa kutekeleza miradi chini ya kiwango, hili ni jambo ambalo uzoefu unaonesha yapo maeneo ambayo miradi mingi haijadumu kwa sababu ya kutekelezwa chini ya kiwango, lakini gharama za mradi zikiwa za chini. Hili litupiwe jicho kwani ni chanzo kikuu cha kukosekana maadili ya kazi. Nne, gharama za mradi zinaweza zisiwe halisi. Kwamba zinaweza kuwa gharama kubwa zaidi, maana makubaliano ndio yanasimamia gharama za mradi."
Je, ni maeneo gani yanayolengwa katika miradi?
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali imeonesha vipaumbele mbalimbali vilivyopangwa kufanyika kutokana na fedha za mkopo huo. Baadhi ya maeneo yaliyolengwa zaidi ni kama ifuatavyo;-
•Ununuzi magari ya wagonjwa ya kisasa 20 na magari ya kawaida 365.
•Ujenzi wa vituo vya dharura na vifaa kwa hospitali zote kuanzia Taifa hadi halmashauri.
•Uimarishwaji wa mfumo wa usambazaji na ununuzi wa mitungi ya gesi katika hospitali za rufaa.
•Usimikaji wa vinu 44 vya hewa ya Oksijeni kwa ajili hospitali za Taifa na halmashauri
•Ununuzi wa mashine za X-Ray 85
•Ufungaji wa mashine za MRI kwa hospitali za Taifa, kanda na mikoa
..Ujenzi wa vituo vinne vya Telemedicine.
•Ujenzi wa vyumba na ununuzi wa vifaa vya uangalizi maalum (ICU) 72 kwa ngazi ya Taifa, kanda, mikoa na baadhi ya halmashauri.
•Utekelezaji wa miradi ya maji kwa wananchi.
•Utekelezaji miradi ya elimu kama vile madawati, vyumba vya madarasa katika vyuo 17.
•Vituo vinne vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Mapambano ya Tanzania dhidi ya korona yana tafsiri gani kiuchumi?
Kupitia hotuba yake Rais Samia amekiri kuwa kipindi cha miezi sita ya uongozi wake ni kigumu kwa sababu alikutana na hali mbaya ya kiuchumi kutokana na wimbi la pili la ugonjwa wa UVIKO-19, hali iliyoathiri uchumi wa nchi hiyo.
Dkt. Bravious Kahyoza, Mtaalamu wa Masuala ya Uchumi amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa hizo ni hatua maalumu kwenye kipindi maalumu na kwa sababu maalumu. Kwamba ni hatua za kukabiliana na athari za korona kwenye uchumi wa jamii, wakati wa korona kuhami uchumi. Kwa miezi 14 sasa, imesisitizwa kuhitajika hatua za kulinda uchumi. Lakini imeonesha kuwa hatua tu za kusisimua uchumi haziwezi kusaidia Taifa hilo, inahitajika hatua chotara; zile za kusisimua uchumi na za kulinda maisha ya jamii na hii inawezesha kuendeleza maisha.
"Hatua hizi zinajaribu kufanya hilo. Kwa kawaida mahitaji ya kusawazisha mambo katika uchumi ili yawe na maana; zinahitaji kati ya asilimia moja hadi mbili ya pato la taifa kuingizwa kwenye uchumi. Kwa uchumi wa hata shilingi Trilioni 150 na hali halisi ya Tanzania, hakuna uwezo wa kutoa fedha hizo, kwa hiyo, njia mbadala ni ya kuendeleza maisha ya jamii kwa mkopo kama wa IMF. Njia hii inahitaji takribani asilimia 0.5 hadi asilimia moja ya pato la Taifa. Hizi fedha zimepatikana kwa njia ya mkopo uliopo sasa.
