China:Jeshi la China lasema 'limeifukuza' meli ya kijeshi ya Marekani kutoka bahari ya Kusini mwa China

Chanzo cha picha, US NAVY
Jeshi la China limesema "limeifukuza" meli ya kivita ya Marekani ambayo lilisema iliingia kinyume cha sheria katika Eneo la bahari ya China karibu na Visiwa vya Paracel vyenye mgogoro Jumatatu, wakati wa kumbukumbu ya uamuzi wa kihistoria wa mahakama ya kimataifa kwamba Beijing haina madai juu ya Bahari ya Kusini mwa China.
USS Benfold iliingia kwenye maji ya Paracels bila idhini ya serikali ya China, ikikiuka sana uhuru wa China na kutishia hali ya utulivu wa Bahari ya Kusini mwa China, Kikosi cha Kusini mwa Jeshi la Wananchi kilisema.
"Tunaihimiza Marekani kuacha mara moja vitendo vya uchokozi," Kitengo hicho cha jeshi kimesema kupitia taarifa
Katika taarifa, Kikosi cha 7 cha Jeshi la Wanamaji la Marekani kimesema Benfold "Imeshikilia haki na uhuru wa kusafiri karibu na Visiwa vya Paracel, kwa mujibu wa sheria za kimataifa" na ikatupilia mbali madai ya Wachina ya ukiukaji mkubwa wa kuingia katika eneo lake kama "ya uwongo" na upotoshaji.
Ilisisitiza kwamba meli zote zina haki ya "kupita bila hatia" chini ya sheria za kimataifa kama inavyoonekana katika Mkataba wa Sheria ya Bahari na idhini haihitajiki.
"Operesheni hiyo inaonyesha dhamira yetu ya kudumisha uhuru wa kusafiri na matumizi halali ya bahari," ilisema taarifa hiyo. "Marekani itaendelea kusafiri, na kufanya kazi popote sheria ya kimataifa inaporuhusu, kama USS Benfold ilivyofanya hapa. Hakuna chochote PRC (Jamhuri ya Watu wa China) inasema vinginevyo kitatuzuia. "
Paracels, inayoitwa Xisha nchini China, ni miongoni mwa mamia ya visiwa, vya bahari ya Kusini yenye utajiri wa rasilimali inayoshindaniwa na China, Vietnam, Taiwan, Ufilipino, Malaysia na Brunei, huku Beijing ikidai haki za kihistoria kwa kila kitu ndani ya eneo hilo.
China ilichukua udhibiti wa Paracels, msururu wa visiwa karibu maili 250 (kilomita 400 mashariki mwa Vietnam) na maili 220 (kilomita 350) kusini mashariki mwa Kisiwa cha Hainan, mnamo miaka ya 1970. vinadaiwa pia na Vietnam, ambayo inaviita Hoang Sa, na vile vile Taiwan. Nchi zote tatu zinahitaji ruhusa au arifa ya mapema kabla ya meli yoyote ya kijeshi kusafiri kupitia eneo hilo, Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema.

Chanzo cha picha, Reuters
Mnamo Julai 12, 2016, Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi huko The Hague ilikataa laini ya Uchina kusema inamiliki vsiwa hivyo na kuamuru kwamba Beijing haikuwa na haki ya kihistoria juu ya Bahari ya Kusini mwa China.
Pia ilisema Uchina iliingilia haki za jadi za uvuvi za Ufilipino huko Scarborough Shoal na kukiuka haki za Ufilipino kwa kutafuta mafuta na gesi karibu na Reed Bank
China imesema mara kwa mara kwamba haikubali uamuzi huo na imeendelea kupanua uwepo wake katika eneo la Bahari ya Kusini mwa China katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Katika taarifa iliyotumwa mwishoni mwa wiki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema uhuru wa bahari ni nia ya "kudumu" ya mataifa yote.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Hakuna mahali ambapo sheria za baharini zipo chini ya vitisho vikubwa kuliko katika Bahari ya Kusini mwa China," Blinken alisema.
"Jamhuri ya Watu wa China inaendelea kulazimisha na kutisha nchi za pwani ya Asia ya Kusini, ikitishia uhuru wa kusafiri katika njia hii muhimu ya ulimwengu."
Alirudia onyo kwa China kwamba shambulio dhidi ya vikosi vya jeshi la Ufilipino katika Bahari ya Kusini mwa China litachochea mkataba wa ulinzi wa pande zote wa Marekani na Ufilipino wa 1951.
"Tunaitaka PRC kutii majukumu yake chini ya sheria za kimataifa, iachane na tabia zake za uchokozi, na ichukue hatua za kuihakikishia jamii ya kimataifa kuwa imejitolea kutii shertia za baharini na kuheshimu haki za nchi zote, kubwa na ndogo. "Aliongeza.













