'Walijaribu kumuua mama yangu mbele yangu mara mbili'

Shuhra Koofi alikuwa na wasiwasi. Mama yake , ambaye amekuwa mbunge nchini Afganistan kwa mihula miwili, alikuwa amepigwa risasi alipokuwa akisafiri kurudi mjini Kabul kwa gari.

Shuhra alimsihi mama yake, Fawzia Koofi, asifunge macho yake ''nitafanya nini bila wewe?'' aliuliza.

''Nilikuwa nina hofu kwa sababu nilidhani nimempoteza mama yangu,'' Shuhra aliiambia BBC, kuhusu jaribio la mauaji mwezi uliopita. ''Lakini baadae nikajikaza kwa kuwa alikuwa akihitaji msaada wangu.''

Fawzia Koofi ni mkosoaji mkubwa wa Taliban katika meza ya mazungumzo. Amekutana na athari kubwa kutokana na kujihusisha na siasa.

-Majaribio mawili ya kuuawa, yote yaliyoshuhudiwa na binti yake.

Mwaka 2010, msafara wake ulivamiwa na Taliban, na mwezi Agosti mwaka huu alipigwa risasi barabarani na watu wasiojulikana

Tarehe 14 mwezi Agosti, Shushra na mama yake walikuwa wakirejea mjini Kabul baada ya kuzuru jimbo la Parwan, Kaskazini mwa mji mkuu wa Afghanistan ndipo walibaini kuwa kulikuwa namagari mawili yaliyokuwa yakiwafuata.

Walihisi kuwa wanakaribia kuwavamia.

''Kabla ya shambulio, gari jeusi lilituzuia na dereva wetu alipiga honi ,'' Shuhra alisema.'' Kisha tukasikia milio ya risadi kutokea nyuma-upande aliokuwa amekaaa mama yangu.'' Kulikuwa na risasi mbili, Shuhra alisema. Ya kwanza iliikosa gari yao.

Shuhra alikuwa amekaa karibu na Fawzia kwenye kiti cha nyuma. Alijaribu kumkinga kichwa mama yake na kumwambia abonyee chini ya kiti wakati dereva akikimbiza gari. Hakuwaona washambuliaji.

''Ilitupasa kuondoka kabisa vinginevyo wangetushambulia tena,'' alisema.

Mnamo mwaka 2010 , Fawzia na Shuhra walikuwa wakisafiri mwenye gari kupitia Nangarhar jimbo lililo Afghanistan . Fawzia tayari alikuwa mmbunge na mshirika wa karibu wa Rais wa kipindi hicho , Hamid Karzai.

Wakati wakiwa katika msafara mdogo, ilishambuliwa.

''Nilikuwa na miaka 10 wakati huo. Nilikuwa nakaa kwenye gari katikati ya mama yangu na dada yangu,'' Shuhra alisema. Ninakumbuka kelele za risasi. Zilikuwa za mfululizo.''

Fawzia alinusurika na tukio hilo na polisi waliusindikiza msafara mpaka kwenye eneo salama ambapo walipanda ndege kuelekea Kabul.

Taliban ilidai kuhusika na uvamizi huo.

''Ilikuwa rahisi kukubali hilo kwa sababu tulijua ni nani anayehusika,'' Shuhra alisema. '' Mara ya pili, washambuliaji hawakufahamika na hakuna aliyekuwa akiwajibika, hiyo ilikuwa ngumu zaidi na ilikuwa ikiiweka familia katika hofu kubwa.''

Mwanamke aliyefanya mazungumzo na Taliban

Kama fawzia, mabinti zake wawili walikua wakishuhudia machafuko mabaya katika jamii. Wakati mwingine mtu wa familia yao alikua mmoja wa waathirika.

Babu yake Shuhra pia alikuwa mbunge na aliuawa na wanamgambo .

Baba yake aliugua ugonjwa wa kifua kikuu baada ya kufungwa na wanamgambo wa Taliban kisha alifariki wakati Shuhra akiwa mdogo.

