Mwanafunzi ashtuka kwa kuuona mwili wa rafiki yake katika darasa la utafiti wa miili ya binadamu Nigeria

Katika msururu wetu wa barua kwa waandishi wa Afrika , mwandishi wa Nigeria Adaobi Tricia Nwauubani anaandika kuhusu ukweli wa miili iliokosa kuuliziwa inayotumwa katika shule za mafunzo ya matibabu.

Mwanafunzi anayesomea somo la matibabu Enya Egbe aliondoka katika darasa lake la utafiti wa mwili wa binadamu baada ya kusumbuliwa na mwili aliokuwa akiufanyia kazi.

Hili halikuwa tukio la kawaida kwa kijana aliyekosa uzoefu wa mambo kama hayo.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 26 bado anakumbuka siku ya Alhamisi jioni miaka 7 iliopita akiwa katika chuo kikuu cha Calabar nchini Nigeria , akikongamana na wanafunzi wenzake katika meza tatu ambazo zilikuwa na wafu waliokuwa wamelazwa katika kila meza.

Dakika chache baadaye, alipigia kelele na kutoroka. Mwili ambao wenzake walikuwa wanakaribia kuupasua ulikuwa ule wa Devine, rafiki yake wa miaka saba.

''Tulikuwa tukienda katika klabu za burudani pamoja aliniambia. ''

''Alikuwa na mashimo mawili yaliokuwa ni majeraha ya risasi katika upande wa kulia wa kifu chake''.

Oyifo Ana ni miongoni mwa wanafunzi ambaye pia alitoka nje alipomuona bwana Egbe akilia.

''Miili ya wafu wengi tuliokuwa tukitumia shule ilikuwa na majeraha ya risasi , nilihisi vibaya wakati nilipogundua kwamba baadhi ya watu huenda sio wahalifu'', bi Ana alisema.

Aliongezea kwamba siku moja mapema aliona gari la maafisa wa polisi likiwa limejaa miili katika shule yao , ambayo ilikuwa na chumba cha kuhifadhia maiti.

Bwana Egbe alituma ujumbe kwa família ya Divine ambayo ilibainika kwamba imekuwa ikimtafuta mwanao katika vituo tofauti vya polisi baada ya yeye na marafiki zake watatu kukamatwa na maafisa wa usalama walipokuwa wakitoka katika klabu za burudani.

Familia yake baadaye ilifanikiwa kuupata mwili wake.

Ugunduzi wa kushangaza wa bwana Egbe uliangazia ukosefu wa wafu nchini Nigeria ili kutumika katika masomo ya wanafunzi wanaosomea matibabu na kile kinachoweza kuwafanyikia waathiriwa wa ghasia zinazotekelezwa na polisi.

Kati ya karne ya 16 na karne ya 19, sheria tofauti nchini Uingereza ziliruhusu miili ya wahalifu waliouawa kutumika katika shule za matibabu.

Nchini Nigeria , sheria za sasa zinasema kwamba miili ambayo imekosa wenyewe katika vyumba vya kuhifadhia maiti vya serikali inapaswa kupelekwa katika vyuo vya kusomea matibabu.

Serikali pia inaweza kutumia miili ya wahalifu walionyongwa , lakini tukio la mwisho la mtu kunyongwa lilifanyika 2007.

Zaidi ya asilimia 90 ya wafu wanaotumika katika shule nchini Nigeria ni wahalifu waliouawa kwa kupigwa risasi , kulingana na utafiti wa 2011 katika jarida la matibabu kwa jina Clinical Anatomy.

Ukweli ni kwamba , hii ina maana kwamba ni washukiwa waliopigwa risasi na vyombo vya usalama. Umri wao ni kati ya miaka 20 hadi 40, ikiwa asimilia 95 ni wanaume , huku watatu kati ya wanne wakiwa watu wanaotoka katika jamii maskini.

''Hakuna lililobadilika miaka 10 baadaye'', alisema Emeka Anyanwu, profesa wa elimu ya miili ya binadamu katika chuo kikuu cha Nigeria ambaye pia ni mmoja wa waazilishi wa utafiti huo.

'Jukumu la ambyulensi'

Mwaka uliopita , serikali ya Nigeria ilibuni majopo ya mahakama katika majimbo tofauti ili kuchunguza madai ya unyanyasaji wa polisi.

