Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mashambulio ya mabomu ya 1998: Kenya imelipia gharama ya juu ya maisha katika vita dhidi ya Ugaidi?
Miaka 23 iliyopita mwezi kama huu tarehe saba ,mashambulizi mawili ya kigaidi yaliotekelezwa kwa wakati mmoja yaliikumba miji ya Nairobi, Kenya na Dar Es Salaam Tanzania.
Mashambulizi hayo ya Agosti mwaka wa 1998, yalibadilisha kabisa hali ya usalama wa kanda hii na kuzitosa nchi hizo katika kampeni iliyojulikana kama 'vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi'.
Wiki hii tunakuletea Makala maalum kuhusu mashambulizi hayo ,wahusika wakuu na matokeo ya kampeni ya vita dhidi ya ugaidi na athari zake kwa nchi za Kenya, Tanzania , Uganda na kanda nzima. Leo tunaangazia jinsi Kenya ,ilivyojipata ndani ya vita vya Somalia katika muendelezo wa mapambano yake dhidi ya ugaidi na gharama kubwa ya kuendeleza vita hivyo hadi ilipojiunga na Amisom .
Mnamo mwaka wa 2011 Kenya iliamua kuyatuma majeshi yake nchini Somalia katika oparesheni iliyopewa jina 'Linda Nchi'.
Lengo lake lilikuwa kukabiliana na kuliangamiza kundi la Al shabaab
Kundi hilo lilikuwa limetekeleza msururu wa mashambulizi katika mpaka wa Kenya na Somalia na hata ndani ya nchi huku milipuko ya mara kwa mara ikiwatia hofu Wakenya wengi .
Ingawaje mwaka mmoja baadaye Kenya ilisema oparesheni hiyo imekamilika na majeshi yake kujiunga na Amisom Machi mwaka wa 2012-Ilikuwa wazi kwamba makabiliano hayo dhidi ya Al shabaab nje ya nchi yalikuwa ni harakati zake za kupambana na ugaidi .
Lakini matokeo yake hadi leo bado yanajadiliwa ikizingatiwa kwamba matukio mengi ya wakati huo na baadaye yalisabbisha maafa kupitia mashambulizi ya Al shabaab na gharama kubwa ya vita hivyo kwa serikali .
Iwapo kuna tukio katika kampeini ya vita vya Kenya dhidi ya ugaidi ambavyo vinaweza kutoa taswira ya gharama ya hatua hiyo basi ni shambulizi baya sana ambalo Al shabaab ilitekeleza dhidi ya Kambi ya wanajeshi wa Amisom iliyokuwa na wanajeshi wa Kenya mwaka wa 2016 .
Shambulizi hilo lilikuwa katika eneo la El Ade.
Hakuna idadi kamili ama rasmi iliyowahi kutolewa ya wanajeshi waliouwa katika shambulio hilo lakini inakadiriwa kwamba zaidi ya 100 waliangamia.
Lilikuwa ndilo shambilio baya zaidi dhidi ya Kenya kuwahi kutokea tangu ijitose katika mapambano dhidi ya ugaidi .
Kilichotokea El Ade
Ilikuwa tarehe 15 Januari mwaka wa 2016 wakati wanamgambo wa Al shabaab walipoishambulia kambi ya wanajeshi wa Kenya katika mji wa El Ade
Wakazi wa mji wa kusini-magharibi wa El-Ade walikuwa wa kwanza kutoa habari, wakisema wapiganaji wa al-Shabab walifika alfajiri.
Uvamizi huo ulianza na mlipuko wa mlipuaji wa gari la kujitoa muhanga kwenye milango ya kituo hicho na baada ya hapo watu kadhaa wenye bunduki walijitokeza wakifyatua risasi .
Mashuhuda wa tukio hilo walisema makumi ya wanajeshi wa Kenya waliuawa wakati wengine walikimbilia porini.
Lakini hii haikuwa simulizi iliyotolewa na jeshi la Kenya kuhusu kilichofanyika .
Makao hayo yaliyoko pembezoni mwa mji yalikuwa na kambi mbili za jeshi - moja ikiwa na jeshi la kitaifa la Somalia na jingine ya kikosi cha wanajeshi wa Kenya.