Ameongeza kwa kusema, "Ifahamike Korona sio mtikisiko wa uchumi kama mitikisiko mingine. Uamuzi wa kutumia fedha za mkopo kutoka IMF kwa mtindo huu unalenga kukabili tatizo. Ingawa hakuna takwimu madhubuti za dawa za kutibia ugonjwa huo, lakini takwimu kutokana na sera ya afya kwa sasa hizo zinapatikana na ndicho kigezo kilichotumika kupatia mkopo. Hili ni muhimu sana kwa sasa kwa sababu linagusa kwenye uchumi mpana. Hizi ni miongoni mwa hatua zinazoweza kuchukuliwa,
Matendo na maneno ya sasa yanaonesha Tanzania iliathirika mno na imeumizwa na janga la Korona kiuchumi na kijamii. Inaonekana serikali inataka bora kupata doa la kukiri makosa ya utawala uliopita lakini isiendelee kuharibu nchi kiuchumi. Swali pekee lililopo kwa sasa ni je, Serikali inasikiliza zaidi na kuimarisha au itakuwa kama ile iliyopita? Hilo ndilo swali la kufuatilia sasa katika juhudi hizi mpya za serikali."
Je, nini nguvu na tija za tishio na amri za rais?
Miongoni mwa mambo ambayo yanaleta gumzo ni amri ya rais katika utekelezaji wa miradi. Kwamba sheria imeagiza zabuni kupitiwa ndani ya miezi mitatu lakini kwa muda wa mradi ulivyopangwa ni vigumu kutumia sheria hiyo, ikiwa na maana ni kama inakiukwa kutokana na amri za rais.

Chanzo cha picha, AFP
"Kwa wale wanaotaka kuzijua rangi zangu halisi, wajaribu kudokoa fedha hizi au wabadilishe matumizi yale bila maelewano. Kila kona ya nchi inakwenda kuwa na ujenzi wa miradi ya maendeleo. Kwenye fedha hii sina huruma na mtu," alisema Rais Samia.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa na utawala bora wanabainisha kuwa amri za rais mara kadhaa zimekuwa chanzo cha kuongezeka gharama za mradi. Kwamba kamati mbalimbali ndani ya mikoa zinaweza kutumika kukagua mradi mmoja, mfano kamati ya mkuu wa mkoa, katibu tawala wa mkoa na wilaya, wakuu wa wilaya na wengineo.
Kwa miaka sita ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali amekuwa akiibua ubadhirifu mkubwa, uvunjaji wa sheria, miradi hewa na mianya mikubwa ya ulaji rushwa licha ya kuwa katikati ya uongozi mkali wa Rais Magufuli.
Katika muktadha huo tishio alilotoa Rais Samia Suluhu haliendani na uhalisi wa mambo, kwa sababu kwenye kauli yake yenyewe yametumika maneno "sina huruma na mtu". Kauli hiyo yaweza kutafsiriwa kuwa zipo nyakati ambazo kiongozi mkuu wa nchi anakuwa na huruma.
Ndiyo maana watendaji mbalimbali huwa wanahamishwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine au sehemu moja kwenye nyingine, Ifahamike kuwa Rais Samia kwa uzoefu wake serikalini anafahamu vizuri kubadilishwa kwa matumizi ya fedha kutoka maeneo yaliyopangwa kwenda mengine tangu alipokuwa mwanaharakati, mbunge, waziri, Makamu wa Rais na sasa rais wa nchi.
Mfumo wa kutekeleza mipango na sera za umma una ukakasi ikiwa sheria inabadilishwa wakati wowote. Hii ndiyo hoja ya msingi kuangalia mbinu zilizopangwa kutumika kutekeleza miradi hiyo na mafunzo yake yamefanyika vipi hadi kuja na uamuzi huo. Nje ya hapo tunatekeleza tunavyotaka badala ya inavyotakiwa kwa kuzingatia utaratibu rasmi uliowekwa kisheria kupitia Bunge lenye uwakilishi wa watu, kwa sababu tu ya maelekezo ya Rais.












