Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita ya Afghanistan: Baada ya Marekani kuondoa Majeshi yake haya ni maswali 10 kuhusu vita vya miongo miwili
Baada ya mzozo wa miaka 20, Marekani imeondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan. Kwa Marekani na washirika wake, kambi ya Bagram ya jeshi la anga ilikuwa kitovu cha vita dhidi ya Taliban and al-Qaeda.
Vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Marekani viliingia nchini humo Disemba mwaka 2001, na kambi hiyo ilitengenezwa kuwa kituo kikubwa chenye uwezo wa kuchukua hadi wanajeshi 10,000.
Sasa wameondoka, baada ya Rais Joe Biden kutangaza kuondoa vikosi vyote vya Marekani kufikia Septemba tarehe 11.
Wakati vikosi vysa Marekani vikiondoka, wanamgambo wa Taliban wanadhihirisha ushindi kwa kuendelea kuvamia maeneo tofauti ya Afghanistan, na kuteka maeeo kadhaa.
Gharama ya vita hivyo imekuwa kubwa ajabu -kimaisha na kifedha.
Lakini vita hivyo vilihusu nini, na je Marekani ilifikia lengo lake? Yapo maswali lukuki ya kujiuliza.
Kwanini Marekani iliivamia Afghanistan kijeshi?
Septemba 11, 2001, shambulio maarufu lilifanyika dhidi ya Marekani na kuua karibu watu 3,000, baada ya ndege zilizotekwa kuelekezwa kwenye jengo la World Trade Center mjini New York, Pentagon katika jimbo la Arlington, Virginia. Ndege ya nne iliangushwa katika kiwanja kimoja huko Pennsylvania.
Osama Bin Laden, kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda, baade alitambuliwa kuhusika na shambulio hilo.
Taliban, kundi la kijihadi lililoendesha Afghanistan na kumlinda Bin Laden, lilikataa kutoa ushirikiano. Kwa hivyo, mwezi mmoja baada ya shambulio la 9/11, Marekani ilifanya mashambulio ya angani dhidi ya Afghanistan kulikabili kundi hilo.
Nini kilifuata baadaye?
Ndani ya miezi miwili baada ya Marekani, washirika wake wa kimataifa na washirika wa Afghanistan kuanza mashambulizi hayo, utawala wa Taliban ulisambaratika na wapiganaji wake kukimbilia Pakistan. Lakini hawakutoweka kabisa - ushawishi wao uliendelea kuwepo, wakarejea nyumbani. Kundi hilo lilikuwa likijipatia mamilioni ya dola za Kimarekani kwa mwaka kutokana na biashara ya dawa za kulevya, uchimbaji madini na ukusanyaji kodi.
Serikali mpya inayoungwa mkono na Marekani iliingia madrakani mwaka 2004, lakini Taliban waliendeleza mashambulio hatari kwa miaka kadhaa. Vikosi vya kimataifa nchini Afghanistan vilikabiliwa na wakati mgumu na tishio kutoka kundi hilo llililopata nguvu mpya.
Mzozo huo uliiathiri vibaya Afghanistan, kiraia na kijeshi.
Je matatizo ya Afghanistan yalianza mwaka 2001?
Kwa ufupi jibu ni la.
Afghanistan ilikuwa nchi ambayo imezongwa na vita vya mara kwa mara kwa miongo kadhaa, hata kabla ya Marekani kuivamia kijeshi.
Mwishoni mwa miaka ya 1970, majeshi ya Sovieti yalivamia Afghanistan kusaidia serikali yake ya kikomunisti. Ilipigana na vuguvugu la mageuzi -linalojulikana kama mujahideen - ambayo iliungwa mkono na Marekani, Pakistan, China na Saudi Arabia, miongoni mwa nchi zingine.
Majeshi ya Sovieti yaliondoka nchini humo mwaka 1989, lakini vita vya wenyewe kwa wenyewe viliendelea. Katika ghasia zilizoliibua na kuzaliwa kwa nguvu kundi la Taliban (inayomaanisha "wanafunzi").
Kwa namna gani Taliban ilipata ushawishi mkubwa?
Taliban ilipata umaarufu katika eneo la mpaka wa kaskazini mwa Pakistan na kusini magharibi mwa Afghanistan mapema katika miaka ya 1990.
Waliahidi kukabiliana na ufisadi na kuimarisha usalama kwa watu wa Afghanistan, ambao baadhi yao walikuwa wameathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Bila kupoteza wakati waliimarisha umaarufu wao kwa kuanzisha na kuunga mkono adhabu ya sheria ya Kiislamu- kama vile kuuawa hadharani kwa wale waliokutwa na makosa ya mauaji na wazinifu na kukatwa mkono kwa wale waliopatikana na hatia ya wizi.
Wanaume walitakiwa kufuga ndevu na wanawake kuvalia burka, vazi maalum linalofunina uso na mwili mzima.
Taliban pia walipiga marufuku utazamaji watelevisheni, muziki na sinema, na kuwakataza wasichana walio na umri wa miaka 10 na zaidi kwenda shule.
Kundi hili la Taliban limetokomezwa?