Saa chache baada ya shambulio hilo kuanza, kanali David Obonyo, msemaji wa kikosi cha ulinzi cha Kenya wakati huo , alisisitiza ni kambi ya Somalia ambayo ilikuwa imevamiwa - na kwamba wanajeshi wa Kenya walikuwa wamekimbia kuwaokoa wenzao wa Somalia
Hata hivyo, afisa mmoja wa serikali ya Somalia alikana hilo na wakati huo kuiambia BBC kwamba kwa kweli ilikuwa sehemu ya kambi ya Kenya ambayo ilivamiwa.
Maafa yaliyofuatia ya wanajeshi wa Kenya sio jambo zuri la kuwakumbusha watu lakini ilikuwa bayana kwamba vita dhidi ya ugaidi vilikuwa kweli vimeanza kulipiwa kwa gharam ya juu ya-maisha .
Wengi wakati huo pamoja na hasa familia zilizoathiriwa na vifo vya jamaa zao walianza kuhoji Iwapo ilistahili kwa Kenya kuendelea na oparesheni nchini Somalia .
Serikali na jeshi zilisalia kimya huku taarifa za kilichofanyika zikipepezewa chini na hakuna aliyetoka na ukweli wa kuaminiwa na Wakenya .
Misheni iliyodhaniwa haitakuwa na makali kama haya na picha za kuogopfya za miili ya wanajeshi wa Kenya na zana zake za kivita zikichomwa ni taswira ambayo iliwarejesha nyuma wengi katika kumbukumbu zao.
Kenya ilikuwa imejiingiza kwa yapi?
Hali ilikuwa kama ile ya miaka ya 1980 wakati makundi ya wapiganaji wa kijihadi nchini Afghanistan yalivyowafurusha Wasovieti au tukio la miaka ya 90 wakati Marekani ilipojipata tabaani kupambana na makundi ya wapiganaji nchini Somalia baada ya kuanguka kwa utawala wa Siad Barre .
Lakini Kenya haikufa moyo -Vita dhidi ya ugaidi na hasa kundi la Al shabaab viliendelea.
Kwa msimamo wa Kenya ,imefaulu kupunguza nguvu za Al shabaab lakini matukio ya hapa na pale ya mashambulizi katika mji wake mkuu Nairobi yalifuatia baadaye.
Hasara na maafa na hofu iliyoambatana na mashambulio hayo yote kwa jumla yalisalia kuwa gharama kubwa ya kulipia katika vita vyake .
Mikakati ya kisasa na ya kudumu
Kando na kinachoendelea Somalia na kushindwa kuangamizwa kabisa kwa kundi la Al shabaab ,Kenya ilizidi kutenga raslimali nyingi na kutumia teknolojia kuanza kujikinga dhidi ya vitisho vya kigaidi .
Uwekezaji katika sekta ya Ulinzi umedhihirisha kujitolea sio tu kwa Kenya bali nchi nyingine za kanda hii kupambana na tishio la ugaidi .
Gharama hiyo ya wasi wasi na hofu ya tishio usiloliona itasalia kuwepo ikizingatiwa pia kwamba mkakati wa awali wa Kenya kuhakikisha kuna serikali dhabiti ya Somalia ili kuweza kuliangamiza kabisa Al shabaab na kuhakikisha usalama wa kudumu haujafaulu.
Kenya imejipata kwenye mgogoro wa kidiplomasia na Somalia hatua ambayo sasa inalemaza uwezo wa nchoi zote mbili kuwa na mpango wa pamoja na wa muda mrefu wa kukabiliana na tishio la Al shabaab .
Kwa Kenya ,kujikinga dhidi ya tishio la ugaidi litasalia jambo la kila siku kwa siku nyingi zijazo .
Hapatakuwa na kipindi ambapo asasi zake za usalama zitalegeza kamba Iwapo utulivu ambao umeshuhudiwa kwa miaka ya hivi karibuni utadumishwa endapo uangalifu , tahadhari na mbinu za kuzuia vitaachwa .