Mbinu zitakazotumiwa kupambana na Taliban baada ya Uingereza, Marekani na Nato kuondoa vikosi vyao Afghanistan

Vikosi vya vita vya Marekani, Uingereza na Nato vinaondoka Afghanistan msimu huu wa joto. Taliban wanazidi kuwa na nguvu kila uchao huku makundi ya al-Qaeda na Islamic State yakifanya mashambulio kwa ukakamavu .

Je ,makaundi hayo yatakabiliwaje wakati huu ambapo nchi za magharibi hazitakuwa na wanajeshi nchini Afghanistan?

Maafisa wa ujasusi wa Magharibi wanaamini bado makundi hayo yanapanga mashambulio ya kigaidi ya kimataifa kutoka maficho yao ya Afghanistan, kama vile Osama Bin Laden alivyofanya mnamokatik shambulio la 9/11.

Ni shida ambayo inaanza kuwasumbua wakuu wa sera za Uingereza wakati tarehe ya mwisho ya Septemba11 ya Rais wa Marekani Joe Biden kuyaondoa majeshi yake nchini humo inapokaribia. Mkuu wa ulinzi wa Uingereza, Jenerali Sir Nick Carter, alisema hivi karibuni: "Haya hayakuwa matokeo tuliyotarajia." Sasa kuna hatari kubwa kwamba mafanikio yaliyopatikana katika kukabiliana na ugaidi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, kwa gharama kubwa, yanaweza kutenguliwa wakati mustakabali wa Afghanistan unachukua sura isiyo na uhakika.

"Tatizo," anasema John Raine, mtaalam wa usalama wa katika Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Mkakati (IISS), "ni uwezekano hali kuharibika kwa kasi na kuwa kitu ambacho serikali ya Afghanistan, hata ikiimarishwa kwa mbali na Marekani , haiwezi kuthibiti. "

Hatahivyo, hii, kwa Rais Biden, ulikuwa ndio mpango wa kudumu. Alipotembelea nchi hiyo kama makamu wa rais katika utawala wa Obama mnamo 2009 na 2011 alifanya uamuzi kuwa ujenzi wa taifa ulikuwa ni kupoteza muda na badala yake Marekani inapaswa kuzingatia njia ya kukabiliana na ugaidi kwa kutumia mashambulizi ya angani na uvamizi wa vikosi Maalum. .

Pentagon haikubaliani na tathmini hiyo na Katibu wa zamani wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates alimuelezea Bwana Biden katika kumbukumbu yake kama "anayekosea karibu kila sera kuu ya kigeni na suala la usalama wa kitaifa kwa miongo minne iliyopita".

Kwa hivyo Marekani na washirika wake watakabilianaje na ugaidi nchini Afghanistan wanapojiondoa nchini humo kufikia mwezi septemba?

Kuimarisha mitandao ya kijasusi

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita CIA, MI6 na mashirika mengine ya ujasusi yamejenga uhusiano wa karibu wa kufanya kazi na Shirika la ujasusi la Afganistan NDS, na kuisaidia kutambua na kuondoa vitisho, wakati pia ikijaribu kuzuia njia kali za watu wengine. "Bado tutaweza kutoa msaada wa maana kwa NDS," afisa usalama wa magharibi wiki jana alisema, "ni kwamba tu mtindo wetu wa uendeshaji utalazimika kubadilika."

Ni sawa ufikiria kwamba Taliban mwishowe wataunda sehemu ya serikali ya baadaye ya Afghanistan. Je,mataifa ya Magharibi yatakuwa tayari kubadilishana habari za kijasusi nao baada ya miaka yote ya kupigana nao? "Hilo," afisa huyo alisema, "litakuwa jambo gumu sana kufikiria."

Swali muhimu ni ikiwa Taliban kweli ilichukua hatua ya kukatiza uhusiano na makundi ya IS na Al Qaeda kama ilivyowaambia wapatanishi wa amani huko Doha .Mahusiano hayo wakati mwingine ni ya kihistoria, ya ndoa na ya kikabila, yalitangulia hata mashambulio ya 9/11 nani ya miaka kadhaa iliyopita .

Taliban sio wajinga na wanafahamu fika kwamba Iwapo watakuwa sehemu ya serikali ijayo ya Afganistan lazima wajitenge na kundi lama Al qaeda ambalo limetajwa kama la kigaidi .

Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani

Mashambulizi haya yanaweza kuongezeka. Matumizi ya ndege zisizo na rubani, au droni yaliidhinishwa sana na utawala wa Obama ambao Joe Biden aliwahi kuwa makamu wa rais.

Katika maeneo ya mbali, ya makabila ya Pakistan yanayopakana na Afghanistan, na katika maeneo ya misitu ya Yemen, ambapo katika visa vyote viwili viongozi wakuu wa al-Qaeda walikuwa wamejificha, mashambulizi mfululizo ya ndege zisizo na rubani yalikuwa na "athari mbaya" kwa shughuli za kikundi hicho , kulingana na maafisa wa ujasusi .

Mashambulizi hayo yaliwalazimisha makamanda kuwa safarini kila wakati, bila kukaa zaidi ya usiku mmoja au siku mbili mahali pamoja, wakizuia uwezo wao wa kuwasiliana na hawajui kabisa ikiwa kuondoka kwa mgeni kutafuatwa na kombora la Moto wa Jehanamu, lililofyatuliwa na adui asiyeonekana .

Lakini matumizi ya droni yana utata. Yanaweza kuwa hatari - sio kwa mwendeshaji, kwa kweli, ambaye huwa anakaa kwenye kontena umbali wa maelfu ya maili kwenye uwanja wa ndege huko Nevada au Lincolnshire - lakini kwa raia katika eneo hilo.

