Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mashambulio ya mabomu ya 1998: Al shabaab iliwezaje kushambulia maeneo ya ndani ya afrika mashariki?
Miaka 23 iliyopita mwezi kama huu tarehe saba ,mashambulizi mawili ya kigaidi yaliotekelezwa kwa wakati mmoja yaliikumba miji ya Nairobi, Kenya na Dar es Salaam Tanzania.
Mashambulizi hayo ya Agosti mwaka wa 1998, yalibadilisha kabisa hali ya usalama wa kanda hii na kuzitosa nchi hizo katika kampeni iliyojulikana kama 'vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi'.
Wiki hii tunakuletea Makala maalum kuhusu mashambulizi hayo ,wahusika wakuu na matokeo ya kampeni ya vita dhidi ya ugaidi na athari zake kwa nchi za Kenya, Tanzania , Uganda na kanda nzima.
Leo tunaangazia jinsi kundi la kigaidi la Al shabaab lilivyogeuza Kenya nan chi za kanda hii kuwa 'uwanja' wa kufanyia mashambulizi .
Ilipobainika wazi kwamba nchi za Afrika mashariki zilikuwa mstari wa mbele katika kuwa walengwa kwenye mashambulio ya kigaidi ,ililazimu kuwepo kwa aina fulani ya ushirikiano wa kiuslama .
Hata hivyo ushirikiano huo haukuwa wa kisawa sawa na uliunda mianya iliyotumiwa na kundi la al shabaab kuendeleza msururu wa mashambulio ndani ya Kenya na hata Uganda .
Kenya ilijipata kuwa mwathiriwa wa kila mara wa mashambulio ya kundi hilo lakini hilo halikuzipa nchi jirani afueni kwani Julai tarehe 11 mwaka wa 210 kundi hilo lilitekeleza shambulio dhidi ya Uganda mjini Kampala na kusababisha vifo vya watu 74. Uganda ilikuwa imeonyesha nia na hata kuanza kutuma vikosi vya kupambana na kundi hilo na iliendelea kulengwa hata ikiwa na Amisom nchini Somalia .
Unaweza pia kusoma
- 'Tufanye nini?' Kenya na Tanzania katika njia panda baada ya mashambulio ya 1998
- Je, Kenya imelipia gharama ya juu kujiingiza katika vita dhidi ya ugaidi?
- Tanzania na Kenya zilifanya nini kulengwa na magaidi hawa watatu mwaka wa 1998?
- Je, Kenya iliyapa ‘zawadi’ makundi ya kigaidi kupitia mbinu zake dhidi ya ugaidi?
Ushirikiano wa karibu ulihitajika na ulipofuatiwa na sheria za kupambana na ugaidi ,nchi za Afrika mashariki zilionekana kuwa na mkakati mmoja wa kupambana na tishio la kigaidi .
Mashambulizi ya Al shabaab nchini Kenya yalizidi wakati Kenya ilipoyatuma majeshi yake Somalia mwaka wa 2011. Kufikia mwaka wa 2012 Kenya ilikuwa imesaidia kulifukuza kundi hilo katika mji wa bandari muhimu wa Kismayu.Tangu wakati huo ilikuwa wazi kwa wadadisi kwamba wajibu wa Kenya katika kulifukuza al shabaab Kismayu sio jambo litakalopokelewa vyema na magaidi hao .
Shambulio la westagate
Mnamo Septemba tarehe 21 mwaka wa 2013 al shabaab ilitekeleza shambulio dhidi ya duka la Westgate. Shambulio hilo lilikuwa la kushtukiza na liliziacha idara za usalama nchini vinywa wazi kwani miaka michache iliyopita haingedhaniwa kwamba kundi hilo lilikuwa na uwezo wa kupanga na kutekeleza shambulio hatari kama hilo katikati ya ngome ya Kenya kama Westgate .
Watu 67 waliuawa na ujumbe ulikuwa ushawafikia walengwa. Al shabaab ilikuwa na nia ya kuwatia hofu wakenya hasa wa kiwango cha kipato cha kadri ambao hapo awali walifikiri wapo nje ya hatari ya kiusalama kwa tishio la ugaidi .
