Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siku ya Mashujaa: Tanzania 'ilivyovichakaza' vikosi vya Gaddafi vilivyojaribu kumsaidia Idi Amin Uganda
Vita vya Uganda-Tanzania, vinavyojulikana nchini Tanzania kama Vita vya Kagera na nchini Uganda kama vita vya Ukombozi vilihusisha Uganda na Tanzania kati ya Oktoba 1978 hadi Juni 1979. Matokeo yake yalikuwa kutimuliwa kwa Idi Amin madarakani na mwezi kama huu wa Juni 1979 ambapo vita viliisha tunakupakulia kumbukumbu za chanzo na matokeo ya vita hivyo . Leo katika sehemu ya pili ya makala zetu tunaangazia jinsi Tanzania ilivyojibu mapigo baada ya Amin kuvamia na kutwaa sehemu ya nchi hiyo.
"Uwezo wa kumpiga (Idi Amin) tunao, sababu ya kumpiga tunayo na nia ya kumpiga tunayo," bila shaka hii ni moja ya nukuu maarufu zaidi ya aliyekuwa rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Ni nukuu pia ambayo ilibeba, nia, dira na ari ya vikosi vya Tanzania na washirika wao toka ilipoamuliwa kuwa vita dhidi ya Idi Amini haiepukiki tena. Hilo lilikuwa tangazo rasmi la vita.
Hata hivyo, mwanzoni mwa vita hivyo, taarifa kwa wananchi juu ya kile kilichokuwa kinaendelea mkoani Kagera zilikuwa zinaminywa na serikali ya Tanzania. Kwa upande wa Uganda, redio ya nchi hiyo ilikuwa ikifanya propaganda ya kuilaumu Tanzania na kujitangazia ushindi hata pale ambapo hapakuwa na ushindi.
Wakati mapambano yalipolipuka mpakani baina ya vikosi vya Idi Amini na Tanzania toka Oktoba 9 mwaka 1978, hakukuwa na taarifa yeyote rasmi iliyotolewa kwenye vyombo vya habari vya Tanzania.
Taarifa pekee katika siku hizo za wali za vita hivyo ilitolewa na Redio Tanzania mnamo Oktoba 31, katika taarifa ya habari ya saa moja asubuhi. Msoma habari alitangaza kuwa sehemu ya Tanzania imevamiwa na kukaliwa na majeshi ya Uganda na mipango ilikuwa ikifanyika ili kuyafurusha majeshi vamizi.
Tanzania yakomboa eneo lake
Kufikia wiki ya pili ya mwezi Novemba 1978, vikosi vya kutosha vya wanajeshi wa Tanzania vilifika katika uwanja wa mapambano kusini mwa mto Kagera. Vikosi vya Tanzania vilirusha mamia ya makombora usiku na mchana kuelekea eneo la kaskazini mwa mto Kagera ambalo lilikuwa chini ya Idi Amin.
Makombora hayo yaliwafanya wapiganaji wa Amin kulikimbia eneo hilo, na kufikia Novemba 19, vikosi vya Tanzania vilifanikiwa kufunga daraja la muda la kivita ili kuruhusu magari ya kivita, vifaru na wanajeshi kuvuka mto Kagera.
Vikosi vya Amin awali vililipua daraja la awali ili kuzuia vikosi vya Tanzania kuvuka mto huo.
Kufifikia Novemba 22, vikosi vya Tanzania vilifanikiwa kulirudisha eneo lote lililovamiwa na majeshi ya Uganda. Maelfu ya raia wa Tanzania ambao walinusurika katika mapambano hayo walijitokeza kutoka katika misitu na vichaka walimojificha kwa wiki tatu na kuwalaki wapambanaji wao waliowakomboa.
Baada ya kuyasukuma majeshi ya Amin mpaka nje ya mpaka wa Tanzania, Mwalimu Nyerere alitembelea mstari wa mbele wa mapambano,ili kujjionea hali halisi. Baada ya mazungumzo na makamanda wake wakafikia muafaka kuwa eneo la Kagera halitakuwa salama mpaka vikosi vya Uganda vilivyokuwa katika eneo la Mutukula visambaratishwe.
Kwa miezi miwili, vikosi vya Tanzania na Uganda vilipigana katika mashambulizi madogo na ya kushtukiza.
Majeshi ya Tanzania yaingia Uganda
Januari 21 vikosi vya Tanzania vilivuka mpaka wa Uganda na kuingia katika mji mdogo wa Mtukula. Vikosi hivyo vilijigawa katika makundi matatu, kikosi kimoja kikipita njia ya wazi na kuonekana na adui, vikosi viwili vilivyosalia vikajificha.
Wakati vikosi vya Uganda vikikishambulia kikosi kilichokuwa kimepita njia ya kawaida, ghafla wakajikuta wanashambuliwa kutoka pande nyengine mbili ambazo hawakutarajia. Hali hiyo ilisababisha wakimbie haraka na kuuacha mji wa Mtukula kwenye mikono ya Watanzania.
Mpaka kufikia wakati huo, Umoja wa Afrika (OAU) ulishindwa kupatanisha mgogoro huo kidiplomasia. Tanzania iliitaka OAU japo iilaani Uganda kwa kile ilichokifanya, kuivamia Tanzania, kunyakua sehemu ya ardhi yake na kutangaza kuwa ni sehemu ya Uganda. OAU haikufanya hivyo.
Tanzania pia ilitaka Amin kuondoa madai kuwa eneo la mpaka kati ya mataifa hayo ni mto Kagera, Amin naye hakufanya hivyo. Kushindikana kwa mambo hayo mawili kukaifanya Tanzania kutokuwa na njia nyengine zaidi ya kuendelea kupambana na majjeshi ya Amin.
