Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Green Card : Fahamu njia saba maarufu zinazoweza kutumika kupata uraia wa Marekani
Marekani ni miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa duniani na maisha ya hali ya juu kutokana na uchumi wake unaokadiriwa kufikia dola trilioni 22.785 kwa mwaka 2021.
Uchumi wake mkubwa unatoa fursa nyingi za ajira na shughuli za kiuchumi kiasi cha kuvutia mamilioni ya raia wa kigeni wanaokimbilia nchini humo kwa ajili ya kutafuta maisha mazuri.
Raia hao hukimbilia huko kama wakimbizi, wanafunzi, watalii ama wafanyabiashara lakini wengi wao baada ya kufika huko hutafuta fursa ya kuendesha shughuli zao kwa sifa kama za raia wa nchi hiyo.
Ili kukuwezesha kupata sifa hiyo ya kufanya kazi na kuishi kama raia wa Marekani, kadi ya kijani (Green card) ama kitambulisho cha mkazi ni moja ya njia maarufu zaidi inayotumika na raia wengi hasa kutoka Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti rasmi, mpaka mwaka 2019, kulikuwa na watu milioni 13.9 kutoka mataifa mbalimbali wenye kadi hizo, kati yao milioni 9.1 wanasifa ya kuwa raia wa Marekani.
Kadi ya Kijani ni nini hasa?
Green card ama kadi ya kijani kwa kiswahili kisicho rasmi ni kadi ama Kibali maalumu cha kuwa mkazi wa kudumu wa Marekani ama kibali cha kukuwezesha kuishi na kufanya kazi sehemu yoyote ndani ya Marekani kwa muda na wakati wowote kama raia wa nchi hiyo. Kwa kifupi ni kuipata kadi hii lazima uanze kwa kuwa na viza.
Kibali hiki kinatolewa kwa watu wasio raia wa Marekani baada ya kutimiza taratibu na kupata sifa zinazopaswa.
Neno Green Card' linatumika zaidi Marekani labda kwa kuwa kadi hiyo ina rangi ya kijani, kwa nchi nyingine kibali hicho wanaita kitambulisho cha mkazi. Kwa mfano Ujerumani wanaita Aufenthaltgenehmigung'.
Mmoja wa aliyeata kibali hicho anasema' ukikamilisha taratibu zao na kuhojiwa wakijiridhisha wanakupa kibali cha miaka miwili kwanza, wanakuangalia kama hujavunja sheria wanakuongeza mpaka miaka 10', alisema.
Kadi ama kibali hiki cha kisasa kabisa kinachotolewa na Marekani kinakuwa na vitu muhimu kama Majina, aina ya kibali hivyo, tarehe ya kuzaliwa, nchi uliozaliwa, jinsia yako, picha na alama za vidole. Inafanana tu kimuundo kama kitambulisho cha taifa, ama kadi za benki zenye taarifa muhimu za mtumiaji.
Inapatikanaje kadi hii na je ni rahisi kuipata?
Kwa mujibu wa baadhi ya raia wa kigeni waliopata kadi hiyo wanasema unaweza kuipata kwa jasho kiasi, sio rahisi kama ambavyo wengi wanadhania.
"Imenichukua miaka 15 kujaribu kuwa raia wa Marekani, kupitia Kadi hii. Lakini nimeshindwa', anasema Yarzidu, sio jina lake halisi raia wa Palestina.
Zipo njia saba maarufu zinazoweza kukuwezesha kupata Kadi hii.
Ya kwanza kubwa na inayotumika sana hutolewa kwa familia, kwa maana ya kwamba ukioa ama kuolewa na raia wa Marekani unapewa kibali hiki, na inaweza kukuchukua mpaka mwaka kukipata.
'Nililazimika kutafuta mwanamke na kuoa, nikiacha mwanamke wangu nyumbani (Tanzania), nikajifanya sijaoa, nikafanikiwa kupata, yote ni kutafuta maisha, anasema Omary (sio jina lake halisi), aliyepata kadi hiyo mwaka jana.
'Nililipa dola 1,800 za serikali kujaza nyaraka tatu muhimu, kibali cha kuishi, kibali cha kufanya kazi na kibali cha kusafiri, nikamlipa mwanasheria dola karibu 3,000 kunifanyia kazi zote', alisema na kuongeza ' ilinigharimu dola 9,000 karibu mpaka Napata kibali ingawa wengine inaweza kugharimu mpaka dola 20,000, inategemea na hali yako na njia zako', alisema.
Njia ya pili ni kwa kuwekeza kibiashara nchini humo kupitia mtaji wa angalau dola nusu milioni mtaji ambao baada ya mwaka mmoja unaweza kufikia dola 900,000.
Pia unaweza kupata kibali hiki kama umeenda kufanya kazi nchini humo. Mwajiri wako anapaswa kuwa raia wa Marekani na kampuni yake imefanya kazi kwa angalau mwaka mmoja. Njia hii inaonekana rahisi zaidi na inakimbiliwa zaidi kwa watu wenye fursa ya ajira kwa makampuni ya huko.
Unaweza pia kupata kibali kwa njia ya kusoma au kwa wale ambao ni raia wa kigeni waliopata mafanikio ya kutukuka mfano Drake au Ryan Renolds ambao mafanikio yao yanawapa fursa ya kupata kadi hii kirahisi.
Ukishinda tuzo kubwa kama za Oscar, Grammy, ama Pulitzer kupata kibali hiki ni rahisi zaidi na njia nyingine inayotumika sana ni kupata kupitia bahati nasibu inayoweza kumdondokea mtu yeyote aliyejaza fomu kupitia njia mbalimbali za mitandao na kujaribu bahati yake.
Kwa mwaka, kuna watu zaidi ya 55,000 huomba kadi hii kwa njia ya bahati nasibu.
Yarzidu anasema alienda Marekani kuhudhuria tukio la vijana kupitia program ya YALE. Anasema katika program hiyo, alikuwa anasoma na Barbara Bush, mtutu wa Rais wa zamani wa Marekani, George Bush
Nilitumia miaka minne kusoma na nilifaulu vizuri tu, lakini kupata kibali hicho ilikuwa kazi kweli kweli', alisema.
'Miaka yote hiyo 15 niliishi kihalali na kufuata taratibu zote, nimelipa kodi zote, nimejaza kila karatasi iliyotakiwa lakini sijafanikiwa, nikaambiwa sijakidhi vigezo'.
Kupata ama kutopata kadi hii, haikufanyi usifikirie njia nyingine, wapo raia wengi wa kigeni wanaotumia njia mpaka za panya ili kufanikiwa kupata
'Nilitengeneza ndoa ya uongo na kushtukiwa, ilinisumbua sana na kusota ndani kwa muda mrefu, ukweli najuta nimepoteza muda bure', Alisema Ghebre (sio jina lake) wa Ethiopia