Zaidi ya miongo miwili iliyopita, Taliban walinyongonyezwa tu, lakini hawakuangamizwa kabisa.
Mwishoni mwa mwaka 2014, kulishuhudiwa umwagikaji mkubwa wa damu nchini Afghanistan tangu mwaka 2001, vikosi vya kimataifa -kwa kuhofia kuendelea kukaa Afghanistan -vilikamilisha oparesheni ya kijeshi na kuiachia majeshi ya Afghan jukumu la kupambana na Taliban.
Lakini hatua hiyo iliipatia nguvu Taliban, kwani waliteka maeneo kadhaa na kufanya mashambuliz ya mabomu dhidi ya serikali na mengine kuwalenga raia.
Mwaka 2018, BBC ilibaini kuwa 70% ya Afghanistan, ilikuwa chini ya Taliban.
Je mzozo huo uligharimu nini?
Zaidi ya maafisa 2,300 wa jeshi la Marekani wakiwemo wanawake waliuawa na wengine zaidi ya 20,000 kujeruhiwa pamoja na Waingereza 450 na mamia ya wengine kutoka nchi mbalimbali.
Lakini raia wa Afghanistan ndio waliathirika zaidi, baadhi ya tafiti zinaonyesha zaidi ya maafisa 60,000 wa vikosi vya uaslama waliuawa.
Karibu raia 111,000 waliuawa au kujeruhiwa tangu Umoja wa Mataifa (UN) ulipoanza kurekodi idadi ya waliojeruhiwa kuanza mwaka 2009, ilisema ripoti.
Kulingana na utafiti, mzozo huo unakadiriwa kuwagahrimu walipa kodi wa Marekani karibu dola trilioni moja.
Mwezi Februari mwaka 2020, Marekani na Taliban walisaini "mkataba wa amani" kwa Afghanistan hiyo ilikuwa baada ya miaka kadhaa.
Chini ya mkataba huo Marekani na washirika wake wa Nata ilikubali kuondoa vikosi vyao vyote nchini humo kwa makubaliano ya Taliban kutoruhusu al-Qaeda au makundi mengine yenye itikadi kali kuhudumu katika maeneo wanayoshikilia.
Kama sehemu ya mazungumzo ya mwaka jana, Taliban na serikali ya Afghanistan ziliwaachilia huru wafungwa wa kiviita.
Karibu wanamgambo 5,000 wa Taliban waliachiwa huru katika miezi iliyofuatia baada ya makubaliano hayo.
Marekani pia iliahidi kuondoa vikwazo dhidi ya Taliban na kufanya kazi na UN kuondoa vikwazo dhidi ya kundi hilo.
Marekani ilijadiliana moja kwa moja na Taliban, bila uwepo wa serikali ya Afghan. "Muda umewadia baada ya miaka hii yote kuwarejesha nyumbani watu wetu," aliyekuwa rais wakati huo Donald Trump alisema.
Je vikosi vya Marekani kuondoka vyote?
Vikosi vya mwisho vya Marekani na Nato viliondoka kambi ya wana anga ya Bagram, na kuachia serikali ya Afghan jukumu la usalam.
Karibu wanajeshi 650 wa Marekani wanatarajiwa kusalia nchini humo, kulingana na shirika la habari la Associated Press.
Zaidi wanatarajiwa kutoa ulinzi kwa wanadiplomasia na kusaidikatika ulinzi wa uwanja wa ndeke wa Kimataifa wa Kabul.
Hali kwa sasa ikoje?
Tangu makubaliano kufikiwa, Taliban wameonekana kubadili mbinu zao za mashambulizi hatari mijini na msururu wa mauaji yanayolenga wanajeshi ambayo yamekuwa yakiwahangaisha raia wa Afghanistan.
Wamekuwa wakiteka maeneo kadhaa ya nchi, kwa mara nyingine wakitaka kuiondoa madarakani serikali ya Kabul baada ya mataifa ya kigeni kujiondoa.
Al-Qaeda pia wanaendelea kuendesha shughuli zao nchini Afghanistan, huku wanamgambo wa Islamic State wakifanya mashambulio nchini humo.
Wasi wasi umekuwa ukiongezeka kuhusu hatma ya baadaye ya Kabul, lakini Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani anasisitiza kuwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo kwamba vina uwezo wa kuwadhibiti wanamgambo.
Miongo miwili ya majeshi ya nje ndani ya Afghanistan ilikuwa na tija?
"Jibu inategemea kigezo kitakachotumika kutathmini hatua hiyo," Mwandishi wa BBC wa maswala ya usalama Frank Gardner anasema.
Vyanzo vya usalama vya ngazi ya juu vimeambia BBC kwamba tangu vita vilipoanza hakuna hata shambulio moja la ugaidi wa kimataifa lililofanikiwa kupangwa kutoka Afghanistan.
"Kwa hiyo, tukizingatia kigezo cha kukabiliana na ugaidi wa kimataifa, uwepo wa majeshi ya magharibi nchini humo umesaidia kufanikisha lengo hilo," Bw. Gardner aliongeza.
Lakini miaka ishirini baadaye, Taliban bado hawajashindwa na wanasalia kuwa kikosi hatari cha vita.