Onyo: China yasema iko tayari kwa lolote kuzuia uchokozi wa Uingereza baharini

Chanzo cha picha, Getty Images
Uchina imeionya Uingereza kuhusu kundi la meli zake za kivita zinazokaribia katika bahari ya Kusini mwa China dhidi ya "vitendo vyovyote visivyofaa " wakati inaingia katika eneo hilo linalozozaniwa .
Msafara wa meli hizo unaongozwa na meli ya kubeba ndege za kivita ya HMS Queen Elizabeth.
'Jeshi la Wanamaji la Ukombozi wa Watu liko katika hali ya juu ya utayari wa mapigano' linasema jarida la Global Times, linaloonekana kutumiwa kutoa kauli za Chama tawala cha Kikomunisti cha China (CCP).
China imekuwa ikifuatilia kwa karibu kinachofanyika katika safari ya msafara huo unaelekea upande wa mashariki kwenda Japan.
Nchi hiyo imeishtumu Uingereza kwa kuendelea kuishi katika 'siku zake za ukoloni".
Jeshi la Wanamaji la Uingereza limekuwa likifanya mazoezi na jeshi la wanamaji la Singapore na Katibu wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace ameonyesha wazi nia ya kuenelea kufanya mazoezi ya "Uhuru wa kusafiri baharini " kupitia Bahari ya Kusini mwa China.
Kinyume na uamuzi wa korti ya kimataifa ya 2016, China inadai sehemu kubwa ya bahari hiyo kuwa yake na imekuwa ikijishughulisha na kujenga visiwa bandia na njia za kuwezesha ndege kupa , zingine zikiwa karibu na maji ya eneo la nchi jirani.
Meli za kivita za Marekani na Uingereza zimepinga madai ya Uchina juu ya kumiliki Bahari ya Kusini mwa China kwa kuipitia katika bahari hiyo kwa makusudi.

Chanzo cha picha, PA Media
Kwa hivyo swali sasa ni: je! Tutaona makabiliano ya karibu karibu sawa na yale yaliyofanyika katika Bahari Nyeusi mnamo Juni wakati meli ya Defender HMS ya Uingereza, ilitishiwa na ndege za kivita za Urusi wakati ilipopita karibu na peninsula ya Crimea ?
"China haitafuti makabiliano ya moja kwa moja na mshirika mkubwa wa Marekani katika Bahari ya Kusini mwa China" anasema Veerle Nouwens, mtafiti mwandamizi katika Kituo cha Huduma cha Royal United (Rusi), "Lakini hakika itaweka nia yake wazi."
Ikiwa Uingereza inafanya mazoezi ya uhuru wa kupitia bahari hiyo, basi Bi Nouwens anaamini tuna uwezekano wa kuona kurudiwa kwa kile kilichotokea wakati HMS Albion ilipitia mwaka 2018. Ilifuatwa kwa karibu na meli ya kivita ya Wachina kutoka mita 200m tu, ikionywa ili kuondoka, wakati ndege za Wachina zilipaa chini juu ya meli ya Uingereza
Uchina imekuwa ikifanya mazoezi mengi ya kijeshi katika eneo hilo wiki hii, ikifanya mazoezi ya shambulio la pwani katika hatua ambayo imekuwa na wasiwasi kwa wachambuzi wengine kwamba inajiandaa kuvamia Taiwan.
Jeshi la Wanamaji la PLA litatumia uwepo wa meli za Uingereza katika Bahari ya Kusini mwa China "kama nafasi ya kufanya mazoezi na kusoma meli za kivita za Uingereza karibu", inasema Global Times.
Inanukuu msemaji wa ubalozi wa China huko London akisema: "Tishio kwa uhuru wa kutumia bahari linaweza pia kutoka kwa yule anayepeleka kikundi cha meli za kivita Kusini mwa China umbali wa nusu ya ulimwengu na kuonyesha misuli yake ya ubabe wa majini ili kuongeza taharuki katika eneo hilo. "

Chanzo cha picha, AFP
Lakini wakati kuwasili kwa Kikundi kikundi cha meli hizo kusini mwa bahari ya China kumezua maneno ya hasira kutoka Beijing, Mtafiti wa Rusi Sidharth Kaushal, anasema kwamba linapokuja suala la utata wa majini , "vitendo vya China vimekadiriwa kuwa viko chini sana na huenda pasiwe na hatari ya kufyatuliana risasi'
Kupelekwa kwa meli ya kivita ya HMS Queen Elizabeth kwenda Asia ya Mashariki kunaonekana kama sehemu ya azma ya serikali ya Uingereza ya kuchukua jukumu muhimu zaidi katika usalama wa ulimwengu, kama ilivyoainishwa katika mkakati uliotathminiwa hivi karibuni na serikali.
Ufaransa, pia, pamoja na mataifa mengine ya Ulaya, imekuwa ikiangalia hali katika Bahari ya Kusini mwa China wakati nguvu inayoongezeka ya jeshi na uchumi wa China inaonekana kuwa haiwezi kuzuiwa.
China hivi karibuni imeanza kuboresha silaha zake za kinyuklia na kujenga maghala mapya ya kuzindua makombora ya masafa ya mbali huko Xinjiang. Imekuwa pia ikitengeneza Magari ya Hypersonic Glide, makombora yenye kasi kubwa ambayo yanaweza kufikia kasi ya mara nane ya kasi ya sauti.