Awali, wakuu wa makundi ya waasi na wapinzani wa Idi Amin kutoka nchni Uganda ambao walikuwa uhamishoni ikiwemo nchini Tanzania yalimhakikishia Nyerere kuwa wangeweza kukusanya wapambanaji wa kutosha ili kuongoza vita ndani ya Uganda.
Raisi ambaye Amin alimpindua madarakani, Milton Obote ndiye alikuwa mpinzani maarufu zaidi na alikuwa amehifadhiwa Tanzania toka apinduliwe. Rais wa sasa wa Uganda, Yoweri Museveni alikuwa mmoja wa makamanda wa waasi walioshiriki vita hivyo kutoka mstari wa mbele. Japo, waasi hao hawakupata wapiganaji wengi kama walivyoahidi ama kutarajjia, hata hivyo walishiriki kikamilifu vita hivyo bega kwa bega na majeshi ya Tanzania.
Jeshi la Tanzania lawashinda wapiganaji Uganda,Libya na PLO
Katika miezi ya awali ya 1979, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na washirka wao wa Uganda walifanikiwa kuikamata miji miwili mikubwa ya kusini ya Uganda, Masaka na Mbarara kufuatia mapambano kadhaa ambayo wanajeshi wa Amin waliyashindwa.
Wakati TPDF ikijiandaa kusafisha njia ya kwenda Kampala, mji mkuu wa Uganda, Muammar Gaddafi, kiongozi wa Libya na mshirika wa Amin, alituma mamia ya wanajeshi kwenda Uganda kusaidia Jeshi la Uganda.
Chama cha Ukombozi la Palestina, PLO pia kilituma wapiganaji kadhaa kumsaidia Amin. Toka walipoingia Uganda wanajeshi wa Tanzania waligundua maiti za wapiganaji wenye asili ya kiarabu katika maeneo ambayo walimshinda Amini mpaka kufikia Masaka. Japo uongozi wa jjuu wa PLO ulikanusha kupeleka wapiganaji Uganda na hata kumtuma mwakilishi wao Tanzania kwenda kusisisitiza kuwa hkuna wapiganajji Uganda, uhalisia ni kuwa kundi hilo lilimchukulia Amin kama rafiki. PLO baadae walikiri kuwa na kmakamanda wao Uganda, lakini walisema hao walikuwa ni washauri wa kijjeshi na si wapiganaji wa mstari wa mbele.
Nyerere hakuwalaumu PLO kwa kushiriki vita hivyo upande wa Amin, badala yake aliendelea kuilaumu umuiya ya kimataifa kwa kuendelea kuitelekeza Palestina mpaka kulazimika kutengeneza urafiki na dikteta kama Amin.
Baada ya kutekwa kwa Masaka na Mbarara na vikosi vya Tanzania, Amin na Kanali Gaddafi walikuwa wakizungumza kila siku, huku misaada ya silaha na wanajjeshi kutoka Libya pia ikiingia Uganda kwa wingi ili kuzuia wanajeshi wa Tanzania wasisonge mbele zaidi.
Mpambano mkubwa zaidi baina ya vikosi vya Tanzania washirika wake pamoja na vikosi vya Uganda na Libya ulitokea mwezi Machi katika eneo la Lukaya. Vikosi vya Tanzania vilitakiwa kushinda mpambano huo ili viuteke mji mkuu wa Uganda Kampala, huku vikosi vya Amin na Libya vilkitaka kushinda ili kuyarudisha nyuma majeshi ya Tanzania na kuurejjesha mikononi mwao mji wa Masaka.
Awali, vikosi vya Tanzania na washirika wake viliukamata mji huo baada ya kufanya mashambulizi ya makombora Machi 10. Vikosi vya Libya na Uganda vilikuwa Kaskazini ya mji huo na vilipewa amri na Amin kuwa viurejeshe mji wa Masaka mikononi mwake baada ya siku mbili. Punde tu baada ya kuviona vikosi vya Tanzania, vikosi vya Libya vilifyatua makombora ya roketi aina ya Katushka. Japo makombora hayo hayakuwapata, lakini mlio wake mkubwa na wakuogofya uliwafanya baadhi ya wapiganajji watanzania kushika nia na kwenda kujjificha.
Majjeshi ya Amin na Libya vikaurejesha mikononi mwake mji wa Lukaya. Endapo vikosi hivyo vingeshika njjia na kuelekea kusini vingeweza pia kuukomboa mji wa Masaka kama alivyoamuru Amin.
Vikosi vyote vya Tanzania vikapewa amri ya kujjikusanya na kwenda Lukaya ili kuokoa hali na kuzuia balaa zaidi kutokea. Vikosi vya Tanzania vikwazunguka maadui zao na kuwashambulia kutoka mbele na nyuma. Vikosi vya Libya na Uganda vilisalimu amri na kukimbia. Mpambano wa Lukaya ulipoisha, takriban wapiganajji 200 wa Libya waliuawa na wengine 200 wa Uganda kuuawa. Wanajeshi nane wa Tanzania pia waliuawa.
Ushindi wa Lukaya ukafungua njia kwa Tanzania kuelekea Kampala.
Usikose sehemu ya tatu ya makala hizi kesho Juni 30 kuhusu Vita ya Kagera ama Vita ya Ukombozi ambapo tutaangazia jinsi majeshi ya Tanzania na washirika wake walivyouteka mji mkuu wa Uganda, Kampala.