Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Chanjo ya Malaria - Maswali ambayo hayajajibiwa
Watafiti na wataalamu wa afya wamekua wakisherehekea hatua ya Shirika la Afya Duniani kuidhinisha utumizi wa chanjo ya kwanza ya malaria.
Huku zaidi ya watoto 260,000 walio na umri wa chini ya miaka mitano wakifariki kutokana na malaria kila mwaka katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, hatua hii ya kihistoria, inaweza kuokoa maelfu ya maisha WHO inasema.
Lakini je watu wataanza lini kunufaika na chanjo hii inayofahamika kama RTS,S?
Tumekuwa tukiangazia hilo na maswali mengine muhimu.
Ni bora na salama kiasi gani?
Chanjo hii ilithibitishwa kuwa na ufanisi miaka sita iliyopita, inatoa kinga dhidi ya malaria kwa asilimia 40 na asilimia 30 ya visa hatari zaidi vya ugonjwa huo.
Tangu mwaka 2019, watafiti wamekuwa wakifanya mipango mipana ya chanjo ya majaribio nchini Ghana, Kenya na Malawi.
Zaidi ya watoto 800,000 wamepokea angalau dozi moja na WHO inasema hakuna hofu yoyote kuhusiana na usalama wa chanjo.
Je! kuna haja ya kuwa na shaka kuwa ulinzi ni mdogo?
Bila shaka ingelikuwa bora zaidi ulinzi ungelikuwa juu zaidi, lakini kile wengi wangesema unahitaji kufikiria juu ya kiwango cha shida - na kupunguzwa kwa asilimia 40 ya mamilioni ya visa vya ugonjwa huku idadi kubwa ya maisha yakiokolewa
Mamlaka za afya pia zinasisitiza kuwa silaha mpya katika mapambano dhidi ya malaria zitumiwe pamoja na hatua zingine za kinga, kama vile kulala ndani ya vyandarua vilivyo na dawa za kuua mbu wanaosababisha malaria.
Mamlaka aa afya pia zinapenda kusisitiza hii ni silaha mpya katika mapambano dhidi ya malaria ikitumika pamoja na hatua zingine za kinga, kama vile vyandarua vilivyotibiwa na dawa zinazolenga vimelea vya malaria.
Je! Chanjo hii inafanya kazi vipi?
Malaria ni vimelea ambavyo huvamia na kuharibu seli zetu za damu ili kuzaliana, na huenezwa na kuumwa na mbu wanaofyonza damu.
Chanjo inalenga vimelea hatari zaidi na vya kawaida barani Afrika: Plasmodium falciparum.
Inajaribu kushughulikia aina ya vimelea vinavyoingia ndani ya damu ya mwathiriwa muda mfupi baada ya kuumwa, kwa kuzuia vimelea hivyo kuingia kwenye seli za binadamu na hivyo kumkinga magonjwa, Dk Alonso alisema.
Inahitaji dozi nne kuwa bora. Tatu za kwanza hutolewa kwa awamu kati ya umri wa miezi mitano, sita na saba, na nyongeza ya mwisho inahitajika karibu na miezi 18.
Watoto wanachukuliwa kuwa katika hatari zaidi ya kufariki kutokana na malaria, tofauti na watu wazima ambao hawajakuwa na nafasi ya kujenga tena kinga ya mwili.
Je! Itagharimu kiasi gani na ni nani atakayelipa?
Chanjo hiyo imetengenezwa na kampuni kubwa ya dawa GSK ambayo imeahidi kusambaza dozi za chanjo kwa wa gharama ya utengenezaji pamoja na 5%, lakini hajabainisha bei.
Suala la ununuzi limeachiwa mataifa na wafadhili kutafuta pesa.
"Jami ya kimataifa ya ufadhili italazimika kujadiliana na hatimaye kuamua jinsi ya kununua chanjo," Afisa mkuu wa afya wa GSK Thomas Breuer aliambia BBC.
Rose Jalang'o, ambaye amekuwa akisimamia mpango wa majaribio nchini Kenya, amesema mamlaka ilikuwa ikisubiri muongozo wa kimataifa juu ya namna chanjo hiyo itafadhiliwa kama sehemu ya mpango wa kitaifa wa chanjo.
Kwa sasa nchini Kenya, sehemu kubwa ya ufadhili wa chanjo unatoka kwa wahisani kama vile muungano wa kimataifa wa chanjo- Gavi na wakfu wa Bill na Melinda.
Ratiba ya usambazaji ni ipi?
Programu za majaribio nchini Ghana, Kenya na Malawi zitaendelea. GSK inasema imetoa msaada wa dozi milioni 10 kwa ajili ya uchunguzi na kufikia sasa robo ya dozi hizo zimetumika.
Kampuni hiyo imejitolea kutoa dozi milioni 15 za chanjo kwa mwaka. Ikiwa pesa zitapatikana basi wanaweza kuanza kupatikana kwa matumizi mapana kutoka mwisho wa 2022 au mapema 2023, Bwana Breuer alisema.
Lakini idadi hiyo huenda isitoshe. Mwisho wa muongo hadi dozi milioni 100 zinaweza kuhitajika kila mwaka, kulingana na Ashley Birkett kutoka Path, ambayo ilisaidia kufanya kazi kwenye mpango wa chanjo.
Kunahitajika miundo mbini gani?
Kwa kuwa chanjo hiyo inawalenga watoto walio na umri wa chini ya miaka miwili huenda ikajumuishwa katika mpango wa chanjo zingine za watoto ili zisihitaji miundo mbinu ya ziada.
Kuna haja ya kuwa na elimu zaidi ya umma na mafunzo ya wafanyikazi wa afya.
Katika mpango wa majaribio nchini Kenya, zaidi ya watoto 200,000 walichanjwa na pia chanjo zilifikishwa hadi maeneo ya vijijini kupitia mipango ya kuwafikia watu nyanjani na kliniki za mbali, Dk Jalang'o aliambia BBC.
Ni chanjo zipi zingine zinatengenezwa?
Chanjo zingine zinazoshughulikiwa , ni pamoja na ile kutoka Chuo Kikuu Cha Oxford nchini Uingereza. Mnamo mwezi Aprili watafiti waliripoti kuwa majaribio ya awali yaliahsiria ufanisi wa asilimia 7.
Lakini utengenezaji wa chanjo za malaria ni mchakato mrefu kwani ni ugonjwa ambao ni vigumu kukabiliana nao ukilinganisha na Covid-19, kwa mfano.
RTS,S ni chanjo ya kwanza ya malaria ambayo imepitia hatua zote zinazohitajika na kufanyiwa majaribio, lakini WHO inasema chanjo ya pili ya malaria "inaweza kuwa na faida kubwa kwa udhibiti wa malaria" kwani itasaidia kukidhi mahitaji makubwa yanayotarajiwa.