Licha ya maelezo na picha zinazoonekana wazi kwa waendeshaji wa droni daima kuna hatari ya "uharibifu wa pembeni", hatari ya kuwasili kwa raia dakika ya mwisho kwenye eneo la tukio, kama ilivyotokea Iraq na Syria. Zaidi ya mara moja Wamarekani walikuwa wamempata mmuaji wa IS Mohammed Emwazi, al maarufu "Jihadi John", lakini ilibidi tu wasirushe makombora ya droni ili kuepuka kuwauawa raia .

Huko Yemen, mashambulizi ya droni hayapendi sana na wanaharakati wa haki za binadamu ambao wanadai kukusanyika kwa watu wa jamii zao kumekuwa kukikidhaniwa kuwa ni waasi wenye silaha. Lakini huko Djibouti, waziri wa mambo ya nje aliniambia anakaribisha matumizi ya droni dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab nchini Somalia na alikuwa tayari kusema hivyo kwenye kamera.

Vikosi maalum vya 'kukamata au kuua'

Mashambulizi ya wa usiku yaliyofanywa na timu ndogo za SBS au Kikosi Maalum cha Marekani, wakifanya kazi kutumia habari za ujasusi walizokusanya katika maeneo husika kuliyaacha na hasara kubwa makamanda wa makundi ya kigaidi .

Mara nyingi wanawasili kwa helikopta wakati wa usiku na kisha kufanya doria kwa miguu, timu hizi za "kukamata au kuua" zilifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Vikosi Maalum vya Afghanistan, kuzuia mashambulio mengi.

Lakini baada ya Septemba mashambulizi haya- ikiwa yataendelea kabisa - yatalazimika kuzinduliwa au angalau kupangwa kutoka nje ya nchi. Hatari ya kucheleweshwa kwa muda na onyo la mapema kutolewa kwa wengine bila shaka itakuwa kubwa. Na jukumu la kutafuta maeneo mapya ya kuzindua sio kitu kinachoweza kurekebishwa mara moja.

Kutafuta kambi mpya za kisiri

Kambi ya siri, mashariki mwa Afghanistan ambayo Vikosi Maalum vya Marekani vimekuwa vikitumia kama uwanja wa operesheni dhidi ya "Walengwa wenye thamani " inafungwa. Hii itakuwa habari njema kwa al-Qaeda na IS ambao sasa hawatakuwa na hofu kubwa kutokana na wanajeshi wa Marekani katikati ya usiku. Kwa hivyo ni wapi katika kanda hiyo ambapo sasa inaweza kuwa eneo mbadala la kuanzisha oparesheni kama hizo?

Pakistan ni eneo zuri kijiografia lakini kuna tuhuma kubwa huko Magharibi kwamba shirika la ujasusi nchini humo (ISI) huenda lina husiano na vikundi vya Kiislam vinavyofanya mashambulizi ya kila mara dhidi ya Wamarekani na washirika wao

Wakati CIA ilipozindua Operation Neptune Spear kumuua au kumkamata Osama Bin Laden mnamo Mei 2011, Marekani ilichagua kutowajulisha Pakistan wakati timu za kikosi maalum cha SEAL kilipotumia helikopta kupita angan ya Pakistani. Waliogopa mtu angempa Bin Laden habari na kumfanya kutoroka.

Badala yake, Oman inaweza kuwa ngome znuri . Pamoja na serikali yake thabiti, inayounga mkono Magharibi, taifa hilo tayari linashikilia vituo vikubwa vinavyotumiwa na Uingereza huko Thumrayt na hivi karibuni huko Duqm kwenye pwani ya Bahari ya Hindi. Duqm bado iko zaidi ya maili 1000 mbali na mpaka wa Afghanistan na ndege yoyote inayobeba wanajeshi bado itahitaji kupita juu ya anga ya Pakistan. Bahrain ni nchi nyingine nzuri inayoweza kutumika , ambapo Uingereza tayari ina kituo kidogo cha majini - HMS Juffair - na Meli ya 5 ya Jeshi la Wanamaji la Marekani lina kambi kubwa sana.

Halafu kuna Asia ya Kati ambayo inapakana na Afghanistan kaskazini. Katika miaka ya karibu ya mashambulizi ya 9/11, jeshi la Marekani lilitumia kituo cha zamani cha Soviet kusini-mashariki mwa Uzbekistan kiitwacho Karshi-Khanabad au "K2". Lakini ilijiondoa mnamo 2005 baada ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili kuzorota na kurejea , hata kwa mwaliko, kutzua mabishano kwani kituo hicho kiliripotiwa kuchafuliwa sana na kemikali na vifaa vyenye mionzi.

Ukweli ni kwamba kukabiliana na al-Qaeda na IS katika maeneo ya ndani mwa Afghanistan kunakaribia kuwa kugumu zaidi.

Hakuna njia nyingine rahisi isipokuwa kuwa na wanajeshi nchini Afghanistan ambao wanaweza kupewa notisi haraka na kuingia vitani bila kungoja kwa muda mrefu kutayarishwa au kusafirishwa kutoka nchi jirani .

Mengi sasa yatategemea matayarisho na ufanisi wa serikali zinazoendelea za Afghanistan kukabili vikundi hivi vya ugaidi na vilivyopigwa marufuku .

Kwasababu ya hali itakavyokuwa tete ,ni bora kuhitimisha kwamba mambo hayatakuwa mazuri katika nchi hiyo na kampeini za kupambana na ugaidi zitavurugika kabisa kwani haitakuwa kazi rahisi kurejea tena na kuyamaliza nguvu makundi ya kigaidi katika taifa hilo na kanda nzima .