Kamati maalum ya Corona Tanzania: Chanjo ya Corona ni salama na fanisi

Chanzo cha picha, IKULU, TANZANIA
Kamati maalum ya Corona Tanzania iliyoundwa na rais Samia Suluhu Hassan mwezi uliopita imewasilisha ripoti yake hii leo huku ikisema kuwa chanjo dhi ya ugonjwa huo ni salama na zimeonesha ufanisi.
Kamati hiyo imeishauri serikali kupitia vyombo vyake kulishughulikia suala la chanjo kwa kujiunga na mpango wa covax ulio chini ya mwamvuli wa Gavi.
Mpango wa covax unalenga kuhakikisha nchi masikini kote duniani zinapata mgao sawa wa chanjo licha ya ufinyu wa uwezo wao wa kiuchumi. Mwamvuli wa Gavi unaundwa na mashirika mbalimbali ikiwemo Shirika la Afya Duniani na baadhi ya serikali za nchi tajiri duniani.
"Kamati inashauri Serikali kwa kutumia vyombo vyake iendelee na hatua kuelekea kuruhusu matumizi huru ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kwa kutumia chanjo zilizoorodheshwa na Shirika la Afya Duniani ili kuwapa fursa ya kinga wananchi wake kwa kuwa kupitia uchambuzi wa Kamati, chanjo hizo zina ufanisi na usalama unaokubalika kisayansi," ameeleza Profesa Said Aboud kutoka Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili na Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Hata hivyo kamati imetaka mamlaka zilizo chini ya serikali kuendelea kutoa ushauri juu ya jambo hilo.
"Pamoja na mapendekezo haya, Kamati Huru ya Kitaifa ya Ushauri wa Chanjo (NITAG) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ziendelee kushirikishwa katika kutoa ushauri na kudhibiti chanjo hizo," ameeleza Prof Aboud.
Baada ya kamati kutoa ushauri wake, ni jukumu sasa la serikali chini ya Rais Samia kutekeleza mapendekezo hayo.
Mapendekezo ya kamati kuhusu chanjo ya corona yanapingana na sera ambayo nchi hiyo iliitekeleza wakati wa hayati rais John Magufuli ambaye alipinga chanjo hizo kabla ya kufariki akiwa madarakani mwezi Machi na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa makamu wake Mama Samaia. Msimamo wa Magufuli juu ya chanjo na kudhibiti ugonjwa huo ulipingwa vikali nadni na nje ya nchi hiyo.
Kipaumbele cha utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19
Kamati hiyo imependekeza matumizi huru ya chanjo nchini Tanzania, hii ikimaanisha kuwa hakutakuwa na mtu atakayeshurutishwa kuchoma chanjo hiyo kinyume na matakwa yake binafsi.
Hata hivyo, kamati pia imependekeza pale chanjo itakapoingia Tanzania kuwe na makundi maalumu matano ambayo yatapewa kipaumbele katika utoaji wa chanjo.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Kundi la kwanza ni wahudumu katika vituo vya kutolea huduma za afya na watumishi walio katika mstari wa mbele wa utoaji wa huduma mathalani watumishi sekta ya utalii, hoteli, mipakani, viongozi wa dini na mahujaji.
Kundi la pili ni wazee na watu wazima kuanzia umri wa miaka zaidi ya 50, kundi la tatu ni watu wazima wenye maradhi sugu mengine mathalani kisukari, shinikizo la damu, maradhi ya mfumo wa upumuaji, magonjwa ya figo.
Makundi mengine ni watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama; na wasafiri wanaokwenda nje ya nchi.
Vipi kuhusu takwimu na 'lockdown'?
Kuhusu utolewaji wa takwimu wa mara kwa mara juu ya mwenendo wa ugonjwa huo, kamati imeitaka serikali kurejea katika utaratibu huo. Mara ya mwisho kwa takwimu za ugonjwa huo kutolewa kila siku ilikuwa ni mwaka mmoja uliopita.
"Serikali itoe takwimu sahihi za ugonjwa wa COVID-19 kwa umma na Shirika la Afya Duniani ili wananchi wapate taarifa sahihi toka Mamlaka za Serikali na kuheshimu makubaliano na kanuni ambazo nchi iliridhia," imeshauri kamati.

Kuhusu kujifungia kama njia ya kudhibiti kasi ya maambukizi, kamati imeishauri serikali "kuendelea kuzingatia mazingira ya kitanzania katika udhibiti wa ugonjwa wa COVID-19 katika kuamua kuweka au kutokuweka shuruti ya kujifungia (lockdown) na kuwa na ubunifu ili kuruhusu ukuaji wa uchumi na kuimarisha sekta zinazochangia katika uchumi."
Rais John Magufuli aliweka hadharani wakati janga hilo lilipoipiga nchi hiyo mwaka jana na kusisitiza mapema mwaka huu kuwa katu chini ya utawala wake asingetekeleza sera hiyo ya 'lockdown' kutokana na athari za kiuchumi ambazo zingejitokea. Hatua hiyo pia ilichangia kukosolewa vikali kwa utawala wake.
Kuhusu athari za kiuchumi kwa ujumla wake, kamati imeshauri wizara yenye dhamana ya fedha na uchumi ifanye tathmini ya kina ya athari za janga la COVID-19 na kuweka mpango madhubuti wa haraka wa sasa, wa muda wa kati na wa muda mrefu unaotekelezeka ili kukuza uchumi wa Tanzania.