Tanzania yafunga kambi ya mafunzo ya itikadi kali
Tanzania kwa upande wake haikuathiriwa sana na mashambulio kama Kenya lakini iliendelea kuwa macho na kuchunguza kwa karibu matukio yaliyotishia usalama wake.
Mnamo Novemba 2017 katika mji wa Tanga ,mamlaka ziliwakamata watu 69 waliokuwa wakiendesha kituo cha kuwapa watoto mafunzo ya itikadi kali za kidini .Watu 50 waliokuwa na umri wa kati ya miaka minne na 13 walinaswa .
Tishio la kuzua mgawanyiko wa kidini
Hatua ya kwanza iliyoonyesha kutoelewa jinsi magaidi walivyokuwa wakifikiria ni serikali ya Kenya kuonekana kulichukulia tisho la ugaidi kama suala la jamii ama dini Fulani .
Mnamo Aprili 2014 polisi walianza kuwakamata na kuwazuilia watu wa jamii ya Wasomali .Hatua hiyo ilizidisha 'maonevu' ambayo tayari jamii hiyo ilikuwa ikihisi kwa muda mrefu ikizingatiwa kwamba kwa miaka mingi imekuwa ikiteta kuchukuliwa kama sehemu ya kando ya taifa la Kenya .
Lilikuwa jambo hatari kwani Iwapo serikali ingetaka suluhisho la kudumu kwa tishio la ugaidi ,jamii hiyo ingekuwa mstari wa mbele kufanikisha ushirikiano wa kupata Habari na kufahamu kiini cha wengi waliokuwa wakijiunga na makundi ya kigaidi . Baadaye Kenya kuonekana kuelewa hali ilivyokuwa ,hilo lilikoma na mikakati mbadala iliyokuwa na ufanisi ikaanza kutumiwa .
Shambulio la chuo kikuu cha Garissa
Mnamo Aprili tarehe 2 mwaka wa 2015 Al shabaab ilitekeleza shambulio jingine katika chuo kikuu cha Garissa kaskazini mwa Kenya na kuwaua watu 148, wengi wao wakiwa wanafunzi.
Lalama za wananchi ziliifanya serikali kuwabadilisha maafisa wa usalama na kuanza kufanya vikao na makundi ya vijana ili kuboresha ukusanyaji wa habari za kijasusi za kufanikisha majibu ya tishio la ugaidi mashambulizi katika maeneo ya miji yalianza kupungua baada ya hapo .
Miaka miwili baadaye mwaka wa 2017 Tanzania ikawa mwathiriwa wa shambulio la kigaidi wakati wapiganaji wa kigaidi walipowaua maafisa wanane wa polisi katika eneo la Kibiti pwani mwa Tanzania.
Oparesheni za usalama nchini Kenya zinawalazimisha wapiganaji wa Al shabaab kubadilsha makao na kuamia kwingine .Wapiganaji wake wanafanya ushirikiano na makundi ya kijihadi nchini Tanzania na kaskazini mwa Msumbuji .
Huku nchini jirani za Somalia zikijizatiti kuepuka mashambulio ,Somalia yenyewe ilikumbwa na shambulio kubwa zaidi Oktoba tarehe 7 mwaka wa 2017 wakati watu 587 walipouawa katika mlipuko wa bomu mjini Mogadishu .
Katikati ya mwezi Januari mwaka wa 2019 ,Al shabab ilirejea na kushambulia jengo la hoteli la Dusit mjini Nairobi. lilikuwa kumbusho kwamba hatari haikuwa imepungua na serikali ililazimika kuzidisha uangalifu wake .
Kupitia ushirikiano na msaada wa Marekani nchi jirani hizi za Afrika mashariki zimekuwa zikifanya oparesheni za pamoja na wakati mwingine kupigwa jeki na mashambulio ya angani ya Marekani kupambana na kundi la Al shabaab .
Mnamo mwaka wa 2019 januri, Al shabaab ilishambuliwa na ndege za Marekani na wapiganaji wake zaidi ya 50 kuuawa katika shambulizi moja .
Marekani imekuwa ikiendelea kufanya oparesheni kama hizo kwa lengo la kuhakikisha kwamba kundi hilo halipati nafasi ya kupata nguvu zaidi kutishia usalama wa kanda hii .