Fawzia aliwalea mabinti zake huku akiendelea na kazi yake ya siasa.

''Wakati wote nilikuwa na hofu ya kupoteza mtu mmoja wa familia yangu na sikuwa na uzoefu kabisa wa maisha ya kawaida,'' Shuhra alisema.

Sekunde kadhaa baada ya mashambulizi mwezi Agosti, mama yake alimtazama na kusema , ''ninafikiri nimejeruhiwa'', Shuhra alikumbuka. Wakati ambao ''hatausahau''.

Baada ya hapo, Fawzia hakusema lolote. Risasi ilipita kwenye gari kutokea nyuma ya gari, ikapenya kwenye kiti na kumpata Fawzia kwenye mkono , chini ya bega lake la kulia.

''Nilifikiri ningempoteza. Niliendelea kumwambia, 'Tafadhali usifunge macho, zungumza na mimi, na nilijaribu kumfanya aendelee kuwa macho ,'' Shuhra alisema. '' Nililaza kichwa changu na chake na nikamwambia, nikamwambia 'Usitazame juu, wanaweza kufyatua tena risasi.''

Fawzia alikuwa ametoka kupona virusi vya Covid-19 na anakabiliwa na upungufu wa madini ya chuma. Shuhra alivua skafu ili kujaribu kuzuia damu kuendelea kutoka.

''Giza lilikua limeingia na sikuweza kuona jeraha lake. Lakini nilipoendelea kumfunga skafu , mikono yangu ilikuwa inajaa damu ,'' Shuhra alisema.

Walifika hospitalini baada ya dakika 40. Vipimo vya CT scan viwili viliweza kuwasaidia madaktari kugundua risasi na kuitoa kutoka kwenye mkono wa Fawzia. Aliruhusiwa kutoka hospitalini baada ya juma moja na sasa anaendelea vizuri.

Mkosoaji wa Taliban

Fawzia Koofi amekuwa akiwatetea wanawake wa Afghanistan ambao sauti zao zimekuwa zikipuuzwa kwa kiasi kikubwa. Alipokaa na Taliban mwaka jana, aliwataka Taliban kuruhusu wapatanishi wanawake kwenye mazungumzo ya amani. Wawakilishi wa Taliban waliangua kicheko baada ya kutolewa hoja hiyo.

Anaendelea kuwa mshiriki mzuri kwenye mazungumzo ya amani kati ya serikali na Taliban, mazungumzo yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa juma hili. Anashuku wale wanaopinga amani ndio waliohusika na shambulio la hivi karibuni dhidi yake.

Taliban wamekataa kuhusika na tukio hilo. Makundi mengine yenye silaha pia wamekuwa wakifanya operesheni zao kwenye eneo ambalo shambulio lilitokea.

Shuhra alisema yeye na mama yake walifadhaishwa sana na tukio hilo.

''Amesikitika sana kwasababu anafikirikuwa amewasaidia watu wake na amekuwa akijiuliza kwanini baadhi ya watu wanataka kumuaa.'' Alisema Shuhra.

Afghanistan inatazamwa kama eneo ambalo ni hatari kwa wanawake na wanasiasa wa kike bado wanapata vikwazo vingi.

Fawzia na dada yake Mariam walikuwa miongoni mwa wale waliozuiwa kugombea katika uchaguzi wa ubunge mwaka 2018 .

Shuhra alijua ugumu ambao mwanamke anaweza kukutana nao, hasa baada ya kuona maoni yasiyopendeza kumhusu mama yake katika magazeti na mitandao ya kijamii, lakini anasoma sayansi ya siasa American University cha Afghanistan kilicho mjini Kabul.

''Siku zote nilitaka kujihusisha na siasa. Ninafuata njia ya mama yangu, alisema. Shuhra na dada yake kwa pamoja walimtia moyo mama yao kuendelea na siasa pamoja na changamoto ya mashambulizi .

''Tumechagua njia hii na tutaendelea,'' alisema.