Binti wa miaka 15 arithi utajiri wa thamani ya zaidi ya dola laki tano

Chanzo cha picha, FINDERS INTERNATIONAL
Binti wa miaka 15 nchini Indonesia anajiandaa kurithi zaidi ya pauni 400,000 baada ya kupatikana kwa aliyeacha mali hiyo na ambaye ametambuliwa kama raia wa uingereza alitefariki dunia Septemba mwaka jana .
Shirika la Finders International, linalomfuatilia mnufaika huyo, liliiambia BBC Indonesia, "mchakato unaofuata ni kuthaminishwa kwa mali na pesa zitatumwa kwa binti wa Muingereza huyo au mwakilishi wake aliyeidhinishwa".
"Mchakato huo kwa sasa uko mikononi mwa wanasheria, na hatujui mchakato huu utachukua muda gani," Finders alisema.
Muingereza, Alexander Thomson, mhariri wa zamani wa BBC World Service ukanda wa Afrika Mashariki na Mashariki ya Mbali, aliaga dunia mwezi Septemba mwaka jana akiwa na umri wa miaka 71, bila kuacha wosia.
Hakuoa, na familia yake ya karibu haijulikani.

Chanzo cha picha, FINDERS INTERNATIONAL
Hii ilisababisha kutafutwa kwa jamaa zake.
Danny Curran, Mkurugenzi wa Finders International, alisema timu yake ilifanikiwa kumpata mtoto anayeaminika kuwa wa wa Thomson
Alisema timu yake ilifanikiwa kugundua kuwa mwandishi wa habari huyo wa zamani alikuwa na watoto nchini Indonesia baada ya kupata picha katika makazi yake huko Ramsgate, kusini mwa England.
BBC Indonesia iliuliza wawakilishi wa watoto wa Thomson, lakini Finders International ilisema: "Hatuwezi kutoa maelezo juu ya binti zao au wawakilishi wao nchini Indonesia."
Msichana huyo, ambaye hakutajwa jina ilibainika kuwa "alikuwa na baba wa Kiingereza kupitia mama yake".
Curran alisema hatua inayofuata ni kwa mtoto kuhitaji kuteua mwakilishi atunze urithi alioupata.
Curran, ambaye amefanya uchunguzi wa mirathi kwa miaka 30 iliyopita, alisema timu yake iliingia nyumbani kwa Thomson ili kuchunguza.

Chanzo cha picha, FINDERS INTERNATIONAL/DAWSONSWNS
"Tulitafiti nyumba hiyo na kusoma habari zote. Tuligundua kuwa ni mhariri wa zamani wa BBC Afrika Mashariki na Mashariki ya Mbali. Tulipata vingi kumhusu nyumbani kwake," Curran aliiambia BBC Radio Kent.
"Tulianza kupata taarifa kumhusu kutoka kwa vitu alivyokuwa navyo na kuanza kuuliza maswali kama ana wapwa ambao wanaweza kurithi."
"Lakini pia tulipata ushahidi wa aina fulani ya sherehe, labda harusi huko Indonesia na kulikuwa na picha za kile kilichoonekana kama Waindonesia.

Chanzo cha picha, FINDERS INTERNATIONAL
"Kwa hivyo hapo ndipo tulipoanza kuchunguza zaidi kujua ikiwa alikuwa na watoto, ambao labda alikuwa hajawaona kwa miaka mingi, lakini ambao bado walikuwa na haki ya kurithi kwa mujibu wa sheria.''
"Tuna mawakala kote ulimwenguni ambao wana uzoefu wa miaka, kwa hivyo tunawasambaza kote na tukagundua alikuwa na mwenzi wa zamani na binti anayeishi huko."
"Kwa hivyo tuliwasiliana nao na kuwaambia ni nini kilitokea kwamba baba wa binti alikuwa amekufa," alisema Curran.

Chanzo cha picha, FINDERS INTERNATIONAL
"Ishara tuliopa ni kwamba, mama amemwambia mtoto wake baba ni Muingereza, na sio mengi zaidi. Na kwa kweli hawakuacha nchi yao, kwa hivyo hatujui ni nini kilitokea."
"Kunaweza kuwa na mipango kwamba mtoto angehamia Uingereza wakati fulani lakini hiyo haionekani kuwa ilitokea. Tunahitaji kuheshimu faragha yao pia lakini angalau tuna wazo la nini kinaendelea."

Chanzo cha picha, FINDERS INTERNATIONAL/DAWSONSWNS
"Haionekani kama kulikuwa na ugomvi kati yao, walitengana tu kwa miaka," akaongeza.
Curran pia alisema vitu vingi vilivyopatikana kwenye makazi ya Thomson vilikuwa vitu vya Asia.
Alitafuta msaada wa kutathmini bei kutoka kwa Richard Harrison, mtaalam wa kampuni ya mnada Dawsons Auctioneers na Wathamini.
Hivyo basi, ni vitu gani binti huyu wa Indonesia atarithi?
Utajiri wa Thomson kwa ujumla unaokadiriwa kuwa zaidi ya pauni 400,000 na inajumuisha:
- Nyumba ya vyumba vitatu iliyopo mjini Ramsgate, Kent, iliyonunuliwa mwaka 2007 kwa gharama ya pauni 235,000
- Mtungi wa enzi za mfalme Guanzu wa karne ya 19, kwa thamani ya pauni 20,000.
- Meli inayodhaniwa kuwa kubwa zaidi ilipozinduliwa mwaka 1923.
- Mto wa mguu kutoka China unakadiriwa kuwa pauni 2,200,

Chanzo cha picha, FINDERS INTERNATIONAL
Curran alisema, "Kama anayeongoza kumtafuta mrithi , kazi yetu ni kupata jamaa ambao wanastahili kurithi kutoka kwa wale ambao wamekufa bila wosia na pia jamaa wanaofahamika wazi."
"Tunafurahi tuliweza kumtafuta binti ya Alexander, ambaye atarithi utajiri wake."
"Tunaamini hiki ndicho Alexander anataka."













