Virusi vya corona: Liberia yatumia dola 71,000 kwa ajili dawa ya mitishamba kutoka Madagascar

Muda wa kusoma: Dakika 1

Liberia imetumia $ 71,000 kusafirisha masanduku matatu madogo yaliyokuwa na dawa ya mimea iliyotengenezwa Madagascar ambayo ilitajwa kuwa tiba ya Covid-19, wizara ya afya imesema.

Hatua hiyo umezua utata nchini, haswa baada ya wizara kubadilisha taarifa yake ya hapo awali kwamba tonic ilikuwa msaada kutoka kwa serikali ya Madagascar na kwamba serikali ya Liberia ililipa tu gharama za kusafirisha masanduku matatu madogo.

Video ya Rais George Weah akipokea kundi kwenye uwanja wa ndege mwaka mmoja uliopita mwezi huu, ilisambaa mitandaoni.

Ufanisi wa dawa hiyo ya mitishamba haujathibitishwa licha ya majaribio kadhaa.

Madagascar, ambayo hapo awali ilitegemea dawa hiyo, sasa imepata chanjo zilizoidhinishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni.

Haijulikani kama mamlaka za Liberia zimetoa dawa hiyo ya mitishamba kwa Umma.

Hii ni kashfa ya hivi karibuni iliyokumba utawala wa Bw Weah kuhusu madai ya matumizi mabaya ya pesa za Umma.

Mnamo mwezi AprilI mwaka jana Madagascar ilizindua dawa ya mitishamba ya maradhi ya Covid-19 ambayo ilisambazwa nchini humo.

Mizigo kadhaa ya dawa hiyo ya Covid Organic pia ilitumwa kwa makumi ya mataifa barani Afrika.

Hatahivyo uwezo wa kinywaji hicho umepuuziliwa mbali na wataalamu wa Afya katika nchi kadhaa zikiwemo Nigeria na DR Congo mataifa ambayo yalifanyia majaribio dawa hiyo.