Hii ilikuwa kujibu maandamano ya #EndSars yaliosababishwa na kusambaa kwa kanda ya video ya kijana mmoja aliyepigwa risasi na kitengo maalum kinachopgana dhidi ya wahalifu SARS katika jimbo la kusini la Delta.

Wengi ya wale waliokuwa wakitoa ushahidi wao mbele ya jopo hilo wamezungumzia kuhusu wapendwa wao kukamatwa na maafisa wa usalama na kutoweka.

Maafisa wa usalama katika visa vingi wanajitetea kwa kusema kwamba wale waliopotea walikuwa wahalifu waliojihami waliouawa wakati wa ufyatulianaji risasi , huku msemaji wa polisi Frank Mba alinimbia kwamba hana ufahamu wa tukio lolote ambapo polisi walipeleka miili katika maabara za shule za matibabu ama vyomba vya kuhifadhia maiti.

Katika ushahidi ulioandikwa na kuwasilishwa kwa jopo hilo la mahakama katika jimbo la Enugu, Cheta Nnamani alisema kwamba aliwasaidia maafisa wa usalama kuondoa miili ya wale iliowatesa au kuwauwa wakati alipokamatwa na kuzuiliwa kwa miezi minne na SARS 2009.

Alisema kwamba , usiku mmoja , alitakiwa kubeba miili mitatu hadi katika gari moja , jukumu linalojulikana katika kizuizi kama 'kazi ya ambyulensi'.

Baadaye maafisa wa polisi walimfunga kwa kutumia seng'enge ndani ya gari hilo na kulipeleka hadi katika chuo kikuu kilichopo karibu cha Nigeria Teaching and Hospital UNTH , ambapo bwana Nnamani alitakiwa kushusha miili hiyo .

Ilichukuliwa na kuingizwa ndani na mhudumu wa vyumba vya kuhifadhia maiti.

Bwana Nnamani baadaye aliniambia kwamba alitishiwa kuuawa.

Katika mji wa kusini wa Owerri, chumba cha kuhifadhi maiti cha kibinafsi cha Hospitali ya Aladinma kilikataa kuchukua miili ya washukiwa wa uhalifu kwasababu maafisa wa polisi hawakutoa vitambulisho vyao ama hata kuwajulisha wapendwa wao kuhusu marehemu hao.

Wapendwao wa hawana habari zozote kuwahusu

Wakili mmoja mwandamizi, Fred Onuobia, anasema kwamba watu wa familia zao walipaswa kuja kuchukua miili ya watu walionyongwa kisheria.

''Iwapo hakuna mtu anayejitokeza baada ya muda Fulani , miili hiyo hupelekwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti katika hospitali zinazotoa mafunzo ya matibabu'', alisema wakili huyo.

Lakini hali hiyo imekuwa mbaya zaidi huku kukiwa na mauaji ya kukusudia bila kufuata sheria , kwasababu wapendwa wao hawawezi kuelezewa kuhusu sababu ya kifo chao ama hata hawawezi kupata miili ya wapendwa wao.

Ilikuwa bahati kwamba familia ya rafikiye Egbe , Divine iliweza kumpatia maziko ya heshima .

Muungano wa madaktari wa kuchunguza miili ya wanadamu kwasasa unapigania sheria kubadilishwa ili kuhakikisha vyumba vya kuhifadhia maiti vinapata rekodi zote za kihistoria za miili inayopeanwa katika shule hizo mbali na kupatiwa ruhusa na familia.

Pia inataka kuanzisha mpango wa watu kupeana miili yao kwa shule hizo.

Hatahivyo kwa bwana Egbe , aliumizwa sana kwa kuona mwili wa rafiki yake na kulazimika kuwacha masomo kwa wiki kadhaa , kwasababu alikuwa akimuona Divine amesimama katika mlango wa chuo hicho kila mara alipokuwa akitaka kuingia katika chumba hicho cha utafiti wa miili ya binadamu.

Alilazimika kufuzu mwaka mmoja baada ya wanafunzi wenzake , na sasa anafanya kazi katika maabara moja ya hospitali katika jimbo la Delta.

Familia ya Divine ilifanikiwa kuwatambua maafisa waliohusika na mauaji yake na kuhakikisha kwamba wamefutwa kazi .