Misikiti 8 ya zamani iliosaidia kusambaza Uislamu yawekwa katika turathi za dunia

Muda wa kusoma: Dakika 2

Misikiti minane nchini Ivory Coast, ambayo inaaminiwa kuwa muundo wake wa ujenzi ulianza wakati wa himaya ya Mali karne kadhaa zilizopita, imepewa hadhi ya kuwa urithi wa dunia na Unesco.

Majengo hayo ni "kielelezo cha ushahidi muhimu wa biashara baina ya maeneo ya sahara " iliyosaidia kueneza Uislamu na utamaduni wa Kiislamu, limesema Shirika hilo la Umoja wa mataifa kuhusu masuala utamaduni.

Umbo la misikiti hiyo ni mchanganyiko wa mitindo ya ujenzi wa misikiti ya Kiislamu na mitindo ya maeneo hayo.

Misikiti hiyo iliyoko katika miji ya Tengréla, Kouto, Sorobango, Samatiguila, M'Bengué, Kong, na Kaouara imehifadhiwa vyema na ni kati ya misikiti 20 mikubwa iliyosalia nchini Ivory Coast, ambako kuna mamia ya misikiti ambayo wakati mmoja ilisimama mwanzoni mwa karne ya 20, kulingana Unesco.

Kulingana na Unesco, walionyesha kielelezo cha usanifu wa majengo yaliyojengwa tangu karne ya 14 katika jiji la Djenné, ambalo ni sehemu ya himaya ya Mali.

Mtindo huo ulisambaa hadi Sudan katika karne ya 16 na kukarabatiwa ili kukabiliana na hali ya hewa ya unyevunyevu.

Misikiti nchini Ivory Coast ina mtindo wa kipekee ambao unadhaniwa kutengenezwa baina ya karne za 17 na 18 wakati wafanyabiashara wa kiislamu na wasomi walipowasili kutoka Himaya ya Mali kusini, wakipanua biashara katika maeneo ya njia ya Sahara.